Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Inakadiriwa kwamba watu milioni 200, ambao ni asilimia 5 ya idadi ya watu ulimwenguni walio kati ya umri wa miaka 15 na 64, walitumia dawa haramu mwaka uliopita.—2005 WORLD DRUG REPORT, IDARA YA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU DAWA ZA KULEVYA NA UHALIFU.

Uchunguzi unaonyesha kwamba kuna uwezekano mara mbili wa kijana kufanya uhalifu katika muda wa miaka miwili baada ya kushuhudia jeuri inayohusisha kutumia bunduki.—GAZETI SCIENCE, MAREKANI.

Huko São Paulo, Brazili, asilimia 16.8 ya wanawake waliopatikana na kansa ya matiti katika hospitali moja katika kipindi cha mwaka mmoja walikuwa na umri wa chini ya miaka 35. Kuna uwezekano mkubwa wa kansa hiyo kutibiwa ikigunduliwa mapema. —FOLHA ONLINE, BRAZILI.

Kukabiliana na Uchoshi

Watafiti wanaochunguza uchoshi wanasema kwamba uchoshi ni “mojawapo ya magonjwa makubwa ya enzi yetu,” linaripoti gazeti The Vancouver Sun. Uchunguzi mmoja uligundua kwamba “watu watatu hivi kati ya wanne wanaoishi Amerika Kaskazini wanasema wangependa kufanya mambo mapya yenye kupendeza maishani.” Baadhi ya mapendekezo ya kukabiliana na uchoshi ni: “Fanya mabadiliko katika maisha yako ili usifuate mpangilio uleule wa kufanya mambo,” “jifunze jambo jipya,” fanya “kazi ya kujitolea,” “fanya mazoezi, kama vile . . . kutembea,” na “jifunze kushukuru.”

Utumwa wa Kisasa

Uchunguzi uliofanywa na Shirika la Wafanyakazi Ulimwenguni la Umoja wa Mataifa (ILO) unaripoti hivi: “Angalau watu milioni 12.3 ulimwenguni wanafanya kazi za kulazimishwa.” Inakadiriwa kwamba, zaidi ya watu milioni 2.4 kati ya hao ni wahasiriwa wa walanguzi wa wanadamu. Baadhi ya kazi au huduma ambazo mtu hulazimishwa kufanya chini ya vitisho ni ukahaba, kazi za jeshi, na kazi ya dhamana ambayo wafanyakazi hupata mshahara kidogo au hawapati kwa sababu unachukuliwa ili kulipia deni. Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa ILO Juan Somavia, kazi kama hizo “huwanyima watu haki zao za msingi na heshima.”

Biblia ya Kwanza Kamili Katika Lugha ya Krioli

Gazeti The Sydney Morning Herald linaripoti kwamba “tafsiri ya kwanza ya Biblia kuanzia Mwanzo hadi Ufunuo katika lugha moja ya kienyeji nchini Australia imekamilishwa.” Tafsiri hiyo mpya katika lugha ya Krioli, ambayo itatolewa mnamo 2007, itawafaidi wenyeji wa asili wa Australia wapatao 30,000 walio katika maeneo ya mbali ya Australia Kaskazini. “Mradi huo ulianzishwa miaka 27 iliyopita,” linasema gazeti hilo. Kulingana na Muungano wa Vyama vya Biblia, “tafsiri mpya 22 za Agano Jipya ziliandikishwa mnamo 2004.” Sasa Biblia inapatikana ikiwa nzima au kwa sehemu katika lugha na lahaja 2,377.

Halijoto Ndani ya Magari Yaliyoegeshwa

Gazeti Pediatrics linasema kwamba mnamo 2004, huko Marekani watoto 35 walikufa kutokana na joto jingi walipoachwa ndani ya magari yaliyoegeshwa. Uchunguzi mbalimbali unaonyesha kwamba halijoto nje inapokuwa nyuzi 30 Selsiasi, halijoto ndani ya gari inaweza kwa urahisi kufikia nyuzi 57 hadi 68 Selsiasi. Hata wakati halijoto nje ni nyuzi 22 Selsiasi, halijoto ndani ya gari inaweza kupanda kwa nyuzi 22, na halijoto hiyo itapanda dakika 15 hadi 30 baada ya gari kuegeshwa. Kufungua dirisha sentimeta nne au kuwasha feni kabla ya kuzima gari hakukutokeza tofauti yoyote. Waandishi wa makala hiyo wanaamini kwamba kufahamisha umma hatari zinazohusika kunaweza kuokoa uhai.