Kuwatafuta Mouflon
Kuwatafuta Mouflon
Tukiwa na ramani, kamera, kofia, na viatu vigumu, tunaingia ndani ya gari letu linaloendeshwa kwa magurudumu manne na kuondoka asubuhi moja. Tunaelekea Msitu wa Paphos ulio juu katika safu ya milima Troodos, katika kisiwa cha Saiprasi, ambako tunatumaini kuona wanyama wanaoitwa mouflon ambao hawapatikani kwa urahisi. Hawa ni wanyama gani?
MOUFLON ni aina ya kondoo-mwitu. Wengine wa jamii yao wanaweza kupatikana katika eneo lote la Mediterania. Lakini mnyama tunayetamani sana kumwona ni mouflon wa kienyeji wa Saiprasi anayesemekana kuwa maridadi kama mbawala na mwepesi kama mbuzi. Wataalamu humwita Ovis gmelini ophion, nao wenyeji wa Saiprasi humwita agrinó. Anaweza kupatikana tu katika sehemu za mbali za milimani.
Tunatoka kwenye barabara kuu, na kuelekea sehemu ya chini ya milima kisha kupitia bonde maridadi. Kuna vijiji kwenye mlima, nayo miti ya matunda imepandwa katika bonde hilo. Hata hivyo, barabara inaanza kuwa mbaya, na katika sehemu fulani gari letu linakaribia sana ncha ya miamba iliyoinuka. Mwishowe, tunafika mahali tunakoelekea, yaani, kituo cha msituni. Tuko ndani sana ya Msitu wa Paphos wenye ekari 150,000 ya misonobari na mierezi. Tunanunua kahawa na kuzungumza na Andreas, mtunza-misitu mwenye sare ya rangi ya kijani ambaye anazungumza kwa hisia nyingi kuhusu mouflon.
Anasema kwamba mouflon ndio wanyama wakubwa zaidi wanaonyonyesha nchini Saiprasi. Zamani kulikuwa na mouflon wengi sana katika kisiwa hicho. Sanaa nyingi za Ugiriki na Roma humwonyesha huyo kondoo-mwitu, na maandishi ya enzi za kati hufafanua jinsi watawala walivyofurahia kuwawinda katika Msitu wa Paphos.
Anapotuelekeza katika sehemu iliyozingirwa, Andreas anatueleza kuhusu historia ya mouflon. Kwa mfano, tunajifunza kwamba idadi ya wanyama hao ilianza kupungua sana bunduki ya kuwinda ilipovumbuliwa. Ilikuwa hivyo hadi katika mwaka wa 1938, wakati sheria za uwindaji za Saiprasi zilipobadilishwa tena ili kulinda mnyama huyo. Watunza-misitu na polisi walishirikiana kupunguza uwindaji haramu. Mwaka mmoja baadaye ilitangazwa kwamba wawindaji hawakuruhusiwa katika msitu huo. Mabadiliko hayo pamoja na hatua nyingine ambazo zilichukuliwa tangu miaka ya 1960, zimefanya idadi ya mouflon kuongezeka sana.
Twawaona kwa Mara ya Kwanza
Tunamfuata Andreas kwenye sehemu iliyozingirwa na kuchungulia katikati ya vichaka na miti. Huku akitoa ishara kwamba tusipige kelele, Andreas anatuongoza hatua fupi kwenye mwinuko fulani. Hapo tunawaona
mouflon watatu wakubwa wa kike na watoto wawili wakila katika eneo lililo wazi ambalo limezungukwa na miti. Wale wakubwa wana kimo cha sentimeta 90 hivi, na manyoya yao yana rangi hafifu ya kahawia.Mimea ya mwitu ambayo wao hula inapatikana kwa wingi wakati huu wa mwaka hivyo wale wakubwa wanashughulika hasa na kula bila kutukazia fikira sana. Hata hivyo, wale wachanga wanaacha kurukaruka na kupiga hatua chache kutuelekea. Tunasisimuka! Lakini kamera moja inapolia tu na kuwashtua, wote wanapotelea kwenye msitu kama umeme.
Kwa kuwa tumesisimuka kuwaona, tunapanga kutembea kwa mguu ili tuweze kuwakaribia. Andreas anapendekeza kwamba tutoke mapema asubuhi, wakati ambapo wanyama hao huja karibu sana na ukingo wa msitu ili kutafuta chakula. Kwa kuwa tunapanga kupiga hema katika bonde usiku, mlima ulio juu ya bonde hilo unaonekana kama mahali pazuri pa kuwatafuta. Tunajifunza kwamba mouflon hupatikana sana katika maeneo ya juu wakati wa majira ya joto. Katika majira ya baridi kali, wakati ambapo vilele huwa na barafu, wao hutafuta mimea wanayoweza kula katika sehemu za chini zilizoinuka, hata nyakati nyingine wakitokea katika maeneo yaliyo wazi.
Mouflon huzalisha baada ya miezi yenye joto kupita. Wakati wa kiangazi wao hutembea wakiwa makundi ya kati ya wanyama 10 hadi 20. Wanapozaa katika mwezi wa Aprili au Mei, makundi hayo hugawanyika na kuwa madogo, kama kundi lile tuliloona. Kwa kawaida, mouflon wakubwa wa kiume hulisha peke yao.
Kondoo-dume Mwituni!
Mapema asubuhi inayofuata, tunaelekea juu ya mlima, tunaacha gari katika eneo lililozungukwa na miti, na kuingia msituni kabla jua halijachomoza sana. Msitu bado umetulia, na kuna ukungu katikati ya miti. Tunaposimama ili kufurahia utulivu huo, tunamwona mouflon dume, mwenye kuvutia, na mwenye misuli ambaye amepoteza manyoya mengi ambayo huwa nayo wakati wa majira ya baridi kali. Ana manyoya meusi shingoni. Akigeuza kichwa chake kwa majivuno, anatutazama kupitia kope zake nyeusi na kunusa hewa ili kutambua harufu yetu. Tunakadiria kwamba kila moja ya pembe zake zilizojipinda ina urefu wa sentimeta 40 hivi! Ni mzito kuliko mouflon wa kike tuliowaona jana na lazima awe na uzito wa kilogramu 35 hivi.
Tunasimama tuli, bila hata kuvuta pumzi. Hata hivyo, ni kana kwamba tayari mnyama huyo mwenye hadhari amehisi harufu yetu kwani anainua kichwa chake na kukimbia kuelekea chini ya mlima. Mambo ambayo tumeona na kujifunza katika siku mbili yametupendeza kwelikweli. Pia tumemthamini zaidi Muumba, ambaye alisema: “Kila mnyama wa mwituni ni wangu, wanyama walio juu ya milima elfu moja.”—Zaburi 50:10.
[Picha katika ukurasa wa 25]
“Mouflon” wa Saiprasi (nyuma) na “Mouflon” wa Ulaya
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]
Top right: Oxford Scientific/photolibrary/Niall Benvie; European Mouflon: Oxford Scientific/photolibrary