Paradiso Katika Kisiwa cha Mchanga
Paradiso Katika Kisiwa cha Mchanga
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA
MNAMO 1770, mvumbuzi Mwingereza Nahodha James Cook alisafiri kwa meli hadi pwani ya mashariki ya Australia. Kilometa 150 hivi kaskazini ya jiji la kisasa la Brisbane, alipita ufuo wenye mchanga wa kisiwa fulani kikubwa ambacho baada ya muda kingewavutia wageni 300,000 kila mwaka. Hata hivyo, Cook hakujishughulisha nacho. Yeye na wengine walidhani kuwa eneo hilo lilikuwa peninsula bali si kisiwa. Miaka michache baadaye, mvumbuzi Matthew Flinders alitia nanga kwenye kisiwa hicho. Aliandika hivi: “Peninsula hii haiwezi kuzaa chochote kabisa.”
Ikiwa Cook na Flinders wangeingia ndani kilometa kadhaa kupita fuo hizo na marundo ya mchanga, wangebadili kabisa maoni yao kuhusu kisiwa hicho. Wangeona misitu safi ya mvua, maziwa yenye maji safi kabisa, milima ya mchanga wenye rangi maridadi, na wanyama wa aina nyingi. Kisiwa hicho ambacho sasa kinaitwa Kisiwa cha Fraser, ndicho kisiwa kikubwa zaidi cha mchanga ulimwenguni na kinavutia sana hivi kwamba mwaka wa 1992 kilitiwa katika Orodha ya Maeneo Yanayostahili Kuhifadhiwa. *
Kisiwa Kilichotokea Milimani
Kisiwa cha Fraser kina urefu wa kilometa 120 na upana wa kilometa 25. Kimeenea katika eneo la ekari 395,200. Kuna vilima vikubwa vya mchanga vyenye kimo cha meta 240 hivi juu ya usawa wa bahari ambavyo hufanya kisiwa hicho kiwe kisiwa cha mchanga chenye kimo kirefu zaidi ulimwenguni. Lakini ni utendaji gani uliotokeza rundo hilo la ardhi lenye kustaajabisha?
Uthibitisho unadokeza kwamba mchanga uliofanyiza kisiwa hicho ulitoka kwenye Safu ya Milima ya Great Dividing, ambayo hutanda pwani ya mashariki ya Australia. Baada ya muda mrefu, mvua kubwa zilimomonyoa vipande vya mawe kwenye milima hiyo na kuvisafirisha hadi kwenye mito na baadaye vikaingia baharini. Mikondo ya bahari ilisaga-saga vipande hivyo kuwa mchanga laini na kuvisukuma kaskazini hadi kwenye sakafu ya bahari. Kwa sababu ya kuzuiwa na rasi na miamba iliyojitokeza kwenye sakafu ya bahari, mchanga huo ulirundamana na kutokeza Kisiwa cha Fraser.
Tangu wakati huo, Bahari ya Pasifiki imeendelea kusukuma mchanga kwenye fuo za kisiwa hicho. Mchanga huo hupeperushwa ndani ya kisiwa hicho na kufanyiza marundo ya mchanga. Marundo hayo husonga meta moja kila mwaka na kufunika kila kitu yanachokuta.
Maziwa na Misitu Isiyo ya Kawaida
Kwa kushangaza, katika kisiwa hicho, kuna maziwa 40 yenye maji safi juu ya marundo hayo ya mchanga. Baadhi ya maziwa hayo huonekana kana kwamba yamening’inia juu ya marundo marefu ya mchanga. Ni nini huzuia maji yasifyonzwe ndani ya mchanga? Majani, maganda, na matawi yaliyooza na kujikusanya chini ya maji.
Kisiwa hicho pia kina maziwa ambayo hujitokeza kwenye mashimo ya machanga yaliyo chini ya tabaka la maji. Maji safi huingia katika mashimo hayo na kufanyiza vidimbwi vyenye maji safi kabisa.
Kila mwaka, maziwa hayo hupata sentimeta 150 za mvua. Maji ambayo hayajaingia katika maziwa au kufyonzwa na mchanga hufanyiza vijito ambavyo huelekea baharini. Inakadiriwa kwamba kijito kimoja tu humwaga lita milioni
tano za maji ndani ya Bahari ya Pasifiki kwa saa moja.Kisiwa cha Fraser kina mimea mingi kwa sababu ya kuwa na maji mengi. Kwa kawaida, misitu ya mvua haiwezi kukua katika mchanga usiokuwa na rutuba. Lakini Kisiwa cha Fraser ni mojawapo ya sehemu chache ulimwenguni ambapo misitu ya mvua imenawiri kwenye mchanga. Kwa kweli, wakati mmoja msitu huo ulikuwa na miti mingi sana hivi kwamba miti yake ilitumiwa kutokeza mbao kwa zaidi ya miaka 100. Miti fulani yenye mbao ngumu ilipendwa sana. Mtaalamu mmoja wa misitu alisema hivi katika mwaka wa 1929: “Mtu anayetembea kwenye msitu huo huona ukuta wa miti mikubwa ya mbao yenye urefu wa meta 45 . . . Miti hiyo mikubwa ina kipenyo cha meta mbili hadi tatu.” Miti fulani ilitumiwa kutengeneza Mfereji wa Suez. Hata hivyo, leo watu hawaruhusiwi kukata miti katika Kisiwa cha Fraser.
Paradiso Yenye Historia ya Kusikitisha
Jina la kisiwa hicho lilitokana na msiba. Mnamo 1836, Nahodha James Fraser na mke wake, Eliza, waliokoka meli yao iliyoitwa Stirling Castle ilipovunjika na wakasukumwa hadi ufuo wa kisiwa hicho. Inasemekana kwamba Fraser aliuawa na kabila fulani la wenyeji, lakini Eliza aliokolewa baadaye. Ili kukumbuka msiba huo, jina la kisiwa hicho, Great Sandy, lilibadilishwa na kuwa Kisiwa cha Fraser.
Wenyeji pia walipatwa na msiba. Wakati mmoja kulikuwa na Wenyeji wa Australia wapatao 2,000 katika Kisiwa cha Fraser. Walisemekana kuwa wenye misuli na wenye nguvu. Waliita kisiwa hicho K’gari au Paradiso. Hekaya moja ya Wenyeji wa Australia kuhusu uumbaji wa kisiwa hicho inakifafanua kuwa sehemu maridadi zaidi ulimwenguni. Kwa kusikitisha, magonjwa kutoka Ulaya yaliwamaliza watu hao. Isitoshe, kufikia mwanzoni mwa karne ya 20, Wenyeji wengi wa Australia waliobaki walikuwa wamehamishwa hadi sehemu za bara za Australia.
Hifadhi Inayopendwa
Leo kisiwa hicho ni hifadhi ya wanyama. Mbwa wa mwituni wa Australia wanaoitwa dingo ni mojawapo ya wanyama wanaojulikana sana katika kisiwa hicho. Mbali na mbwa wa kufugwa huko Australia bara, dingo wa Kisiwa cha Fraser huonwa kuwa ndio dingo wa asili zaidi huko Australia mashariki. Huenda wakaonekana kama mbwa wa kufugwa lakini sivyo, kwa hiyo mtu anapaswa kutahadhari wanapokuwa karibu.
Zaidi ya aina 300 za ndege wameonekana katika kisiwa hicho. Aina fulani za kipanga na tai huruka juu ya fuo za kisiwa hicho, huku aina fulani ya mdiria wakiruka kwa kasi juu ya maziwa yake. Ndege wanaohama-hama wanatia ndani aina fulani ya kiluwiluwi ambao hutaga mayai huko Siberia na kuruka kuelekea kusini wakati wa majira ya baridi kali. Wao hupumzika kwa muda kwenye Kisiwa cha Fraser kabla ya kukamilisha safari yao. Kwa kuongezea, katika misimu fulani, popo 30,000 hivi wa aina fulani wenye ukubwa kama wa kunguru, hutua kwenye kisiwa hicho ili wale nekta ya maua ya mikalitusi.
Maji yanayozunguka Kisiwa cha Fraser yana wanyama wengi, kutia ndani nyangumi wenye nundu wanaorudi kutoka Antaktiki kuelekea Tumbawe Kubwa la Australia ambako wao huzaa na kujamiiana. Wanaporudi, nyangumi hao huwa na mbwembwe nyingi wanapojitupa juu na kupiga maji kwa kishindo na hivyo kutupa maji mengi sana juu hivi kwamba yanaweza kuonekana kutoka mbali. Ni kana kwamba wanasalimu kisiwa hicho chenye kustaajabisha!
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 4 Maeneo ya kitamaduni na ya kiasili ambayo yana thamani ya pekee kwa wanadamu kimwili, kibiolojia, kijiolojia, au kisayansi hutiwa kwenye Orodha ya Maeneo Yanayostahili Kuhifadhiwa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni.
[Ramani katika ukurasa wa 14]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
BAHARI YA PASIFIKI
Kisiwa cha Fraser
[Picha katika ukurasa wa 15]
Kulia, kuanzia juu kwenda chini:
Chanzo cha Kijito cha Kurrnung
Maziwa 40 yanaweza kuonekana kotekote katika Kisiwa cha Fraser
Jambo lisilo la kawaida—misitu ya mvua inayokua juu ya mchanga
[Hisani]
All photos: Courtesy of Tourism Queensland
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
“Dingo” na koala
[Hisani]
Courtesy of Tourism Queensland
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Ufuo wenye urefu wa kilometa 120 katika Kisiwa cha Fraser ni mojawapo ya fuo ndefu zaidi ulimwenguni
[Picha katika ukurasa wa 17]
Aina fulani ya tai
[Picha katika ukurasa wa 17]
Kookaburras
[Picha katika ukurasa wa 17]
Waari
[Picha katika ukurasa wa 17]
Nyangumi mwenye nundu akiruka kabla ya kuelekea Antaktika
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]
Eagle: ©GBRMPA; all other photos except pelicans: Courtesy of Tourism Queensland