Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Simu za Dharura—London

Simu za Dharura—London

Simu za Dharura—London

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

“LENGO letu ni kuwafikia wagonjwa mahututi na watu waliojeruhiwa vibaya wanaoishi mahali popote katika eneo la London lenye ukubwa wa kilometa 1,600 za mraba dakika nane baada ya kupokea simu ya dharura,” anaeleza Rob Ashford, meneja wa kituo cha Huduma za Ambulansi cha London. “Sisi hufaulu kufanya hivyo kwa asilimia 75 ya visa vya dharura ingawa visa hivyo vinazidi kuongezeka kila mwaka.”

Nilialikwa katika Kituo Kikuu cha Kuendesha Huduma za Ambulansi kilicho kwenye kituo cha magari-moshi cha Waterloo katika ukingo wa kusini wa mto Thames. Kituo hicho ndicho kikubwa zaidi barani Ulaya nacho hupokea simu za dharura 3,000 hivi kila siku. Simu hizo hutoka kwa watu milioni saba hivi ambao huzungumza zaidi ya lugha 300. Wafanyakazi 300 katika kituo hicho hufanyaje kazi hiyo?

Kupanga Simu Kulingana na Umuhimu

Nilimsikiliza mfanyakazi mmoja akijibu “simu ya dharura 999” kama zinavyoitwa huko Uingereza kwa kuwa 999 ndiyo nambari ya dharura. Mara moja akitumia kompyuta, alitafuta mahali mpigaji simu alipokuwa na makutano ya barabara yaliyokuwa karibu. Alipopata mahali hapo, ramani ya barabara ilitokea kwenye kompyuta yake. Ili kujua umuhimu wa simu hiyo, mpokeaji simu aliuliza maswali kama: Ni watu wangapi wanaohitaji msaada? Wana umri gani, ni wa kiume au wa kike? Je, wamepoteza fahamu? Je, wanapumua? Wana maumivu ya kifua? Je, wanavuja damu?

Mpokeaji simu anapokuwa akichapa habari hiyo, kompyuta inapanga kisa hicho kulingana na umuhimu wake: rangi nyekundu—maisha yamo hatarini, manjano—hali ni baya, lakini maisha hayamo hatarini, au kijani—si mahututi wala maisha hayamo hatarini. Kisha mpokeaji simu hupitisha habari hizo kwa mfanyakazi mwenzake ambaye hutuma msaada kwa mhasiriwa.

Msaada Unaotolewa Mahali pa Aksidenti

Kituo hicho kina ambulansi 395 na magari 60 yanayoweza kufika kwa haraka mahali pa dharura. Simu ya dharura inapopokewa, gari la dharura lililo karibu na mahali hapo hutumwa. Pia wahudumu wa afya wanaotumia pikipiki huwa tayari wakati wowote kwa mwito wa dharura kwa kuwa wanaweza kujipenyeza kwa urahisi mahali penye msongamano wa magari. Kwa kuongezea, madaktari 12 huwa tayari kuitwa wakati wowote kuwasaidia wahudumu hao.

Nilipokuwa katika kituo hicho, polisi waliripoti kuhusu aksidenti mbaya iliyotokea kwenye barabara moja kuu yenye magari mengi. Tayari kulikuwa na ambulansi mahali pa aksidenti, lakini polisi bado walipiga simu kwenye kituo cha ambulansi. Kwa nini? Ili kuwajulisha kwamba huenda wakahitaji helikopta yao. Helikopta hiyo yenye rangi nyekundu inayoonekana wazi hufunga safari za dharura 1,000 hivi kila mwaka. Huwa na daktari na msaidizi wake ambao kwa kawaida huwapeleka watu waliojeruhiwa vibaya kwenye hospitali ya Royal London ili kupata matibabu ya haraka.

Mnamo 2004, mbinu nyingine ilianzishwa, yaani, majaribio ya huduma za dharura kwa kutumia baiskeli katika Uwanja wa Ndege wa Heathrow huko London. Huduma hizo tayari zilikuwa zikitumika katika eneo la West End. Baiskeli hizo hutumiwa na kikundi cha watu watano wanaotia ndani watu wanaotoa huduma za dharura, jambo ambalo huwezesha ambulansi zitumiwe kutoa huduma nyingine. Kila baiskeli ina taa ya bluu na king’ora, mifuko ya kubebea vifaa vyenye uzito wa kilogramu 35 kutia ndani kifaa cha kufanya moyo uanze kupiga tena, oksijeni, na madawa ya kupunguza maumivu.

Umuhimu wa huduma za baiskeli ulionekana siku chache baada ya kuanzishwa. Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 35 alikuwa mgonjwa alipokuwa kwenye Kiingilio cha 4 cha uwanja wa ndege wa Heathrow na akaacha kupumua. Wahudumu wawili wa afya kutoka kikundi hicho waliitikia haraka mwito wa dharura wa 999 na kumpa oksijeni, na mara moja wakaanza kumfanyia huduma ya kwanza ili aanze kupumua tena. Alikimbizwa hospitali iliyo karibu kwa ambulansi. Alipopata nafuu, mwanamke huyo alienda kwenye kituo hicho ili kuwashukuru wahudumu hao wa afya kwa kuokoa maisha yake.

Huduma Inayopanuka

Ikiwa mtu anayepiga simu ya dharura hajui Kiingereza, simu hiyo huelekezwa kwa mtafsiri. Bila shaka, inaweza kutatanisha kujaribu kutambua lugha ya mtu aliyepiga simu hasa ikiwa mtu huyo anazungumza haraka kwa sababu ya wasiwasi au mkazo!

Ili kuelimisha umma kuhusu matibabu ya dharura, filamu fupi yenye maelezo mafupi yaliyoandikwa katika Kiingereza imetolewa kwenye DVD. Lengo lake ni kuwatia moyo wakazi wa London wa jamii ya Waasia “wajifunze jinsi ya kumsaidia mgonjwa kupumua tena kwa kumpulizia pumzi mdomoni,” kinasema LAS News, kichapo cha kituo cha Huduma za Ambulansi cha London. Filamu hiyo pia huonyesha jinsi simu za dharura zinavyoshughulikiwa katika kituo hicho.

Wakazi wa jiji hilo kuu la Uingereza huthamini sana wahudumu hao wanapoitikia haraka hali ya dharura inapotokea, iwe hali hiyo inahusisha mtu mmoja au wengi, iwe imetokea kwenye vijia vilivyo chini ya ardhi au kwenye jengo refu sana. Mmoja wa madaktari wa kujitolea alisema hivi kuhusu wanaume na wanawake wanaofanya kazi katika kituo cha Huduma za Ambulansi cha London: “Wao ni baadhi ya wataalamu bora sana wa kitiba ambao nimewahi kufanya kazi nao.” Hiyo ni sifa nzuri kwa wafanyakazi wa kituo kikubwa zaidi ulimwenguni kinachotoa huduma za ambulansi bila malipo.

[Sanduku katika ukurasa wa 11]

Matatizo Wanayokabili

Simu zinazopigwa kuuliza habari za kibinafsi na simu kuhusu magonjwa na majeraha madogo-madogo, na pia kupiga nambari 999 kimakosa au kwa mzaha kumesababishia matatizo wale wanaotoa huduma za dharura. Jambo baya hata zaidi ni kwamba wagonjwa fulani na watu wengine, kutia ndani watu wa familia ya mgonjwa, wamewatusi au hata kuwapiga wahudumu wa afya ambao walienda kuwasaidia! Huenda hasira yao ilisababishwa na mkazo au dawa za kulevya au kukosa subira na kufikiri kwamba hawakupokea msaada kwa wakati unaofaa. Hakuna suluhisho kamili kwa matatizo hayo ingawa kuelimisha umma kumesaidia kuyatatua.

[Picha katika ukurasa wa 10]

Kituo hicho hupokea simu za dharura 3,000 hivi kila siku

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 10]

All photos: Courtesy of London Ambulance Service NHS Trust