Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Chernobyl Kutembelea

Chernobyl Kutembelea

Chernobyl Kutembelea

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UKRAINIA

Msiba usio na kifani ulitukia miaka 20 iliyopita katika kituo cha nguvu za nyuklia cha Chernobyl. Aprili 26, 1986, mmojawapo wa mitambo minne ya nyuklia katika kituo cha Chernobyl ulilipuka na kusababisha msiba mkubwa sana. Kwa kawaida watu huweza kuondoa takataka na kuendelea na maisha baada ya misiba kutokea, iwe imesababishwa na wanadamu au iwe ya asili. Lakini, takataka zilizotokezwa na msiba huu zimekuwa na madhara ya muda mrefu.

KATIKA miaka ya karibuni, kila ifikapo Mei 9, wakazi wa zamani wa majiji yaliyo karibu na kituo hicho wametembelea nyumba zao zilizoachwa ukiwa, nyakati nyingine wakiandamana na marafiki na watu wa ukoo. Wakati mwingine wameenda huko kwa ajili ya mazishi. Wanasayansi wametembelea eneo hilo kuchunguza madhara ya mnururisho. Isitoshe, hivi karibuni makampuni ya utalii ya Ukrainia yamekuwa yakiwatembeza wageni kwa siku moja katika eneo hilo.

Mnamo Juni 2005, ukurasa wa mbele wa gazeti The New York Times ulisema kwamba kuna mpango wa ‘kuwatembeza watu kifupi katika jiji la Pripet.’ Safari hizo haziwezi “kudhuru afya.” * Jiji la Pripet lilianzishwa miaka ya 1970. Lilikuwa na watu wapatao 45,000, nalo liko kilometa tatu hivi kutoka kwenye mitambo hiyo ya nyuklia. Hata hivyo, kama miji mingine mingi, watu wote waliondoka Pripet baada ya msiba wa nyuklia. Watu hawakuruhusiwa kurudi katika maeneo hayo kwa sababu ya mnururisho. Wakati mtambo huo ulipolipuka, Anna na Victor Rudnik walikuwa wameishi Pripet kwa mwaka mmoja hivi. *

Mji mdogo wa Chernobyl (ambalo pia ni jina la kituo cha nguvu za nyuklia) uko kilometa 15 hivi kutoka kwenye mitambo hiyo ya nyuklia. Kwa miaka kadhaa wakazi wa awali wa mji huo wameruhusiwa kuutembelea mara moja kwa mwaka. Akina Rudnik wametembelea Chernobyl wakati huo kwa sababu huko ndiko nyumbani. Miaka michache iliyopita, mimi, mke wangu, na akina Rudnik tulitembelea Chernobyl. Hebu niwasimulie jinsi ilivyokuwa.

Safari Yetu Yenye Kuhuzunisha

Tuliondoka Kiev, mji mkuu wa Ukrainia, na kuelekea kaskazini. Tulipokuwa tukipita miji midogo njiani, tuliona nyumba kandokando ya barabara zilizokuwa na bustani zenye maua upande wa mbele na watu wakilimia mashamba ya mboga. Kati ya miji hiyo, kulikuwa na mashamba makubwa sana ya mahindi, ngano, na alizeti.

Lakini tulipofika eneo fulani, hali ilibadilika. Ingawa hakukuwa na ishara yoyote barabarani, tulitambua badiliko hilo. Kimya kizito chenye kuogofya kilitanda miji ambayo sasa tulipita. Nyumba zilikuwa zimechakaa, madirisha yalikuwa yamevunjika na milango kutiwa kufuli. Magugu yalitawala bustani na mashamba.

Kumbe tulikuwa tumeingia katika eneo ambalo watu hawaruhusiwi, kilometa 30 hivi kutoka kwenye mitambo ya nyuklia. “Miji iliyo katika eneo hili ina kiasi kikubwa cha mnururisho,” Anna alituambia. “Zaidi ya watu 150,000 walihamishwa kutoka miji mingi na vijiji vingi vya eneo hili na kupelekwa sehemu nyingine za ule uliokuwa Muungano wa Sovieti.”

Tuliendelea na safari, na punde si punde, tukafika eneo lingine lililotengwa kabisa kwa ua mrefu wa nyaya. Karibu na hapo, kulikuwa na walinzi katika kituo kilichojengwa kwa mbao kinachofanana na cha forodha ambako magari yote yalikaguliwa. Mlinzi mmoja alikagua pasipoti zetu, akaandikisha gari letu na kutufungulia lango.

Sasa tulikuwa tumeingia katika eneo ambalo watu hawaruhusiwi kuingia bila idhini. Msitu wenye majani mengi ulifunika barabara juu yetu kama mwavuli. Vichaka vilishikana sana chini ya msitu huo. Hilo lilinishangaza kwa kuwa nilitarajia kuona miti iliyoungua na vichaka vilivyonyauka. Mbele yetu kulikuwa na ishara ya Chernobyl iliyoandikwa kwa maandishi ya buluu kwenye jiwe jeupe.

Kwenye mpaka wa Chernobyl kulikuwa na duka la dawa ambako zamani mamake Victor alifanya kazi. Bado ishara iliyochakaa iliyokuwa ikionyesha saa za kazi ilining’inia kwenye dirisha chafu. Karibu na bustani kuu ya mji kulikuwa na jengo la maonyesho ya kitamaduni. Anna alikumbuka jinsi yeye na wengine walivyokuwa wakienda kuburudika huko baada ya kazi wakitazama maonyesho mbalimbali. Karibu na hapo kulikuwa na jumba la sinema lililoitwa Ukraina. Kulipokuwa na joto kali nje, watoto walikuwa wakienda kutazama sinema katika jumba hilo lenye kustarehesha. Vicheko vilivyoanguliwa ndani ya jengo hilo havisikiki tena. Anna na Victor walitupeleka nyumba walimoishi ambayo haikuwa mbali na mji. Miti iliyomea ovyoovyo iliziba mlango wa mbele, kwa hiyo tulilazimika kupita katikati ya magugu chungu nzima na kutumia mlango wa nyuma ambao sasa ulikuwa tu kama shimo kubwa ukutani.

Ndani mlikuwa vurugu tupu. Godoro lenye kuvu lilikuwa limebonyea katika kitanda chenye kutu. Karatasi chafu zilining’inia ukutani ovyoovyo. Anna aliinama na kuokota picha ya zamani kwenye takataka zilizotapakaa sakafuni. “Nimekuwa nikitamani sana kurudi na kupata kila kitu kikiwa jinsi tulivyokiacha,” alisema kwa huzuni. “Nahuzunika sana kuona nyumba yetu ikiwa imechakaa na vitu vyetu kuibiwa katika muda ambao umepita.”

Tuliondoka kwa akina Rudnik na kuteremka barabarani. Kwenye kona moja, kulikuwa na watu waliokuwa wakizungumza kwa uchangamfu. Tulitembea kwa nusu kilometa hivi kufikia bustani iliyokuwa kwenye mwinuko kando ya mto mpana uliotulia. Maua meupe ya miti yalikuwa yanapeperushwa-peperushwa na upepo mwanana. Pindi moja mnamo 1986, mamia ya watu walingoja kwenye ngazi zinazoteremka kwenye gati wahamishwe kwa mashua.

Mwaka uliopita akina Rudnik walitembelea kwa mara ya kwanza nyumba yao ya zamani huko Pripet. Walitoroka jiji hilo miaka 19 iliyopita wakati mtambo wa nyuklia ulipolipuka.

Wakati wa Kutafakari

Mwezi wa Aprili 2006, kutakuwa na maadhimisho mbalimbali ya kukumbuka mwaka wa 20 tangu ule msiba wa nyuklia. Jambo hilo linawakumbusha watu wengi kwamba licha ya jitihada zake za unyoofu, mwanadamu hawezi kufanikiwa kusimamia mambo ya dunia pasipo msaada wa Mungu.—Yeremia 10:23.

Septemba mwaka uliopita, matokeo ya ripoti moja iliyochunguza msiba huo yalitolewa. Ripoti hiyo iliyoidhinishwa na Umoja wa Mataifa ilisema kwamba mwanzoni msiba huo ulisababisha vifo vya watu 56 na ilitabiri kwamba ni vifo 4,000 pekee vingesababishwa na magonjwa yanayotokana na mnururisho. Awali ilitabiriwa kwamba kati ya watu 15,000 na 30,000 wangekufa. Tahariri ya gazeti New York Times la Septemba 8, 2005, ilisema kwamba ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa “ilishutumiwa na mashirika kadhaa yanayotetea mazingira yaliyodai kwamba ilificha madhara yanayoweza kusababishwa na nguvu za nyuklia.”

Victor, ambaye alijifunza kuhusu Muumba wake, Yehova Mungu, baada ya msiba huo, alisema hivi: “Hatujashuka moyo tena, kwa kuwa twajua kwamba Ufalme wa Mungu ujapo, misiba mibaya kama hiyo haitatukia tena. Twatazamia wakati ambapo eneo lililo katika ujirani wa nyumba yetu karibu na Chernobyl litaboreka na kuwa paradiso ya ajabu.”

Tangu msiba wa Chernobyl, mamilioni ya watu wamesadiki kabisa kwamba Paradiso ya awali itarudishwa na kuenea duniani pote kama Biblia inavyoahidi. (Mwanzo 2:8, 9; Ufunuo 21:3, 4) Nchini Ukrainia pekee zaidi ya watu 100,000 wamekubali tumaini hilo katika miaka 20 iliyopita! Wewe pia na uchochewe kuchunguza wakati ujao mzuri ambao watu wanaopendezwa kujifunza makusudi ya Mungu wameahidiwa.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Ingawa watu mbalimbali wenye mamlaka wamesema kwamba safari hizo ni salama, Amkeni! haitoi mapendekezo yoyote kuhusu safari za kibinafsi za kutembelea eneo hilo.

^ fu. 5 Ona toleo la Amkeni! la Aprili 22, 1997, ukurasa wa 12-15.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16]

Nguzo ya Ukumbusho

Nguzo hii yenye kimo cha meta nne ilijengwa kwa heshima ya wafanyakazi wa msiba wa Chernobyl ambao walisaidia kuondoa sumu. Wafanyakazi hao walizima moto, wakafunika mtambo huo wa nyuklia, na kuondoa sumu. Kabla ya kazi hiyo kumalizika, mamia ya maelfu ya watu walisaidia kuifanya. Inatabiriwa kwamba vifo vya watu wapatao 4,000 vitasababishwa na msiba huo, wengi wao wakiwa wafanyakazi hawa.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Ishara ya mji wa Chernobyl na jumba la sinema

[Picha katika ukurasa wa 15]

Akina Rudnik na nyumba yao huko Chernobyl

[Picha katika ukurasa wa 16]

Kituo cha nguvu za nyuklia ambako mlipuko ulitukia, kilometa tatu hivi kutoka kwenye nyumba ya akina Rudnik huko Pripet (picha ndogo)