Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Huko Brazili, matumizi ya dawa inayoitwa amphetamine ili kupunguza uzito kwa kuzuia hamu ya kula yaliongezeka kwa asilimia 500 kuanzia mwaka wa 1997 hadi 2004.—FOLHA ONLINE, BRAZILI.

Kuna uwezekano mara tatu kwa marubani wa ndege kuwa na watoto wa jicho. Huenda wakapatwa na ugonjwa huo kwa sababu wao hupigwa zaidi na miali-anga.—THE WALL STREET JOURNAL, MAREKANI.

Kwa miaka kumi ijayo, karibu nusu ya watoto bilioni 1.27 wa Asia watakosa mahitaji yao ya lazima kama vile maji safi, chakula, matibabu, elimu, na makao.—PLAN ASIA REGIONAL OFFICE, THAILAND.

Moshi wa sigara inayovutwa na mtu mwingine ni “hatari zaidi kuliko ilivyodhaniwa.” Miezi 18 baada ya kuvuta sigara kupigwa marufuku katika ofisi, mikahawa, na majumba mengine huko Pueblo, Colorado, Marekani, visa vya mshtuko wa moyo vilipungua kwa asilimia 27.—TIME, MAREKANI.

Kuvunjika kwa Ndoa Kunaongezeka Nchini Hispania

Katika mwaka wa 2000, idadi ya ndoa nchini Hispania ilikuwa mara mbili zaidi kuliko mitengano na talaka. Lakini kufikia mwaka wa 2004, ndoa mbili kati ya arusi tatu zilikuwa zikivunjika. Tangu sheria za kuruhusu talaka zilipoidhinishwa mwaka wa 1981, zaidi ya watoto milioni moja wameona wazazi wao wakitengana. Ni nini kinachosababisha ongezeko la kuvunjika kwa ndoa? Mwanasaikolojia Patricia Martínez, anasema kwamba “mabadiliko ya kitamaduni, kuzorota kwa viwango vya dini na vya maadili, wanawake kuanza kufanya kazi za kuajiriwa, na wanaume kutoshirikiana katika kufanya kazi za nyumbani ndiyo hasa yanafanya uhusiano wa ndoa usiwe imara.”

Wachina Wanenepa Kupita Kiasi

Gazeti The Guardian la London linasema kwamba nchini China, “kutakuwa na watu milioni 200 walionenepa kupita kiasi kwa njia yenye kuhatarisha afya katika miaka 10 inayokuja.” Mikahawa inayouza vyakula vyepesi “inapatikana kila mahali katika miji mingi. Jambo hilo limefanya kuwe na ongezeko la idadi ya watu wenye mapato ya kadiri ambao hawafanyi mazoezi, wanatumia gari zaidi, na ambao hutumia wakati mwingi wakiwa wameketi kitako wakitazama televisheni, kucheza michezo ya kompyuta au video.” Idadi ya watoto wanaosemekana kuwa wanene kupita kiasi inaongezeka kwa asilimia 8 kila mwaka, na huko Shanghai zaidi ya asilimia 15 ya watoto wa shule ya msingi tayari ni wanene kupita kiasi.

Mto Waonyesha Kutumiwa Sana kwa Dawa za Kulevya

Maji yaliyopimwa ya Mto Po huko Italia yalionyesha kwamba wakazi wengi zaidi wanaoishi kwenye bonde la mto huo hutumia kokeini kuliko ilivyokadiriwa na serikali, unasema uchunguzi mmoja uliochapishwa katika gazeti Environmental Health. Mkojo wa watumizi wa kokeini huwa na kemikali inayoitwa benzoylecgonine. Mara nyingi, kemikali hiyo inapopatikana kwenye mkojo hutumiwa kortini kuthibitisha kwamba mtu anatumia kokeini. Kiasi cha kemikali hiyo kinachoingia kwenye mto huo kupitia kwa mfumo wa kuondoa maji machafu kinaonyesha kwamba kilogramu nne hivi za kokeini au dozi 40,000, hutumiwa kila siku na watu wanaoishi katika bonde la mto huo. Kiasi hicho ni mara 80 zaidi ya makadirio ya awali.

Vifo Vinavyoweza Kuzuiwa

Ripoti ya 2005 ya Shiriki la Afya Ulimwenguni ilisema kwamba “mwaka huu, karibu watoto milioni 11 walio chini ya umri wa miaka mitano watakufa hasa kutokana na visababishi vinavyoweza kuzuiwa.” Asilimia 90 hivi ya vifo hivyo husababishwa na mambo machache tu: hali ambayo huwapata watoto walio chini ya umri wa mwezi mmoja kama vile kuzaliwa kabla ya wakati, maambukizo, na kuishiwa na hewa wakati wa kuzaliwa; maambukizo ya mapafu; nimonia; kuendesha; malaria; surua; na UKIMWI. Ripoti hiyo inasema: “Vingi vya vifo hivyo vinaweza kuzuiwa kupitia matibabu ya sasa ambayo ni rahisi, hazigharimu sana na hufanya kazi.” Kwa kuongezea, wanawake zaidi ya nusu milioni hufa kila mwaka wakiwa waja-wazito au wanapojifungua hasa kwa sababu “hawawezi kupata matibabu yanayofaa.”