Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jinsi Upigaji-Picha Ulivyoanza

Jinsi Upigaji-Picha Ulivyoanza

Jinsi Upigaji-Picha Ulivyoanza

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI SWEDEN

HEKAYA MOJA HUSEMA KWAMBA WAGENI WA MWANAFIZIKIA MWITALIANO GIAMBATTISTA DELLA PORTA (1535?-1615) WALISHTUKA. KWENYE UKUTA ULIOKUWA MBELE YAO, WALIONA WATU WADOGO WAKITEMBEA VICHWA VIKIWA CHINI NA MIGUU JUU. WAGENI HAO WALIOKUWA NA WOGA WALITIMUKA MBIO KUTOKA KWENYE CHUMBA HICHO. DELLA PORTA ALISHTAKIWA KUWA MCHAWI!

JITIHADA zake za kuwachekesha wageni wake kwa kuwaonyesha camera obscura, ambayo katika Kilatini inamaanisha “sanduku lenye giza” zilimletea matata. Kamera hufanya kazi kwa njia rahisi lakini matokeo yake huvutia. Kamera hufanyaje kazi?

Nuru inapoingia kwenye sanduku au chumba chenye giza kupitia tundu dogo, picha ya kitu kilicho nje huonekana ndani kikiwa chini juu. Wageni wa Della Porta waliona tu picha ya watu waliokuwa wakiigiza huko nje. Sanduku hilo lenye giza lilikuwa mwanzo wa kamera ya kisasa. Leo huenda ukawa mmoja wa mamilioni ya watu walio na kamera au ambao wametumia kamera za bei rahisi.

Sanduku hilo lenye giza lilijulikana hata kabla ya siku za Della Porta. Aristotle (384-322 K.W.K.) alitambua kanuni ambayo ilitumiwa baadaye kutengeneza kamera. Alhazen, msomi Mwarabu aliyeishi katika karne ya 10 alieleza kwa undani kanuni hiyo, naye mchoraji Leonardo da Vinci, aliyeishi katika karne ya 15 aliifafanua katika vitabu vyake. Kuvumbuliwa kwa lenzi katika karne ya 16 kuliboresha picha zilizopigwa kwa kamera, nao wasanii wengi walitumia lenzi kupiga picha zilizoonyesha kwa usahihi umbali na ukubwa wa vitu. Lakini licha ya jitihada nyingi, bado ilikuwa vigumu kusafisha picha hizo hadi karne ya 19.

Mpigaji-Picha wa Kwanza Ulimwenguni

Yaonekana mwanafizikia Mfaransa, Joseph-Nicéphore Niepce, alianza jitihada za kusafisha picha mapema mnamo 1816. Lakini alifanikiwa mara ya kwanza alipogundua kwamba anaweza kutumia aina fulani ya lami kuchora picha kwenye mwamba. Wakati fulani katikati ya miaka ya 1820, alipaka lami bamba lililotengenezwa kwa bati na risasi na kuliweka ndani ya sanduku lenye giza likielekea dirisha la nyumba yake na kuliacha lipigwe na nuru kwa muda wa saa nane. Hakuna mpiga-picha yeyote wa leo asiye na uzoefu ambaye angejivunia picha isiyoonekana waziwazi ya jengo, mti, na ghala iliyopigwa na Niepce. Lakini Niepce alikuwa na sababu ya kujivunia picha hiyo. Huenda ikawa hiyo ndiyo iliyokuwa picha ya kwanza kusafishwa!

Ili kuboresha mbinu yake zaidi, mnamo 1829, Niepce alijiunga na mwanabiashara maarufu Louis Daguerre. Miaka iliyofuata baada ya kifo cha Niepce mnamo 1833, Daguerre alifanya maendeleo fulani muhimu. Alipaka mchanganyiko wa madini ya fedha na iodidi kwenye mabamba ya shaba. Mchanganyiko huo uliathiriwa zaidi na nuru kuliko lami. Bila kutazamia, aligundua kwamba bamba hilo lilipopigwa na mvuke wa zebaki baada ya kusafishwa, picha ilionekana waziwazi. Hilo lilipunguza muda wa kusafisha picha. Daguerre alipogundua kwamba kusafisha bamba hilo kwa maji ya chumvi kulizuia picha isiwe nyeusi baada ya muda, kwa ghafula watu walianza kuvutiwa na upigaji-picha.

Upigaji-Picha Waanza

Watu walipoonyeshwa uvumbuzi wa Daguerre ulioitwa daguerreotype mnamo 1839, walivutiwa sana. Msomi Helmut Gernsheim anaandika hivi katika kitabu chake The History of Photography: “Huenda ikawa hakuna uvumbuzi mwingine uliowahi kuwazuzua watu na kupendwa sana ulimwenguni kwa haraka zaidi kuliko ule wa Daguerre.” Mmoja wa watu waliojionea kutolewa kwa uvumbuzi huo kwa umma aliandika: “Saa moja baada ya uvumbuzi huo, watu walijaa katika maduka yote ya miwani, lakini hayangeweza kukusanya vifaa vya kutosha kuridhisha wateja hao wengi ambao baadaye wangetumia uvumbuzi huo; siku chache baadaye kwenye jiji la Paris kulikuwa na masanduku yenye giza yaliyo na miguu mitatu mbele ya makanisa na makasri. Wanafizikia, wanakemia, na wasomi wote wa jiji hilo walikuwa waking’arisha mabamba ya fedha, na hata wauzaji wa mboga wenye pesa hawangeweza kujizuia kutumia mali zao kununua kifaa hicho.” Punde si punde, vyombo vya habari viliita pilikapilika hizo “kichaa” cha uvumbuzi wa Daguerre.

Uvumbuzi wa Daguerre wenye kutokeza ulimchochea mwanasayansi Mwingereza John Herschel kuandika: “Hatutakuwa tukitia chumvi kusema kwamba uvumbuzi huo ni muujiza.” Hata watu fulani walisema kwamba uvumbuzi huo ulitokezwa kwa nguvu za uchawi.

Lakini si watu wote waliopokea kwa furaha uvumbuzi huo mpya. Mnamo 1856, mfalme wa Naples alipiga marufuku upigaji-picha labda kwa sababu ulifikiriwa kuwa unahusiana na uchawi. Alipoona uvumbuzi wa Daguerre, mchoraji Mfaransa Paul Delaroche alisema: “Kuanzia leo sanaa ya uchoraji imekwisha!” Pia, uvumbuzi huo ulizua wasiwasi mwingi miongoni mwa wachoraji ambao waliuona kuwa tisho kwa njia yao ya kujiruzuku. Mtangazaji mmoja alieleza wasiwasi wa wachoraji aliposema: “Kwa kuwa upigaji-picha hutokeza picha halisi kabisa unaweza kuharibu mawazo ya watu kuhusu umaridadi.” Isitoshe, picha za kamera zilichambuliwa kwa kuharibu maoni ya watu kuhusu umaridadi wa mahali na ujana wa watu.

Daguerre na Talbot Wang’ang’ana

Mwanafizikia Mwingereza William Henry Fox Talbot, aliamini kwamba yeye ndiye aliyevumbua upigaji-picha, kwa hiyo alishangaa sana aliposikia tangazo kuhusu uvumbuzi wa Daguerre. Talbot alikuwa akiweka karatasi iliyopakwa mchanganyiko wa madini ya fedha na kloridi ndani ya sanduku lenye giza. Alisugua picha kwa nta ili kuifanya ipenyeze nuru, akaiweka juu ya karatasi iliyokuwa na madini, kisha akaiweka mahali penye nuru ya jua, na hivyo kutokeza nakala ya picha halisi.

Ingawa hapo mwanzoni uvumbuzi wake haukupendwa na wengi na ulitokeza picha za hali ya chini, uvumbuzi wa Talbot ulionekana kuwa ungetokeza kamera bora. Uliwezesha nakala nyingi zitolewe kutokana na picha moja, na nakala za karatasi zilikuwa za bei ya chini na rahisi kubeba kuliko zile za Daguerre ambazo zingeweza kuharibika kwa urahisi. Upigaji-picha wa kisasa bado unatumia mbinu ya kusafisha picha ya Talbot, ilhali uvumbuzi wa Daguerre ambao ulipendwa hapo mwanzoni haukuendelea kutumika.

Hata hivyo, mbali na Niepce, Daguerre, na Talbot, kuna watu wengine ambao walidai kuwa wa kwanza kuvumbua upigaji-picha. Baada ya Daguerre kutangaza uvumbuzi wake mnamo 1839, angalau wanaume 24, kutoka Norway huko kaskazini hadi Brazili huko kusini, walijitokeza na kudai kuwa tayari walikuwa wamevumbua upigaji-picha.

Mabadiliko Makubwa Yaliyotokezwa na Upigaji-Picha

Jacob August Riis, aliyekuwa mrekebishaji wa mambo ya kijamii, aliona mapema sana kwamba upigaji-picha ungekuwa njia nzuri ya kuwajulisha watu kuhusu umaskini na kuteseka. Mnamo 1880 alianza kupiga picha usiku nyumba za mabanda huko New York City akitumia madini ya manganisi yaliyokuwa yakiwaka kwenye kikaango ili kutokeza nuru aliyohitaji. Mbinu hiyo ilikuwa hatari. Nyumba aliyotumia kufanya kazi hiyo ilishika moto mara mbili, na wakati mmoja nguo zake zilishika moto. Inasemekana kwamba picha zake zilimchochea Rais Theodore Roosevelt afanye mabadiliko ya kijamii alipochaguliwa kuwa Rais. Pia, picha zenye kuvutia zilizopigwa na William Henry Jackson zilichochea Bunge la Marekani lifanye Yellowstone kuwa mbuga ya wanyama ya kwanza ulimwenguni mnamo 1872.

Watu Wote Waweza Kupiga Picha

Mwishoni mwa miaka ya 1880, watu wengi waliotaka kupiga picha hawangeweza kufanya hivyo kwa sababu ya gharama na ugumu wa kupiga picha. Lakini mnamo 1888, George Eastman alipovumbua Kodak, kamera iliyokuwa na filamu na ambayo ilikuwa rahisi kubeba na kutumia, alifanya iwezekane kwa kila mtu kupiga picha.

Baada ya kutumia filamu yote, mpigaji-picha aliipeleka kamera yote kwenye kiwanda. Filamu hiyo ilisafishwa na kamera ikarudishwa ikiwa na filamu nyingine pamoja na picha zilizosafishwa. Yote hayo yangefanywa kwa bei rahisi sana. Usemi wa kampuni hiyo “Piga picha, tukufanyie hayo mengine” ulikuwa kweli.

Sasa kila mtu angeweza kupiga picha, na mabilioni ya picha ambazo hupigwa kila mwaka zinaonyesha kwamba bado upigaji-picha ni maarufu. Kuongezea umaarufu wake, sasa kuna kamera zinazotumia kompyuta ambazo hutoa picha za hali ya juu. Kamera hizo hutumia kidude cha elektroniki ambacho kinaweza kuhifadhi picha nyingi sana. Mtu anaweza kutoa picha za hali ya juu kwa kutumia kompyuta nyumbani na mashini ya kuchapa. Hakuna shaka yoyote kwamba maendeleo makubwa yamefanywa kuhusiana na upigaji-picha.

[Picha katika ukurasa wa 20]

Picha ya Paris iliyopigwa kwa kamera ya Daguerre, karibu 1845

[Picha katika ukurasa wa 20]

Nakala ya ile inayodhaniwa kuwa picha ya kwanza iliyosafishwa, karibu 1826

[Picha katika ukurasa wa 20]

Mchoro wa sanduku lenye giza, lililotumiwa na wasanii wengi

[Picha katika ukurasa wa 21]

Niepce

[Picha katika ukurasa wa 23]

Picha ya 1844 ya Louis Daguerre, iliyopigwa kwa kamera aliyovumbua, na kamera hiyo

[Picha katika ukurasa wa 23]

Studio ya William Talbot, karibu mwaka wa 1845 na kamera zake

[Picha katika ukurasa wa 23]

Picha ya 1890 ya George Eastman akiwa na kamera ya Kodak Na. 2, na kamera yake Na. 1 yenye kigurudumu cha filamu

[Picha katika ukurasa wa 23]

Picha ya iliyokuja kuwa Yellowstone, iliyopigwa na W. H. Jackson, 1871

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kamera za kisasa zinazotumia kompyuta hupiga picha za hali ya juu

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 20]

Panoramic of Paris: Photo by Bernard Hoffman/Time Life Pictures/Getty Images; Niepce’s photograph: Photo by Joseph Niepce/Getty Images; camera obscura: Culver Pictures

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 22]

Page 23: Talbot’s studio: Photo by William Henry Fox Talbot & Nicholaas Henneman/Getty Images; Talbot’s camera: Photo by Spencer Arnold/Getty Images; Kodak photo, Kodak camera, and Daguerre camera: Courtesy George Eastman House; Yellowstone: Library of Congress, Prints & Photographs Division, LC-USZ62-52482