Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
▪ Meno ya asilimia 60 ya watoto nchini Brazili huwa tayari yameoza wanapofikia umri wa miaka mitatu. Sababu moja ni kwamba hawasafishwi meno baada ya kunyweshwa vinywaji vyenye sukari usiku.—FOLHA ONLINE, BRAZILI.
▪ Asilimia 25 ya watoto wanaozaliwa nchini Marekani sasa huzaliwa kupitia upasuaji. Huko New York City, idadi hiyo imezidi kwa mara tano ile ya mwaka wa 1980. Sababu moja ni kwamba wanawake wanaweza kujipangia wakati wa kujifungua, hata hivyo kuna hatari “kubwa sana” ya kuzaa kwa kupasuliwa isivyo lazima.—THE NEW YORK TIMES, MAREKANI.
▪ Katika miaka 100 iliyopita, wastani wa kiwango cha joto huko Mexico City umeongezeka kwa nyuzi 4 hivi za Selsiasi, ukilinganishwa na ongezeko la nyuzi 0.6 za Selsiasi ulimwenguni pote. Wataalamu wanasema kwamba ongezeko hilo limesababishwa na ukataji wa miti na watu kuhamia mijini.—EL UNIVERSAL, MEXICO.
▪ Zaidi ya nusu ya watu wanaooana nchini Marekani tayari huwa wameishi pamoja. Kuna uwezekano mara mbili kwa wenzi hao kutalikiana kuliko wale ambao hawajaishi pamoja kabla ya kuoana.—PSYCHOLOGY TODAY, MAREKANI.
Tabia Zinazoudhi Zaidi Kazini
Gazeti Washington Post linaripoti kwamba “kuzungumza kwa sauti kubwa kwenye simu, kutumia simu zenye vikuza-sauti, na kulalamika daima kwamba kuna kazi nyingi ni baadhi ya tabia zenye kuudhi sana za wafanyakazi wenzetu.” Tabia nyingine zinazowaudhi sana wafanyakazi wengine ni “wafanyakazi fulani kufanyiza vikundi vya kirafiki, kuchelewa kufika kazini, kujizungumzia, kuzungumza na mfanyakazi mwenzetu kupitia ukuta mfupi unaogawanya ofisi, kutozingatia usafi wa mwili, na kutafuna kwa sauti.” Pia tabia hizo mbaya zinaweza kuwazuia watu wasifanye kazi vizuri. Hata hivyo, wengi wa wale waliohojiwa walisema kwamba hawakuwa wamezungumza na watu wenye tabia zilizowaudhi. “Kuna sababu nzuri ya kutofanya hivyo,” likasema gazeti hilo. “Huenda ikawa wao wenyewe wana tabia kama hizo.”
Watu Wengi Zaidi Wanaishi Majijini
Shirika la habari la CBC News linasema kwamba “katika miaka miwili ijayo nusu ya watu wote ulimwenguni watakuwa wakiishi majijini.” Kulingana na ripoti moja ya Umoja wa Mataifa, Marekani ndiyo nchi yenye wakazi wengi zaidi majijini, ambapo watu 9 kati ya 10 huishi majijini. Miaka 55 tu iliyopita, New York na Tokyo ndiyo majiji pekee yaliyokuwa na wakazi milioni 10 au zaidi. Leo idadi hiyo imeongezeka kufikia majiji 20 yenye watu zaidi ya milioni 10. Majiji hayo yanatia ndani, Jakarta, Mexico City, Mumbai, na São Paulo. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, anasema: “Nchi nyingi zitahitaji kufanya marekebisho makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa sababu ya ongezeko hilo la haraka.”
Kukataa Utumishi wa Kijeshi kwa Sababu za Dhamiri
Kamati ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Jamhuri ya Korea inasema kwamba kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu za dhamiri ni haki isiyoweza kupingwa. Kamati hiyo ilipendekeza kwamba haki hiyo iheshimiwe kwa kubuni utumishi wa kijamii wa badala. Gazeti The Korea Times, linasema kwamba pendekezo hilo “linapingana” na uamuzi wa karibuni wa Mahakama ya Kikatiba iliyounga mkono sheria ya jeshi, ambayo haimruhusu mtu kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Mahakama Kuu imesema kwamba bunge, na si mahakama, ndilo linaweza kufanya haki hiyo itambuliwe kisheria. Kila mwaka, kati ya vijana 500 hadi 700 ambao ni Mashahidi wa Yehova hutupwa gerezani katika Jamhuri ya Korea kwa sababu ya kukataa utumishi wa kijeshi. Kwa muda mrefu, Mashahidi 10,000 hivi wamefungwa kwa sababu hiyo.