Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Unapokuwa Mgonjwa kwa Kula Samaki

Unapokuwa Mgonjwa kwa Kula Samaki

Unapokuwa Mgonjwa kwa Kula Samaki

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI FIJI

Arebonto alitatanika. Hakujua kama ale au asile samaki huyo. Alijua madhara yake, lakini alikuwa na njaa. Naye samaki aliyechomwa alinukia vizuri. Alilemewa na njaa na hivyo akala samaki huyo. Lakini baada ya muda mfupi alianza kuhisi kichefuchefu, maumivu ya tumbo, kutapika na kuharisha, naye akajuta kula samaki huyo.

KUFIKIA wakati rafiki zake walipomkimbiza Arebonto hospitali iliyo kwenye kisiwa chao kidogo cha Pasifiki, alikuwa karibu kupoteza fahamu na kuishiwa na maji mwilini. Alikuwa na maumivu ya kifua, shinikizo la chini la damu, na moyo wake ulipiga polepole. Katika siku chache zilizofuata, mbali na kuumwa na kichwa, kuhisi kizunguzungu, na uchovu, miguu yake ilikufa ganzi, akahisi uchungu alipokojoa, na alihisi vitu baridi vikiwa moto na moto vikiwa baridi. Siku nane baadaye moyo wake ulianza kupiga kwa ukawaida, lakini bado alikuwa amekufa ganzi na aliendelea kuhisi uchovu kwa majuma kadhaa.

Arebonto alikuwa amepatwa na ugonjwa unaosababishwa na sumu kali za asili ambazo huingia katika samaki wanaoliwa ambao huishi kati ya matumbawe ya maeneo yenye joto. Ugonjwa huo unaoitwa ciguatera fish poisoning (CFP), hutukia katika maeneo yenye joto jingi na yale yenye joto la kadiri ya Bahari ya Hindi na Pasifiki na huko Karibea. Katika maeneo hayo, chakula cha kawaida ni samaki.

CFP si ugonjwa mpya. Kwa kweli, uliwadhuru wavumbuzi kutoka Ulaya waliosafiri baharini. Pia, watu wengi wanaoenda likizo siku hizi wamepatwa na ugonjwa huo. Basi inaeleweka kwamba ugonjwa huo umeathiri biashara ya uvuvi na ya utalii katika visiwa vingi. Isitoshe, biashara ya kimataifa ya samaki walio hai na waliogandishwa wanaopatikana kati ya matumbawe imeeneza ugonjwa wa CFP toka maeneo yenye joto hadi sehemu ambako hautambuliwi kwa urahisi. *

Ni nini hufanya samaki wanaoishi kati ya matumbawe wawe na sumu? Je, samaki wenye sumu wanaweza kutambuliwa? Ona mambo ambayo utafiti uliofanywa kwa miaka mingi umefunua.

Kutambua Chanzo

Inadhaniwa kuwa kiumbe mdogo anayeitwa dinoflagellate ndiye chanzo cha sumu inayosababisha ugonjwa wa CFP. * Kiumbe huyo huishi kwenye marijani zilizokufa na kujishikilia kwenye miani. Samaki wadogo hula miani na kumeza sumu inayoitwa ciguatoxin ambayo hutokezwa na dinoflagellate. Samaki hao huliwa na samaki wakubwa ambao pia huliwa na wengine wakubwa zaidi na hivyo sumu huenezwa kutoka samaki mmoja hadi mwingine. Hata hivyo, inaonekana kwamba samaki hawaathiriwi na sumu hiyo.

Ciguatoxin ni mojawapo ya vitu vya asili vyenye sumu hatari zaidi. Lakini jambo la kupendeza ni kwamba “ni jamii chache sana za samaki ambao husababisha CFP,” linasema gazeti la kiserikali la Australia. Sumu hiyo haibadili umbo, harufu, au ladha ya samaki, na haiwezi kuharibiwa kwa kupikwa, kukaushwa, kutiwa chumvi, kuchomwa, au kutiwa marinadi. Katika kisa cha Arebonto, hakukuwa na dalili yoyote ya kuonyesha kwamba samaki huyo alikuwa na sumu hadi Arebonto alipopatwa na maumivu ya tumbo, moyo, na mfumo wa neva.

Uchunguzi na Matibabu

Kwa sasa hakuna njia ya kuchunguza kama mtu ana ugonjwa wa CFP. Ugonjwa huo hutambuliwa kupitia dalili mbalimbali ambazo kwa kawaida huonekana saa kadhaa baada ya kula na unaweza kuthibitishwa kwa kupima mabaki ya samaki. (Ona sanduku kwenye ukurasa unaofuata.) Ikiwa unadhani una CFP, inafaa kumwona daktari. Ingawa hakuna dawa, matibabu yanaweza kupunguza athari za ugonjwa huo, ambazo kwa kawaida hupungua baada ya siku chache. Hata hivyo, ugonjwa wa CFP unaweza kumdhoofisha mtu, na huenda matibabu ya mapema yakazuia madhara yake yasidumu.

Dalili za ugonjwa huo huwa mbaya ikitegemea mambo mbalimbali. Mambo hayo yanatia ndani kiwango cha sumu katika samaki, sehemu za samaki zilizoliwa na kiasi cha samaki aliyeliwa, kiasi cha sumu kilicho tayari katika mwili wa mgonjwa, na mahali samaki huyo alipovuliwa, kwa kuwa inaonekana kwamba sumu hiyo hutofautiana kidogo kutoka eneo moja hadi lingine. Kwa kuwa mwili wa mwanadamu hautokezi kinga ya sumu hiyo, wao huathiriwa zaidi, na hivyo kadiri wanavyokula samaki mwenye sumu ndivyo wanavyopata madhara zaidi! Pia kunywa kileo huzidisha dalili za ugonjwa huo. Kichapo fulani kinachoeleza kuhusu ugonjwa huo ulioenea sana kinasema kwamba, ili mtu asipatwe na madhara hayo tena, anapaswa kuepuka kula samaki kwa miezi mitatu hadi sita baada ya kupatwa na ugonjwa wa CFP.

Dalili mbaya zaidi zinaweza kudumu kwa majuma au miezi na nyakati nyingine kwa miaka kadhaa, na kuwa dalili kama za ugonjwa wa kuchoka daima. Katika visa vichache, kifo hutokea kwa sababu ya mshtuko, kushindwa kupumua, moyo kushindwa kufanya kazi, au kuishiwa na maji mwilini. Hata hivyo, visa kama hivyo hutukia hasa mtu anapokula sehemu za samaki zenye sumu nyingi kama vile kichwa au viungo vya ndani.

Fumbo Linaloendelea

Karibu samaki wote wanaoishi kati ya matumbawe, na wale wanaowala, wanaweza kuwa na sumu hiyo. Lakini hapo pana fumbo. Samaki kutoka tumbawe moja wanaweza kuwa na sumu nyingi, lakini samaki wa jamii hiyohiyo waliovuliwa karibu na hapo huenda wasiwe nayo. Jamii fulani ya samaki inayosemekana kuwa na sumu hiyo katika sehemu moja ya ulimwengu huenda isiwe nayo katika sehemu nyingine. Kwa kuwa haijulikani kiumbe anayeitwa dinoflagellate atatoa sumu wakati gani, si rahisi kujua samaki wenye sumu watapatikana wapi.

Kuongezea tatizo hilo, hakuna njia yenye kutegemeka na isiyogharimu sana ya kupima samaki wenye sumu. Wakitegemea visa vilivyoripotiwa vya CFP, jambo ambalo wataalamu wa afya wanaweza kufanya kwa sasa ni kuwajulisha watu samaki ambao wanapaswa kuepukwa na mahali ambapo hupatikana. Jamii zinazosemekana kuwa hatari sana ni msusa, grouper, nguru, red bass, rockfish, janja, na vilevile mkunga. Kwa kawaida samaki waliokomaa na wakubwa huwa hatari zaidi. Katika nchi fulani ni kinyume cha sheria kuuza samaki wanaoweza kuwa hatari. Hata hivyo, kwa kawaida samaki wa baharini ambao hawali samaki wanaoishi kati ya matumbawe na pia samaki wanaotoka maeneo yasiyo na joto huonwa kuwa salama.

Inatabiriwa kwamba visa vya CFP vitaongezeka. Kwa sehemu, kisababishi kimoja ni kwamba marijani zilizokufa hufanya iwe rahisi kwa kiumbe mwenye sumu anayeitwa dinoflagellate kuongezeka, na ripoti zinaonyesha kwamba idadi kubwa ya matumbawe yanaugua au yanakufa.

Licha ya kwamba ugonjwa wa CFP hautambuliwi kwa urahisi, unaweza kupunguza hatari zake kwa kufuata kanuni fulani za msingi. (Ona sanduku lililo juu.) Karibu Arebonto afe kwa sababu hakufuata kanuni hizo. Alikula kichwa na nyama ya rockfish wa eneo lao anayejulikana kuwa hatari sana. Alikuwa amekula samaki huyo awali bila kuathiriwa na, kama wenyeji wengi wa kisiwa hicho, hilo likamfanya awe na uhakika kupita kiasi.

Je, mambo yaliyotajwa yanamaanisha kwamba unapaswa kuepuka chakula cha baharini, labda unapoenda likizo katika nchi za tropiki? La. Jambo la busara ni kutii maonyo na kuchagua kwa hekima samaki utakayekula.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Kutokana na kutotambuliwa au kutoripotiwa, idadi kamili ya watu ulimwenguni wanaoathiriwa na ugonjwa wa CFP haijulikani. Vyanzo fulani vinakadiria kwamba watu wapatao 50,000 ulimwenguni hupata ugonjwa huo kila mwaka.

^ fu. 9 Dinoflagellate anatokana na jamii ya Gambierdiscus toxicus.

[Sanduku Picha katika ukurasa wa 21]

Dalili za Kawaida

▪ Kuharisha, kichefuchefu, kutapika, kuumwa na tumbo

▪ Kuhisi baridi, kutokwa na jasho, kizunguzungu, kuumwa na kichwa, kuwashwa

▪ Kufa ganzi au kuwashwa kwenye mdomo, mikono, au miguu

▪ Kuhisi vitu baridi vikiwa moto na vitu moto vikiwa baridi

▪ Kuhisi maumivu ya misuli na viungio, na unapokojoa

▪ Moyo kupiga polepole, shinikizo la chini la damu, uchovu

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 21]

Kupunguza Hatari

▪ Uliza wizara ya uvuvi au wataalamu wa samaki kuhusu samaki walio hatari wanaopaswa kuepukwa na mahali ambapo samaki wenye sumu hupatikana.

▪ Epuka kula samaki wanaotoka maeneo ambapo sumu ya ciguatera imeripotiwa karibuni.

▪ Epuka kula samaki wakubwa na waliokomaa wanaoishi kati ya matumbawe.

▪ Usile kichwa au ini au sehemu nyingine za ndani.

▪ Unapovua samaki wanaoishi kati ya matumbawe, ondoa matumbo yao mara moja.

[Picha katika ukurasa wa 20, 21]

Samaki Wanaoweza Kuwa na Sumu

(MAJINA YANAWEZA KUTOFAUTIANA IKITEGEMEA ENEO)

Msusa

“Grouper”

“Rockfish”

Janja

Nguru

Mkunga

[Picha katika ukurasa wa 20]

“Dinoflagellate,” chanzo cha sumu

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 20]

All fish except eel: Illustrated by Diane Rome Peebles - Provided by the Florida Fish and Wildlife Conservation Commission, Division of Marine Fisheries Management; eel: Photo by John E. Randall; dinoflagellate: Image by D. Patterson and R. Andersen, provided courtesy of micro*scope (http://microscope.mbl.edu)

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]

Fish backgrounds: Illustrated by Diane Rome Peebles - Provided by the Florida Fish and Wildlife Conservation Commission, Division of Marine Fisheries Management