Imani ya Mtoto
Imani ya Mtoto
PINDI kwa pindi, Dustin alikuwa akiketi na kusikiliza mama yake alipokuwa akijifunza Biblia pamoja na Shahidi wa Yehova. Ingawa alikuwa na miaka 11 tu, alifikiria mambo kwa uzito, naye aliuliza maswali mengi mazuri. Muda si muda, alimwomba Shahidi aliyekuwa akijifunza na mama yake, ajifunze naye pia. Shahidi huyo aliwahi kuwa mmishonari. Pia Dustin alianza kuwaambia wanashule wenzake mambo aliyokuwa akijifunza.
Dustin alianza kuhudhuria mikutano katika Jumba la Ufalme lililokuwa karibu na mahali walipoishi, na hata alishiriki kujibu maswali wasikilizaji walipoombwa wafanye hivyo. Yeye na ndugu na dada zake wadogo walipomtembelea baba yake mzazi, baba alisisitiza waende kanisani pamoja. Dustin alimweleza kwa nini alipendelea kwenda kwenye Jumba la Ufalme. Baba yake alikubaliana naye na akamruhusu Dustin aende huko.
Jioni moja, baada ya kuhudhuria mkutano fulani kwenye Jumba la Ufalme, mama yake alianza kumtafuta Dustin. Bila kumwambia mama yake, Dustin alimwendea mwangalizi wa Shule ya Huduma ya Kitheokrasi na kumwomba amwandikishe kwenye shule. Mama yake alikubali. Dustin alitazamia kwa hamu hotuba yake ya kwanza. Hata hivyo, wakati huohuo, alianza kuhisi maumivu makali kwenye nyonga, kwa hiyo akapelekwa kwa madaktari mbalimbali ili afanyiwe uchunguzi. Hatimaye, usiku ambao Dustin angetoa hotuba yake kwenye Jumba la Ufalme ukawadia. Wakati huo alikuwa akitumia mikongojo kutembea. Hata ingawa ilionekana wazi kwamba ana maumivu, Dustin alitembea hadi jukwaani bila kutumia mikongojo.
Muda mfupi baadaye, Dustin alichunguzwa na ikagunduliwa kwamba ana kansa ya mifupi (Ewing’s sarcoma). Ugonjwa huo hauwapati watu wengi. Mwaka uliofuata, alilazwa mara nyingi sana kwenye hospitali ya watoto huko San Diego, California. Alipewa matibabu ya kemikali, mnururisho, na hatimaye mguu wake wa kulia na mfupa wa nyonga ukakatwa. Licha ya matibabu hayo yanayoumiza sana, imani yake thabiti na upendo wake kwa Yehova haukupungua. Alipokuwa mnyonge sana asiweze kusoma, mama yake ambaye alishinda naye karibu wakati wote alimsomea kwa sauti.
Hata ingawa hali ya Dustin ilizorota, yeye hakulalamika kamwe. Huku akiendesha kiti chake cha magurudumu, Dustin alifanya mengi kuwatia moyo wagonjwa wengine pamoja na wazazi wao, kutia ndani mgonjwa mmoja aliyekuwa Shahidi. Wafanyakazi wa hospitali hiyo waliona kwamba Dustin na yule kijana mgonjwa aliyekuwa Shahidi walikuwa tofauti na wengine. Waliona kwamba imani yao inawaimarisha.
Dustin alitaka kubatizwa. Kwa hiyo, akiwa amelala kwenye kiti, kwa kuwa alikuwa dhaifu sana asiweze kuketi, wazee Wakristo walipitia naye maswali ambayo wale wanaotaka kubatizwa na kuwa Mashahidi wa Yehova huulizwa. Akiwa na miaka 12 na nusu, Dustin alibatizwa kwenye kusanyiko la mzunguko Oktoba 16, 2004.
Kabla tu ya hotuba ya ubatizo, Dustin alisukumwa akiwa kwenye kiti chake cha magurudumu hadi mahali ambapo wale waliotaka kubatizwa walikuwa wameketi. Walipoombwa wasimame, Dustin ambaye alikuwa amevalia suti yake nzuri, alisimama kwa mguu mmoja huku akijitegemeza kwenye kiti. Alijibu maswali ya ubatizo kwa sauti kubwa iliyosikika wazi. Washiriki wote wa familia ya Dustin, kutia ndani baba yake mzazi na mama yake wa kambo, walikuwepo. Wafanyakazi wa hospitali na wazazi wa watoto wenye kansa katika hospitali hiyo walikuwepo pia.
Siku iliyofuata ubatizo wake, Dustin alilazwa tena hospitalini. Kansa ilikuwa imeenea kwenye mifupa yake yote. Alipoendelea kudhoofika na kutambua kwamba anakaribia kufa, Dustin alimwuliza mama yake kama alikuwa anakaribia kufa. Mama yake akauliza: “Mbona wauliza hivyo? Waogopa kufa?”
“La,” akajibu. “Nitafunga tu macho, na nitakapoyafungua wakati wa ufufuo, itakuwa ni kana kwamba niliyafunga kwa sekunde mmoja tu. Sitahisi maumivu tena.” Kisha akasema, “Nina wasiwasi kuhusu familia yetu.”
Dustin alikufa mwezi uliofuata. Hotuba yake ya mazishi ilihudhuriwa na madaktari, wauguzi, familia za wafanyakazi wa hospitali, walimu, na majirani. Washiriki wote wa familia ya Dustin, walio Mashahidi wa Yehova na wale ambao si Mashahidi walihudhuria pia. Dustin alikuwa ameomba kwamba wale wote watakaohudhuria hotuba yake ya mazishi wapewe ushuhuda mzuri kuhusu imani yake. Mwangalizi wa Shule ya Huduma ya Kitheokrasi ambaye alimpa Dustin hotuba yake ya kwanza na ya mwisho, alitoa hotuba nzuri na yenye kuimarisha imani kwa umati uliojaa kwenye jumba hata ikabidi wengi wasimame.
Wale waliohudhuria hotuba ya mazishi ya Dustin walipewa karatasi iliyokuwa na Maandiko mawili ambayo Dustin alipenda sana, yaani, Mathayo 24:14; 2 Timotheo 4:7. Imani yake yenye nguvu na utimilifu wake uliwatia nguvu wote waliomjua. Tunatazamia kwa hamu kumwona tena atakapofufuliwa.—Imesimuliwa na Shahidi aliyejifunza na Dustin.
[Blabu katika ukurasa wa 27]
“Nimepigana pigano zuri, nimekimbia mwendo mpaka mwisho, nimeishika imani.”—2 Timotheo 4:7
[Picha katika ukurasa wa 26]
Juu: Dustin, alipokuwa na afya
[Picha katika ukurasa wa 26]
Chini: Dustin akibatizwa akiwa na umri wa miaka 12 na nusu