Kutia Damu Mishipani—Je, Kutaendelea?
Kutia Damu Mishipani—Je, Kutaendelea?
“Matibabu yanayohusisha kutia damu mishipani yataendelea kuwa kama kutembea kwenye msitu, ambako licha ya kwamba mtu anajua vijia vyake, bado anahitaji kutembea kwa uangalifu, na huenda kukawa na hatari zisizotazamiwa na wale wasiokuwa waangalifu.”—Ian M. Franklin, profesa wa matibabu yanayohusisha kutia damu mishipani.
TANGU ugonjwa wa UKIMWI ulipofanya watu ulimwenguni pote wajihadhari zaidi na damu katika miaka ya 1980, jitihada za kumaliza “madhara yasiyoonekana” ya damu zimezidishwa. Lakini matatizo makubwa yangalipo. Mnamo Juni 2005, Shirika la Afya Ulimwenguni lilisema hivi: “Uwezekano wa kutiwa damu iliyo salama . . . unatofautiana sana kutoka nchi moja hadi nyingine.” Kwa nini?
Katika nchi nyingi hakuna utaratibu wa kitaifa wa kuweka viwango vya usalama katika kukusanya, kupima, na kusafirisha damu na bidhaa za damu. Nyakati nyingine damu huhifadhiwa kwa njia hatari kama vile kwenye friji zilizoundwa ili kutumiwa nyumbani au kwenye masanduku ya kuhifadhi baridi! Kwa kuwa hakuna viwango vya usalama, wagonjwa wanaweza kuathiriwa na damu iliyokusanywa kutoka kwa watu walio umbali wa mamia au maelfu ya kilometa.
Damu Isiyo na Magonjwa —Jambo Lisilowezekana
Nchi kadhaa zinadai kwamba damu wanayokusanya ni salama kuliko ilivyokuwa zamani. Lakini bado inafaa kujihadhari. “Taarifa” iliyotayarishwa na mashirika matatu ya damu nchini Marekani inasema hivi katika ukurasa wake wa kwanza: “ONYO: Kwa kuwa damu nzima na sehemu kuu za damu hutokana na damu ya binadamu, huenda zikapitisha viini vya magonjwa kama vile virusi. . . . Kuchagua kwa uangalifu watu wanaotoa damu na kutumia mbinu za kuchunguza damu hakuondoi hatari hizo.”
Peter Carolan, ambaye ni afisa mkuu wa Shirika
la Kimataifa la Msalaba Mwekundu na Mwezi Mwekundu, ana sababu nzuri ya kusema hivi: “Huwezi kuhakikishiwa kwamba damu ni salama kabisa.” Anaongeza hivi: “Sikuzote kutakuwa na maambukizo mapya, ambayo kwa sasa hayawezi kuchunguzwa.”Vipi viini vipya vinavyopitishwa kupitia damu vikitokea, viini ambavyo kama UKIMWI, vinabaki bila kugunduliwa na bila kumwathiri mtu kwa muda mrefu? Alipokuwa akizungumza kwenye warsha ya kitiba huko Prague, katika Jamhuri ya Cheki, mnamo Aprili 2005, Dakt. Harvey G. Klein wa Taasisi za Afya za Marekani, alisema kwamba uwezekano huo unapaswa kufikiriwa kwa uzito. Aliongezea: “Wale wanaokusanya sehemu kuu za damu hawatakuwa tayari vya kutosha kuzuia ugonjwa unaopitishwa kwa kutiwa damu mishipani kuliko walivyokuwa UKIMWI ulipogunduliwa.”
Makosa na Madhara ya Kutiwa Damu Mishipani
Ni nini baadhi ya hatari kubwa wanazokabili wagonjwa wanaotiwa damu katika nchi zilizositawi? Kuna makosa yanayotukia damu inaposhughulikiwa na pia kuna madhara ya mfumo wa kinga. Kulingana na uchunguzi uliofanywa Kanada mnamo 2001, gazeti Globe and Mail liliripoti kwamba uhai wa maelfu ya wagonjwa waliotiwa damu ulikuwa hatarini kwa sababu ya makosa kama vile, “kupima damu ya mgonjwa tofauti, kutia vibandiko visivyo sahihi, na kuagiza damu isiyofaa kwa ajili ya mgonjwa.” Kati ya mwaka wa 1995 na 2001, watu 441 hivi nchini Marekani walikufa kwa sababu ya makosa kama hayo.
Wale wanaotiwa damu ya mtu mwingine wanakabili hatari sawa na za watu wanaopandikizwa viungo. Mara nyingi mfumo wa kinga hukataa tishu kutoka kwa mtu mwingine. Katika visa fulani, kutiwa damu mishipani kunaweza kuzuia utendaji wa kawaida wa mfumo wa kinga. Mfumo huo unapodhoofishwa, mgonjwa anaweza kupatwa na maambukizo baada ya upasuaji na kuathiriwa na virusi ambavyo havikuwa vikitenda. Si ajabu kwamba Profesa Ian M. Franklin, aliyenukuliwa awali, aliwahimiza wataalamu wa afya ‘wafikirie mambo kwa uangalifu sana kabla ya kuwatia wagonjwa damu.’
Wataalamu Watoa Maoni Yao Waziwazi
Wakijua hilo, wahudumu wengi wa afya wanachanganua kwa makini zaidi matibabu yanayohusisha kutiwa damu mishipani. Kitabu Dailey’s Notes on Blood charipoti hivi: “Madaktari fulani wanasema kuwa [damu ya mtu mwingine] ni dawa hatari sana na kwamba ikiwa ingekaguliwa kwa kutumia viwango vinavyotumiwa kukagua dawa nyinginezo, ingepigwa marufuku.”
Mwishoni mwa 2004, Profesa Bruce Spiess alisema hivi kuhusu kumtia mgonjwa anayefanyiwa upasuaji wa moyo, mojawapo ya sehemu kuu za damu: “Ikiwa kuna makala zozote za [kitiba] zinazounga mkono wazo la kwamba kumtia mgonjwa mojawapo ya sehemu kuu za damu huboresha hali yake baada ya upasuaji, makala hizo ni chache sana.” Ama kweli, anaandika kwamba kutiwa damu “kunaweza kusababisha madhara mengi katika karibu visa vyote isipokuwa visa vya majeraha mabaya,” na kunaongeza “hatari ya kupatwa na nimonia, maambukizo, mshtuko wa moyo, na kiharusi.”
Watu wengi hushangaa kujua kwamba viwango vya kuwatia watu damu mishipani vinatofautiana sana. Hivi karibuni, Dakt. Gabriel Pedraza aliwakumbusha madaktari wenzake nchini Chile kwamba “kuwatia watu damu mishipani ni mbinu ambayo haina viwango mahususi,” jambo ambalo hufanya iwe “vigumu . . . kufuata viwango vilevile ulimwenguni pote.” Basi si ajabu kwamba Brian McClelland, msimamizi wa Huduma za Kuwatia Watu Damu huko Edinburgh na Scotland, anawaambia madaktari “wakumbuke kwamba kutia damu mishipani ni kupandikiza kiungo, kwa hiyo huo ni uamuzi mzito.” Anapendekeza madaktari
wajiulize hivi, “Ikiwa ingekuwa mimi au mtoto wangu, je, ningekubali matibabu yanayohusisha damu?”Kwa kweli, wahudumu wengi wa afya wana maoni sawa na ya mtaalamu wa damu aliyemwambia mwandishi wa Amkeni! hivi: “Sisi wataalamu wa matibabu yanayohusisha damu hatupendi kutiwa wala kuwatia watu damu.” Ikiwa hivyo ndivyo baadhi ya wataalamu wa afya wenye uzoefu mwingi wanavyohisi, sembuse wagonjwa?
Je, Mbinu za Matibabu Zitabadilika?
‘Ikiwa kuna hatari nyingi za matibabu yanayohusisha kutia damu,’ huenda ukajiuliza, ‘kwa nini damu bado inatumiwa sana, hasa wakati huu ambapo kuna matibabu ya badala?’ Sababu moja ni kwamba madaktari wengi hawataki kubadili mbinu zao za matibabu au hawajui matibabu ya badala yanayotumiwa sasa. Kulingana na makala katika jarida Transfusion, “madaktari huamua kuwatia watu damu kwa kutegemea mambo waliyojifunza zamani, uzoefu wao, na maoni yao baada ya kumpima mgonjwa.”
Ustadi wa daktari wa upasuaji husaidia kupunguza kiasi cha damu inayopotea wakati wa upasuaji. Dakt. Beverley Hunt, wa London, Uingereza, anaandika kwamba “kiasi cha damu inayopotea hutofautiana sana ikitegemea daktari wa upasuaji, na kuna uhitaji mkubwa wa kuwazoeza madaktari wa upasuaji mbinu bora za kuzuia kuvuja damu nyingi wakati wa upasuaji.” Wengine wanadai kwamba gharama za kutumia mbinu za badala ni kubwa sana ingawa ripoti zinaonyesha kwamba sivyo ilivyo. Hata hivyo, madaktari wengi watakubaliana na msimamizi wa tiba Dakt. Michael Rose, ambaye anasema: “Mgonjwa yeyote anayefanyiwa upasuaji bila kutiwa damu ndiye anayepokea matibabu bora zaidi.” *
Bila shaka ungependa kupata matibabu bora zaidi, sivyo? Ikiwa ndivyo, maoni yako yanapatana na ya wale waliokupa gazeti hili. Tafadhali soma makala zinazofuata ili ujue msimamo wao thabiti kuhusu kutiwa damu mishipani.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 19 Ona sanduku “Matibabu ya Badala,” kwenye ukurasa wa 8.
[Picha katika ukurasa wa 6]
“Fikirieni mambo kwa uangalifu sana kabla ya kuwatia wagonjwa damu.”—Profesa Ian M. Franklin
[Picha katika ukurasa wa 6]
“Ikiwa ingekuwa mimi au mtoto wangu, je, ningekubali matibabu yanayohusisha damu?”—Brian McClelland
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
Vifo Vinavyosababishwa na TRALI
Ugonjwa wa TRALI, yaani, majeraha mabaya ya mapafu yanayosababishwa na kutiwa damu mishipani, uligunduliwa katika miaka ya 1990. Ugonjwa huo ni mojawapo ya athari mbaya sana ambazo mtu hupata mfumo wa kinga unapokataa damu aliyotiwa. Inajulikana kwamba mamia ya watu hufa kila mwaka kutokana na TRALI. Hata hivyo, wataalamu husema kwamba idadi hiyo inaweza kuwa kubwa kwani wahudumu wengi wa afya hawatambui dalili zake. Ingawa haijulikani kabisa ni nini husababisha ugonjwa huo, kulingana na gazeti New Scientist, damu inayousababisha “hutolewa hasa na watu ambao wametiwa aina mbalimbali za damu, kama vile . . . wale ambao wametiwa damu mara kadhaa.” Ripoti moja inasema kwamba nchini Marekani na Uingereza, TRALI yaelekea kuwa mojawapo ya visababishi vikuu vya vifo vinavyotokana na kutiwa damu mishipani, na hivyo kuwa “tatizo kubwa kwa wale wanaohifadhi damu kuliko magonjwa yanayojulikana sana kama vile virusi vya UKIMWI.”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Sehemu Kuu za Damu
Kwa kawaida watu wanaotoa damu hutoa damu nzima. Hata hivyo katika visa vingi, watu hutoa plazima tu. Ingawa katika nchi fulani watu hutiwa damu nzima, mara nyingi damu hugawanywa katika sehemu zake kuu kabla ya kupimwa na kutumiwa katika matibabu. Acha tuzungumzie sehemu nne kuu za damu, matumizi yake, na asilimia ambayo kila mojawapo ya sehemu hizo hufanyiza.
PLAZIMA hufanyiza kati ya asilimia 52 na 62 ya damu. Plazima ni umajimaji wenye rangi hafifu ya manjano. Chembe za damu, protini, na vitu vingine huelea na kusafirishwa kupitia plazima.
Maji hufanyiza asilimia 91.5 ya plazima. Protini, ambayo hutumiwa kutokeza visehemu vya plazima, hufanyiza asilimia 7 ya plazima (kutia ndani albumini ambayo ni asilimia 4; globulini, asilimia 3 hivi; na fibrinojeni, chini ya asilimia 1). Vitu vingine kama vile virutubishi, homoni, gesi, elektroliti, vitamini, na takataka za nitrojeni hufanyiza asilimia 1.5 inayosalia.
CHEMBE NYEUPE ZA DAMU (lukositi) hufanyiza chini ya asilimia 1 ya damu. Chembe hizo hushambulia na kuharibu viini hatari vinavyoingia mwilini.
VIGANDISHA DAMU (thrombositi) hufanyiza chini ya asilimia 1 ya damu. Chembe hizo hugandisha damu na kuizuia isitoke mwilini kupitia kwenye vidonda.
CHEMBE NYEKUNDU ZA DAMU (erithrositi) hufanyiza kati ya asilimia 38 na 48 ya damu. Chembe hizo hutegemeza uhai wa tishu kwa kuingiza oksijeni ndani ya tishu na kuondoa kaboni dioksidi.
Kama vile plazima inavyoweza kugawanywa katika visehemu kadhaa, ndivyo sehemu zile nyingine kuu za damu zinavyoweza kugawanywa. Kwa mfano, hemoglobini ni kisehemu cha chembe nyekundu ya damu.
[Picha]
PLAZIMA
MAJI ASILIMIA 91.5
PROTINI ASILIMIA 7
ALBUMINI
GLOBULINI
FIBRINOJENI
VITU VINGINE ASILIMIA 1.5
VIRUTUBISHI
HOMONI
GESI
ELEKTROLITI
VITAMINI
TAKATAKA ZA NITROJENI
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 8]
Page 9: Blood components in circles: This project has been funded in whole or in part with federal funds from the National Cancer Institute, National Institutes of Health, under contract N01-CO-12400. The content of this publication does not necessarily reflect the views or policies of the Department of Health and Human Services, nor does mention of trade names, commercial products, or organizations imply endorsement by the U.S. Government
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Matibabu ya Badala
Katika miaka sita iliyopita, Halmashauri za Uhusiano na Hospitali za Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote, zimewapa wataalamu wa tiba makumi ya maelfu ya nakala za video yenye kichwa Transfusion-Alternative Strategies—Simple, Safe, Effective. * Video hiyo inapatikana katika lugha 25 hivi. Katika video hiyo madaktari maarufu ulimwenguni wanazungumzia mbinu zenye mafanikio zinazotumiwa sasa kuwatibu wagonjwa bila kuwatia damu mishipani. Watu wanazingatia ujumbe wa video hiyo. Kwa mfano, baada ya kuitazama mwishoni mwa mwaka wa 2001, Huduma ya Kitaifa ya Damu (NBS) ya Uingereza iliwatumia wasimamizi wa hifadhi za damu na wataalamu wa damu kotekote nchini barua iliyoambatanishwa na nakala ya video hiyo. Walitiwa moyo waitazame kwa sababu “idadi ya watu wanaotambua kwamba kuepuka kutia damu mishipani inapowezekana ni mojawapo ya malengo ya matibabu mazuri, inazidi kuongezeka.” Barua hiyo ilisema kwamba “habari [iliyo katika video hiyo] inastahili kusifiwa na inaungwa mkono kabisa na NBS.”
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 57 Wasiliana na Shahidi wa Yehova ikiwa ungetaka kutazama DVD yenye kichwa Transfusion Alternatives—Documentary Series, iliyotengenezwa na Mashahidi wa Yehova.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]
Kugawanya Damu Matumizi ya Visehemu vya Damu Katika Tiba
Sayansi na teknolojia hufanya iwezekane kuchunguza na kugawanya damu. Kwa mfano: Maji ya bahari ambayo asilimia 96.5 ni maji, yanaweza kugawanywa ili kutenganisha vitu vilivyo ndani yake kama vile magnesi, bromini, na chumvi. Hali kadhalika, plazima hufanyiza zaidi ya asilimia 50 ya damu. Zaidi ya asilimia 90 ya plazima ni maji na inaweza kugawanywa ili kutokeza visehemu mbalimbali kama vile protini inayoitwa albumini, fibrinojeni, na globulini mbalimbali.
Huenda daktari akapendekeza mgonjwa atiwe kiasi kikubwa cha kisehemu cha plazima. Mojawapo ya visehemu hivyo ina protini nyingi nayo hutenganishwa kwa kugandisha na kisha kuyeyusha plazima. Kisehemu hicho kisichoweza kuyeyuka kina vitu vingi vinavyofanya damu igande na kwa kawaida wagonjwa hutiwa kisehemu hicho ili kufanya damu iache kuvuja. Matibabu mengine yanaweza kuhusisha matumizi ya bidhaa ambazo zina kiasi kidogo sana au kikubwa sana cha kisehemu fulani cha damu. * Protini fulani zinazotokana na plazima hutumiwa katika dawa za chanjo ambazo zinaweza kuongeza kinga za mwili baada ya mtu kupata maambukizo fulani. Karibu visehemu vyote vya damu ambavyo hutumiwa katika matibabu vina protini ambayo imetolewa katika plazima.
Kulingana na gazeti Science News, “wanasayansi wamegundua tu mamia kadhaa ya maelfu ya protini katika damu.” Kadiri wanavyozidi kuifahamu damu, ndivyo bidhaa mpya zinazotengenezwa kutokana na protini hizo zitakavyotokezwa.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 63 Visehemu vilivyotolewa katika damu ya wanyama hutumiwa pia kutengeneza bidhaa fulani.
[Picha katika ukurasa wa 6, 7]
Wahudumu fulani wa afya hujihadhari sana wasiguse damu