Mashua ya Galilaya—Hazina ya Nyakati za Biblia
Mashua ya Galilaya—Hazina ya Nyakati za Biblia
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ISRAEL
BAADHI ya matukio muhimu ya huduma ya Yesu yalitendeka katika Bahari ya Galilaya. Mwana wa Mungu alitembea juu ya maji, akatuliza mawimbi yenye dhoruba, akalisha maelfu, na kuponya wagonjwa kwenye ziwa hilo na kwenye fuo zake.
Mnamo 1986, uvumbuzi wa ajabu ulifanywa kwenye sakafu ya bahari hiyo karibu na jiji la kale la Kapernaumu. Uvumbuzi huo ulikuwa mashua iliyokuwa imetumiwa kusafiri katika bahari hiyo wakati wa huduma ya Yesu. Ilipatikanaje? Na tunaweza kujifunza nini kutokana mashua hiyo?
Yavumbuliwa kwa Sababu ya Ukame
Ukosefu wa mvua ya kutosha kwa miaka mingi na kiangazi kikali cha mwaka wa 1985, yalifanya maji ya Bahari ya Galilaya yapungue sana na pia maji yake yalitumiwa kunyunyiza mashamba. Kiwango cha maji kilishuka sana hivi kwamba baadhi ya maeneo yenye matope yaliyokuwa yamefunikwa kwa maji kwa muda mrefu yakaonekana. Wanaume wawili ambao ni ndugu kutoka kwa jamii fulani ya wakulima walioishi karibu, waliiona hiyo kuwa nafasi ya pekee ya kutafuta hazina zilizofichwa. Walipokuwa wakitembea juu ya maeneo hayo yenye matope, waliona sarafu kadhaa za shaba na misumari michache mizee. Kisha wakaona kitu chenye umbo la yai. Umbo hilo lilikuwa la mashua ya kale iliyokuwa imefunikwa kwa matope. Kwa kweli walikuwa wamepata hazina!
Wachimbuzi wa vitu vya kale hawakutazamia kamwe kupata katika Bahari ya Galilaya, mashua iliyoundwa miaka 2,000 iliyopita. Walifikiri kwamba mbao zozote zingalikuwa zimeliwa na kuharibiwa kabisa na vijiumbe. Hata hivyo, sarafu zilizopatikana mahali hapo na mbinu za kukadiria tarehe ziliwafanya wataalamu wakate kauli kwamba mashua hiyo ni ya karne ya kwanza K.W.K. au karne ya kwanza W.K. Kwa kustaajabisha, mashua hiyo ilikuwa imehifadhiwa vizuri. Hilo liliwezekanaje?
Inaonekana kwamba mashua hiyo ilikaa mahali palepale bila kuguswa, na hivyo sehemu yake ya chini ikafunikwa kwa mchanga-tope. Baada ya muda, mchanga-tope ukawa mgumu. Mashua hiyo ya kale ikahifadhiwa kwa miaka 2000 hivi!
Habari za kupatikana kwa mashua hiyo zilipoenea, watu walianza kuiita Mashua ya Yesu. Kwa kweli, hakuna aliyedai kwamba mashua hiyo ilitumiwa na Yesu na wanafunzi wake. Hata hivyo, wanahistoria na wasomi wa Biblia wamevutiwa na mashua hiyo kwa sababu ni ya kale na kwa sababu inafanana na mashua zinazotajwa katika masimulizi ya injili.
Mashua hiyo ina urefu wa meta 8.2 na upana wa meta 2.3. Mjenzi wake alitumia mbinu tofauti ya ujenzi. Badala ya kupigilia vipande virefu vya mbao kwenye viunzi, aliviunganisha moja kwa moja kwenye uti wa mashua. Kisha akajenga sehemu zake za kando kufanyiza umbo lake. Mbinu hiyo ilitumika sana kujenga mashua zilizotumiwa kusafiri katika Bahari ya Mediterania. Hata hivyo, huenda ikawa mashua ya Galilaya ilibadilishwa ili ifae kusafiri katika ziwa la Galilaya.
Ni wazi kwamba mashua hiyo ilikuwa na tanga moja ya mraba. Kwa kuwa ilikuwa na makasia manne inaonekana kwamba iliendeshwa na mabaharia watano, yaani, wapiga-makasia wanne na nahodha mmoja. Hata hivyo, mashua hiyo ingeweza kubeba watu wanane au zaidi. Ni rahisi kuwazia mashua yenye ukubwa kama huo unaposoma kuhusu wanafunzi saba ambao walikuwa wakivua samaki walipomwona Yesu baada ya ufufuo wake.—Yohana 21:2-8.
Bila shaka, mashua ya Galilaya ilikuwa na tezi kwa ajili ya kuhifadhi nyavu kubwa za uvuvi. Sakafu hiyo ya tezi iliandaa mahali palipofichika ambapo mvuvi aliyechoka angeweza kupumzika. Marko 4:38) Imesemekana kwamba huenda “mto” huo ulikuwa mfuko uliojaa mchanga uliotumiwa kusawazisha uzito wa mashua. *
Huenda Yesu alikuwa katika sehemu kama hiyo ya mashua kwani dhoruba ilipotokea, “alikuwa katika tezi, akiwa amelalia mto.” (Wavuvi Katika Bahari ya Galilaya
Wazia umo katika mashua kama hiyo katika karne ya kwanza. Ungeona nini unaposafiri kwenye Bahari ya Galilaya? Kuna wavuvi, baadhi yao wakiwa katika mashua ndogo huku wengine wakitembea katika maji yasiyo na kina kirefu na kutupa nyavu zao. Kwa ustadi, wanatumia mkono mmoja tu kuvuta nyavu zao za mviringo ambazo zimefungiliwa vitu vizito kandokando. Nyavu hizo zina kipenyo cha kati ya meta 6 na 8. Nyavu hizo hujitandaza juu ya uso wa maji, kisha zinazama na kunasa samaki. Mvuvi hukusanya samaki kwa kukokota wavu hadi ufuoni au kwa kupiga mbizi na kubeba wavu pamoja na samaki. Biblia inasema kwamba Simoni na Andrea ‘walitupa’ nyavu zao. Huenda walifanya hivyo kwa njia kama ile iliyotajwa hapa.—Marko 1:16.
Huenda ukaona wavuvi kadhaa wakizungumza kwa msisimko huku wakitayarisha wavu wa kukokotwa. Wavu huo unaweza kuwa na urefu wa meta 300, na kimo cha meta 8 kwenye sehemu ya katikati, ukiwa na kamba za kuvuta kwenye miisho yake. Wavuvi huchagua mahali watakapovua, kisha baadhi yao huenda ufuoni wakiwa wameshikilia kamba moja ya kukokota wavu huo. Mashua huingia majini na kusonga mbele kwa njia iliyonyooka, huku ikivuta wavu huo na kuunyoosha kabisa. Kisha mashua hiyo hugeuka na kuvuta wavu huo polepole na kufanyiza nusu duara kuelekea ufuoni. Wavuvi waliosalia hushuka nchi kavu wakiwa wameshika upande wa pili wa kamba ya kuvutia. Vikundi hivyo viwili vya wavuvi vinapokaribiana, wao huvuta samaki hadi ufuoni.—Mathayo 13:47, 48.
Kule mbali unamwona mvuvi akitumia ndoano. Wakati fulani Yesu alimwambia Petro atupe ndoano ndani ya bahari hii. Unaweza kuwazia jinsi Petro alivyostaajabu alipovua samaki na kupata sarafu ya fedha kinywani mwake. Sarafu hiyo ilitosha kulipa kodi ya hekalu.—Mathayo 17:27.
Giza linapoingia kimya hutanda kwenye ziwa hilo. Kwa ghafula, kimya hicho hukatizwa kwa makelele ya wavuvi wanaopigapiga miguu yao kwenye mashua na kupiga maji kwa makasia ili kutokeza kelele nyingi ajabu. Kwa nini? Wameshusha nyavu majini katika njia ambayo samaki, wakiwa wameogopeshwa na kelele hizo, huelekea moja kwa moja mtegoni. Wavu huo uliosimama wima, usioweza kuonekana gizani, umeundwa kwa njia ya kwamba samaki hunaswa kwa urahisi. Nyavu hizo hushushwa mara nyingi usiku wote. Asubuhi nyavu hizo husafishwa na kuanikwa. Huenda ukajiuliza, ‘Je, nyavu kama hizo ndizo zilitumika kuvua samaki kimuujiza kama inavyofafanuliwa kwenye Luka 5:1-7?’
Kazi ya Kurekebisha
Acha turudi nyakati zetu. Ni nini kilichoipata mashua iliyofukuliwa? Ingawa haikuwa imeharibika, mbao za mashua hiyo hazikuwa ngumu kwani zilikuwa zimelowa. Haingeweza kuchimbuliwa moja kwa moja kutoka kwenye matope. Ingesikitisha sana ikiwa mashua hiyo iliyokuwa imedumu kwa muda mrefu ingeharibiwa ilipokuwa ikifukuliwa! Kwa kuwa maji ya ziwa hilo yangeongezeka tena, ukuta wa kuzuia maji ulijengwa kuzunguka eneo hilo. Mitaro ilichimbwa chini ya mashua hiyo ili kuingiza vitu vya kuitegemeza. Kisha matope yalipokuwa yakiondolewa kwa uangalifu, sehemu ya ndani na nje ya mashua hiyo ilipuliziwa kemikali fulani ya kuiimarisha.
Kazi nyingine ngumu ilikuwa kusafirisha mashua hiyo hadi kwenye eneo lililokuwa meta 300 kutoka hapo ili kuihifadhi. Kemikali ambayo mashua hiyo ilikuwa imepuliziwa iliimarisha sana, hata hivyo iwapo ingetikiswa ghafula, mbao za mashua hiyo zingevunjika-vunjika. Watu waliokuwa wakishughulikia kuhifadhi mashua hiyo walibuni njia bora ya kusuluhisha tatizo hilo. Walitoboa shimo kwenye ukuta uliozunguka na kuruhusu maji yaingie. Kwa mara ya kwanza baada ya karne nyingi, mashua hiyo, iliyokuwa imepuliziwa kemikali ya kuiimarisha, ilielea kwenye Bahari ya Galilaya.
Tangi fulani lilijengwa kwa saruji ili litumiwe katika kazi ya kuhifadhi mashua hiyo. Kazi hiyo iliendelea kwa miaka 14. Tatizo lilizuka viluwiluwi wa mbu walipojaa ndani ya tangi hilo na kuwatatiza wale waliohitaji kuingia humo kushughulikia mashua hiyo. Hata hivyo, wahifadhi hao
walitumia mbinu ya kiasili ambayo imetumiwa tangu zamani kutatua tatizo hilo. Walitumia samaki kadhaa wanaoitwa samaki wa Mtakatifu Petro, ambao walikula viluwiluwi hao na kusafisha maji.Wakati wa kukausha mashua hiyo ukafika. Bado mashua hiyo ilikuwa hafifu sana isiweze kuachwa ikauke yenyewe. Maji yaliyokuwa yamefyonzwa na mbao yalihitaji kuondolewa na mahali pake kuwe na kitu kingine. Wahifadhi hao walitumia mbinu fulani ya kuondoa maji na kuingiza nta iliyochanganywa na maji ambayo iliwezesha mbao hizo kukauka bila kubadili umbo.
Kazi ya kuihifadhi ilipokamilika, ilikuwa wazi kwamba mashua hiyo haikuwa ya kifahari. Ilikuwa imeundwa kwa aina 12 za mbao. Kwa nini? Huenda sababu moja ikawa kwamba mbao hazikupatikana kwa urahisi wakati huo. Lakini yaelekea kwamba mwenyewe hakuwa tajiri. Mashua hiyo ilikuwa imerekebishwa mara nyingi sana kabla ya kuzama kwenye bahari hiyo.
Huenda mashua hiyo ya Galilaya haina uhusiano wowote na Yesu. Hata hivyo, ni hazina kwa watu wengi. Inawapa nafasi ya kuwazia mambo yalivyokuwa katika Bahari ya Galilaya karne nyingi zilizopita wakati wa matukio muhimu ya huduma ya Yesu alipokuwa duniani.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 12 Ona makala “Kwenye Bahari ya Galilaya,” katika Mnara wa Mlinzi la Agosti 15, 2005, ukurasa wa 8, ambalo pia limechapishwa na Mashahidi wa Yehova.
[Picha katika ukurasa wa 15]
Wafanyakazi walitoa matope kwa uangalifu ndani ya mashua hiyo
[Picha katika ukurasa wa 15]
Mashua hiyo ikiwa imepuliziwa kemikali ya kuimarisha
[Picha katika ukurasa wa 15]
Baada ya miaka 2,000 hivi, mashua hiyo ilielea tena
[Picha katika ukurasa wa 15]
Mfano wa jinsi ambavyo huenda mashua hiyo ilionekana katika karne ya kwanza
[Picha katika ukurasa wa 15]
Mashua ya Galilaya—baada ya kazi ya kuihifadhi kukamilika
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]
All photos except model and sea: Israel Antiquities Authority - The Yigal Allon Center, Ginosar