Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Thamani Halisi ya Damu

Thamani Halisi ya Damu

Thamani Halisi ya Damu

“Wanadamu wote hutegemea kitu kimoja ili wawe hai: damu. Hiyo ndiyo nguvu ya uhai iliyo katika wanadamu wote, haidhuru rangi, jamii, au dini.” —Msimamizi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

BILA shaka, maneno hayo ni ya kweli kwa kadiri fulani. Damu ni muhimu kwa uhai wa wanadamu wote. Ni umajimaji wenye thamani. Lakini je, unasadiki kwamba ni jambo la hekima kwa wanadamu kuwapa wenzao umajimaji huo kwa sababu za kitiba?

Tumeona kuwa viwango vya usalama wa damu ulimwenguni vinatofautiana sana, na matibabu yanayohusisha damu ni hatari kuliko wengi wanavyofikiri. Isitoshe, madaktari hawaafikiani kuhusu matumizi ya damu ikitegemea elimu, ustadi, na maoni yao. Hata hivyo, madaktari wengi wanasita kuwatia wagonjwa damu. Idadi ya madaktari wanaopendelea matibabu yasiyohusisha damu inazidi kuongezeka.

Hilo linatufanya tufikirie tena swali lililozushwa mwanzoni mwa makala ya kwanza ya mfululizo huu. Ni nini kinachoifanya damu iwe na thamani kubwa sana? Kwa kuwa matumizi ya damu katika tiba yanazidi kuwa hatari, je, damu inaweza kutumiwa kwa kusudi lingine?

Maoni ya Muumba Kuhusu Damu

Hapo kale katika siku za Noa, ambaye ni babu ya wanadamu wote, Mungu aliweka sheria fulani muhimu. Aliwaruhusu wanadamu kula nyama ya wanyama, lakini akawakataza kula damu. (Mwanzo 9:4) Pia alionyesha sababu iliyomfanya aweke sheria hiyo alipohusianisha damu na nafsi au uhai wa kiumbe. Baadaye alisema: “Nafsi ya mwili iko katika damu.” Damu ni takatifu machoni pa Muumba. Inawakilisha zawadi ya uhai yenye thamani ambayo kila nafsi iliyo hai inayo. Mungu aliirudia tena na tena kanuni hiyo.—Mambo ya Walawi 3:17; 17:10, 11, 14; Kumbukumbu la Torati 12:16, 23.

Muda mfupi baada ya Dini ya Kikristo kuanzishwa miaka 2000 hivi iliyopita, waamini walipewa amri ya Mungu iliyowataka “wajiepushe . . . na damu.” Katazo hilo halikutegemea masuala ya kiafya bali lilitegemea utakatifu wa damu. (Matendo 15:19, 20, 29) Watu fulani husisitiza kwamba katazo hilo kutoka kwa Mungu linahusu tu kula damu. Hata hivyo, neno “wajiepushe” linaeleweka vizuri. Iwapo daktari angetuambia tujiepushe na pombe, bila shaka hatungefikiri kwamba ni sawa kutiwa pombe mishipani mwetu.

Biblia inaeleza sababu inayofanya damu iwe takatifu sana. Damu iliyomwagwa ya Yesu Kristo, ambayo iliwakilisha uhai wake wa kibinadamu alioutoa kwa ajili ya wanadamu, ni muhimu sana kwa tumaini la Wakristo. Damu hiyo ndiyo msingi wa msamaha wa dhambi na wa tumaini la uzima wa milele. Kwa kujiepusha na damu, Mkristo huonyesha anaamini kwamba damu ya Yesu Kristo tu ndiyo inayoweza kumkomboa na kuokoa uhai wake.—Waefeso 1:7.

Mashahidi wa Yehova wanajulikana kwa kushikamana sana na amri hiyo ya Biblia. Wao hukataa katakata kutiwa damu nzima au mojawapo ya sehemu kuu za damu, yaani, chembe nyekundu, plazima, chembe nyeupe, na vigandisha damu. Biblia haisemi chochote kuhusu visehemu vidogo vinavyotokana na sehemu hizo kuu za damu au bidhaa ambazo zina visehemu hivyo. Kwa hiyo, kila Shahidi hufanya uamuzi wake mwenyewe kuhusu visehemu hivyo. Je, msimamo huo unaotegemea Biblia unamaanisha kwamba Mashahidi hukataa matibabu yoyote au kwamba hawathamini afya na uhai? Sivyo kamwe!—Ona sanduku “Maoni ya Mashahidi wa Yehova Kuhusu Afya.”

Katika miaka ya karibuni, madaktari wengi wametambua kwamba Mashahidi wamenufaika kitiba kwa sababu ya kushikamana na viwango vya Biblia. Kwa mfano, hivi karibuni daktari wa upasuaji wa mfumo wa neva aliunga mkono waziwazi matibabu yasiyohusisha kutiwa damu. Alisema: “Matibabu ya badala ndiyo matibabu salama zaidi, si kwa Mashahidi wa Yehova tu, bali pia kwa watu wengine wote.”

Si rahisi kufanya maamuzi mazito ya kitiba, nayo yanaweza kumfadhaisha mtu sana. Kuhusu zoea la kawaida la kuwatia watu damu, ona yale ambayo Dakt. Dave Williams, mtaalamu wa mfumo wa kupumua ambaye pia ni msimamizi wa matibabu alisema: “Ni muhimu tuheshimu maoni ya watu, . . . na tunapaswa kuwa waangalifu sana kuhusu vitu tunavyoingiza mwilini mwetu.” Maneno hayo ni ya kweli—hasa leo.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 11]

Visafirisha-Oksijeni Vinavyotokana na Hemoglobini

Ndani ya kila chembe nyekundu ya damu, kuna molekuli milioni 300 hivi za hemoglobini. Hemoglobini hufanyiza thuluthi moja hivi ya chembe nyekundu iliyokomaa. Kila molekuli ina protini inayoitwa globini na rangi inayoitwa hemu, ambayo ina atomu moja ya chuma. Chembe nyekundu ya damu inapopita kwenye mapafu, molekuli za oksijeni hupenya ndani ya chembe hiyo na kujishikanisha na molekuli za hemoglobini. Muda mfupi baadaye, oksijeni huingizwa kwenye tishu za mwili, na hivyo kuendeleza uhai wa chembe za tishu hizo.

Leo watu fulani husafisha hemoglobini. Kwanza hemoglobini hukusanywa kutoka kwenye chembe nyekundu za damu ya watu au ng’ombe. Kisha hemoglobini huchujwa ili kuondoa uchafu, husafishwa na kufanyiwa mabadiliko kwa kutumia kemikali, na hatimaye huchanganywa na umajimaji fulani na kuhifadhiwa. Mchanganyiko huo, ambao matumizi yake bado hayajaidhinishwa katika nchi nyingi, ndio unaoitwa Visafirisha-Oksijeni Vinavyotokana na Hemoglobini (HBOC). Kwa kuwa hemu ndiyo hufanya damu iwe nyekundu, painti ya Visafirisha-Oksijeni hivyo hufanana na painti ya chembe nyekundu za damu, ambayo ndiyo sehemu kuu ya damu inayotumiwa kutengeneza mchanganyiko huo.

Chembe nyekundu za damu zinahitaji kuhifadhiwa kwenye friji na inabidi kuzitupa baada ya majuma machache, lakini Visafirisha-Oksijeni hivyo havihitaji kuhifadhiwa kwa njia hiyo, navyo vinaweza kutumiwa miezi kadhaa baadaye. Kwa kuwa utando wa chembe na antijeni zimeondolewa, hakuna uwezekano wa kupata athari mbaya ambazo hutokea mgonjwa anapotiwa damu isiyopatana na damu yake. Hata hivyo, inapolinganishwa na visehemu vingine vya damu, Visafirisha-Oksijeni hivyo huwatatanisha sana Wakristo wanaofuata dhamiri zao na kujitahidi kutii sheria ya Mungu kuhusu damu. Kwa nini? Visafirisha-Oksijeni hivyo hutengenezwa kutokana na damu na hilo linatokeza vipingamizi viwili. Kwanza, Visafirisha-Oksijeni hivyo hufanya kazi muhimu ya mojawapo ya sehemu kuu za damu. Pili, hemoglobini, ambayo HBOC imetolewa kwake, hufanyiza asilimia kubwa ya sehemu hiyo kuu ya damu. Wakristo wanakabili uamuzi mzito sana wanapozingatia matumizi ya Visafirisha-Oksijeni Vinavyotokana na Hemoglobini (HBOC) na ya bidhaa nyingine za damu. Ni lazima wasali na kutafakari kwa makini kanuni za Biblia kuhusu utakatifu wa damu. Kila mmoja, akitamani sana kudumisha uhusiano mzuri na Yehova, anapaswa kutegemea dhamiri yake inayoongozwa na Biblia.—Wagalatia 6:5.

[Picha]

MOLEKULI YA HEMOGLOBINI

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 12]

Mbinu ya Matibabu Inayovutia

“Idadi ya hospitali zinazotumia mbinu ya badala, yaani, kufanya upasuaji ‘bila kutumia damu,’ imezidi kuongezeka,” laripoti The Wall Street Journal. “Mbinu hiyo ambayo ilianza kutumiwa hasa kwa ajili ya Mashahidi wa Yehova,” linasema jarida hilo, “sasa inakubaliwa na watu wengi, nazo hospitali nyingi zinawajulisha watu kwamba zinafanya upasuaji bila kutumia damu.” Hospitali nyingi ulimwenguni pote zimetambua kwamba kutumia mbinu zinazopunguza uhitaji wa kutumia damu huleta manufaa nyingi, hasa kwa mgonjwa. Kwa sasa, maelfu ya madaktari huwatibu wagonjwa bila kutumia damu.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 12]

Maoni ya Mashahidi wa Yehova Kuhusu Afya

Mashahidi wa Yehova, ambao baadhi yao ni madaktari na wauguzi, wanajulikana kotekote ulimwenguni kwa kukataa kutiwa damu nzima au sehemu kuu za damu. Je, msimamo wao wakiwa kikundi unategemea itikadi au maoni ya watu kwamba imani ya mtu inaweza kumponya? Si kweli hata kidogo!

Kwa kuwa wanathamini sana zawadi ya uhai waliyopewa na Mungu, Mashahidi hujitahidi sana kuishi kulingana na Biblia, kwani wanaamini kuwa ‘imeongozwa na roho ya Mungu.’ (2 Timotheo 3:16, 17; Ufunuo 4:11) Biblia inawahimiza Wakristo waepuke mazoea na tabia zinazohatarisha afya na uhai kama vile ulafi, kuvuta au kutafuna tumbaku, matumizi mabaya ya pombe, na kutumia dawa kwa matumizi yasiyo ya kitiba.—Methali 23:20; 2 Wakorintho 7:1.

Wanapodumisha usafi wa mwili na wa mazingira, na wanapofanya mazoezi ili wawe na afya nzuri, wao huwa wakifuata kanuni za Biblia. (Mathayo 7:12; 1 Timotheo 4:8) Mashahidi wa Yehova wanapokuwa wagonjwa, wao huonyesha usawaziko kwa kukubali matibabu mengi yanayopatikana leo. (Wafilipi 4:5) Wao hutii amri ya Biblia ya “kujiepusha na . . . damu” huku wakisisitiza wapewe matibabu ya badala. (Matendo 15:29) Uchaguzi huo unawawezesha kupata matibabu bora zaidi.