Vitwitwi Ndege Wanaotangatanga Kote Ulimwenguni
Vitwitwi Ndege Wanaotangatanga Kote Ulimwenguni
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA
HEBU wazia ukikaa miezi miwili wakati wa kiangazi kwenye maeneo ya Aktiki, ambako jua halitui kamwe. Hata hivyo, majira ya baridi kali yanapokaribia unaelekea Amerika Kusini, Australia, au Afrika Kusini. Unasafiri mwaka mzima ukitafuta chakula unachopenda zaidi katika fuo za kila bara. Vitwitwi wengi ulimwenguni huishi maisha kama hayo.
Vitwitwi ni ndege wanaopenda kulisha mahali penye maji yasiyo na kina kirefu. * Katika miezi yenye baridi zaidi katika maeneo ya Kaskazini, ndege hao hukusanyika kwenye milango ya mito iliyo na matope, fuo, maeneo ya upwa tope, au fuko zenye miamba. Hayo ni maeneo yasiyotembelewa na wanadamu kwa ukawaida. Katika miezi yenye joto zaidi, wakati ambapo watalii hujazana kwenye fuo, vitwitwi wengi huhamia maeneo ya Aktiki na maeneo yaliyo karibu. Kipindi hicho kifupi cha joto huwawezesha kupata utulivu na chakula cha kutosha wanachohitaji ili kuwatunza makinda yao.
Vitwitwi hawana rangi zenye kuvutia sana, lakini njia yao ya kuruka na alama za mabawa yao huwavutia watu wengi. “[Vitwitwi] wanaweza kuruka huku ncha za mabawa yao zikigusa maji au waruke kilometa sita au zaidi juu ya usawa wa bahari. Wao ni warukaji stadi,” kinasema kitabu Shorebirds—Beautiful Beachcombers.
Wanakuwa Salama Wanapokuwa Wengi
Kwa kawaida vitwitwi hukusanyika kwa wingi mahali palipo na chakula kingi. Inaonekana kwamba wao hujikusanya mahali pamoja ili wawe salama. Ndege wawindaji kama vile kozi-kipanga hupenda kuwawinda ndege walio peke yao, lakini huenda wakasita kushambulia kikundi cha ndege. Isitoshe, ndege wanapojikusanya mahali pamoja, inakuwa rahisi kumwona mwindaji kabla hajashambulia. Ili wafaidike na ulinzi huo wa ziada, vitwitwi wa jamii mbalimbali hukusanyika pamoja.
Inavutia sana kutazama vitwitwi wanaporuka. Mamia au hata maelfu ya ndege wanaoruka karibukaribu wanaweza kujipinda-pinda, kupaa juu na chini, kana kwamba wanaongozwa na mkono fulani usioonekana. Kitabu Handbook of the Birds of the World kinasema: “Ni muujiza kwamba maelfu ya ndege wanaoruka kwa kasi wakiwa pamoja wanaweza kujipinda-pinda kwa upatano mkubwa sana.” Baada ya kuchunguza filamu za
kikundi cha ndege wengi aina ya dunlin, wataalamu wa ndege wamefikia mkataa wa kwamba ndege mmoja anaweza kuanzisha mbinu ya kujipinda nao ndege wote wamwige mara moja.Wanaweza Kusafiri Ulimwenguni Pote
Baadhi ya vitwitwi husafiri ulimwenguni pote. Kwa mfano, vitwitwi wanaoitwa red knot na sanderling husafiri hadi maeneo ya mbali zaidi ya kaskazini kuliko ndege mwingine yeyote ili kuzalisha. Vitwitwi wanaweza kutua kwenye ufuko wowote ulimwenguni na kila mwaka wanaweza kusafiri umbali wa kilometa 32,000 hivi.
Ingawa ndege hao wanapohama inawabidi kuvuka bahari, hawawezi kuogelea wala kupumzika juu ya maji. Kwa hiyo, lazima wabebe kiasi kikubwa cha nishati, kinachozidi kile ambacho ndege kubwa sana za abiria hubeba. Wakati ndege hizo za abiria zinapopaa, asilimia 40 hivi ya uzani wake ni mafuta. Vitwitwi hupataje nishati hiyo yote?
David Attenborough anasema hivi katika kitabu chake The Life of Birds: “Wao huhifadhi [nishati hiyo] ikiwa mafuta nao hula sana kwenye upwa tope wa pwani hivi kwamba katika majuma machache uzani wao huongezeka maradufu. Mafuta hayo huwa mengi kuliko inavyokadiriwa, kwani ukubwa wa viungo vingi vya ndani, kutia ndani ubongo na matumbo hupungua ili kuwe na nafasi ya kuhifadhi mafuta na kupunguza uzani.”
Kiluwiluwi-dhahabu wa pasifiki, hufunga safari ndefu sana kutoka Alaska hadi Visiwa vya Hawaii. Licha ya jitihada zinazohitajiwa ili kusafiri umbali wa kilometa 4,500, inastaajabisha zaidi kufikiria jinsi ambavyo ndege huyo huweza kutambua mahali ambapo Hawaii ipo katikati ya bahari. Kiluwiluwi-dhahabu mmoja aliyechunguzwa alipokuwa akisafiri, alitumia karibu siku nne kusafiri umbali huo. Na ndege mmoja mzee alikuwa amefunga safari hiyo zaidi ya mara 20!
Mwishowe, wanapoanza kufika kwenye maeneo yao ya kuzalisha huko Aktiki, ndege hao wanaosafiri
sana huwa na shughuli nyingi. Katika majuma mawili lazima watafute mwenzi, watafute eneo lao, na kujenga kiota. Kisha wana majuma matatu hivi ya kulalia mayai na majuma mengine matatu ya kutunza makinda yao. Kufikia mwisho wa Julai, wao huanza kuelekea kusini tena.Hatari za Kusafiri
Vitwitwi hukabili hatari nyingi wanapofunga safari zao ndefu. Hatari moja kubwa ni wanadamu. Katika karne ya 19, mtaalamu wa mambo ya asili, John James Audubon, aliripoti kwamba katika siku moja viluwiluwi-dhahabu wa Amerika wapatao 48,000 walipigwa risasi na wawindaji. Leo, idadi ya jamii hiyo ya ndege ulimwenguni imeongezeka, lakini bado ni wachache kuliko wale waliouawa siku hiyo.
Tisho kubwa pia kwa vitwitwi ni kukauka kwa maeneo yenye majimaji. Vitwitwi hukabili hali ngumu sana maeneo hayo yanapokauka. Kitabu Shorebirds—An Identification Guide to the Waders of the World kinaeleza hivi: “Mazoea ya kuzalisha, kuhama na maeneo ambayo vitwitwi huhamia wakati wa majira ya baridi kali, yamesitawi katika muda wa maelfu ya miaka na ni rahisi sana kwa mwanadamu kuyabadili au kuyaharibu.” Ili mamilioni ya vitwitwi waendelee kuwa hai, lazima maeneo yao muhimu ya kuhamia yahifadhiwe.
Mojawapo ya maeneo hayo ni Ghuba ya Delaware kwenye pwani ya kusini-magharibi ya New Jersey, huko Marekani. Katika eneo hilo karibu viluwiluwi mia moja elfu wanaoitwa red knot hukusanyika wakati wa majira ya kuchipua ili kula mayai ya kaa wanaoitwa horseshoe. Ndege hao huwa na njaa kali kwa kuwa wamemaliza “mojawapo ya safari ndefu zaidi ambazo ndege hufunga bila kutua.” Katika majuma mawili wameruka kilometa 8,000 kutoka kusini-mashariki ya Brazili hadi eneo hilo. Baada ya safari yao wao huwa wamepoteza nusu ya uzani wao.
Huenda jitihada za wahifadhi wa mazingira zikasaidia kuhakikisha kwamba maeneo kama hayo ambayo vitwitwi hupenda kuhamia hayataharibiwa. Huenda kukawa na eneo kama hilo karibu na mahali unapoishi. Ukiwatazama vitwitwi wakiruka kwa kujipinda-pinda juu ya mawimbi au ukisikiliza vilio vyao, ni vigumu kuwasahau.
Arthur Morris, mtaalamu wa mambo ya asili, anaandika: “Watu wote ambao hupenda kuwatazama vitwitwi hupata hisia zilezile: kila mmoja wetu amesimama mara nyingi kwenye ufuo au upwa tope usiokuwa na watu na kutazama kikundi cha chamchanga wenye rangi mbalimbali wakijipinda-pinda na kugeuka-geuka wanaporuka kwa upatano. Na kila tunapotazama mbwembwe zao, sisi hushangaa na kustaajabu sana.”
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 4 Wanasayansi huwapanga vitwitwi katika kikundi kinachoitwa Charadrii nao husema kuna zaidi ya jamii 200.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]
Ndege Stadi wa Kufunga Safari Ndefu
Huenda Red knot ndio wanaofunga safari ndefu zaidi. Kwa kawaida wale ambao huzalisha kaskazini ya mbali huko Kanada huhamia Ulaya Magharibi au ukingo wa Amerika ya Kusini (zaidi ya umbali wa kilometa 10,000) katika majira ya baridi kali
[Hisani]
KK Hui
Vikundi vya dunlin milioni moja hivi wameonekana huko uholanzi na Mauretania
Bar-tailed godwit hutoka katika maeneo yao ya kuzalisha huko Siberia na kusafiri hadi Visiwa vya Uingereza, Afrika Kusini, Mashariki ya Kati, Australia, au New Zealand
Sanderling wanaweza kupatikana wakikimbia katika karibu fuo zote ulimwenguni. Wengine huzalisha katika maeneo yaliyo kilometa 950 hivi karibu na Ncha ya Kaskazini ya dunia
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Lazima vitwitwi wahifadhi mafuta mengi sana ili wavuke bahari kubwa kwa kuwa hawawezi kutua majini
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Sanderling husafiri wakiwa wengi kwa sababu za usalama
[Picha katika ukurasa wa 17]
Kizamiachaza
[Picha katika ukurasa wa 17]
Kiguuhina mwenye madoa akitafuta chakula kwenye vinamasi
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]
Top and bottom panoramic photos: © Richard Crossley/VIREO