Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
▪ “Bahari ndiyo makao yaliyo na viumbe wengi zaidi duniani. Pia ndiyo makao hatari zaidi . . . Lakini popote tunapotazama kuna viumbe wengi sana.”—NEW SCIENTIST, UINGEREZA.
▪ Hivi karibuni, kwenye kesi fulani ya majaribio, mahakama ya Harrisburg, Pennsylvania, Marekani, iliamua kwamba “ni kinyume cha sheria kufundisha [kwamba vitu vilibuniwa na mtu mwenye akili] badala ya kufundisha mageuzi wakati wa somo la sayansi katika shule za umma.”—NEW YORK TIMES, MAREKANI.
▪ Kulingana na uchunguzi uliofanywa mnamo 2005, “asilimia 51 ya Wamarekani wanapinga nadharia ya mageuzi.”—NEW YORK TIMES, MAREKANI.
▪ Mnamo Juni 2006, Harriet, kobe mkubwa wa Galápagos mwenye kilo 150, alikufa katika hifadhi ya wanyama huko Brisbane, Australia. Akiwa na umri wa miaka 175, Harriet alikuwa “mnyama mzee zaidi ulimwenguni.”—SHIRIKA LA UTANGAZAJI LA AUSTRALIA.
▪ Watafiti wa Uswisi wamegundua jinsi aina mbalimbali za mahindi hujilinda dhidi ya minyoo wanaoshambulia mizizi yao. Mahindi hutoa harufu fulani mchangani. Harufu hiyo huvutia minyoo wanaoitwa minuscule ambao huua viwavi wa minyoo wanaokula mizizi hiyo.—DIE WELT, UJERUMANI.
Ngisi Mkubwa Apigwa Picha
Kwa mara ya kwanza wanasayansi wamempiga picha ngisi mkubwa aliye hai karibu na Visiwa vya Bonin, kusini mwa Japani. Waliweka ngisi wadogo na visehemu vya uduvi kwenye ndoana kisha wakaning’iniza kamera juu ya vyambo hivyo. Inasemekana kuwa ngisi mkubwa aliyetokea meta 900 chini ya maji, alikuwa na urefu wa meta 8.
“Dinosa Walikula Nyasi”
Shirika la Habari la Associated Press linaripoti kuwa “ni jambo linalowashangaza wanasayansi wengi” kugundua kwamba “dinosa walikula nyasi.” Wanasayansi Waligundua hilo walipochunguza kinyesi cha dinosa kilichopatikana huko India. Kwa nini wanasayansi walishangazwa? Ripoti hiyo inasema ilifikiriwa kwamba “nyasi hazikuwako hadi muda mrefu baada ya dinosa kufa na kutoweka.” Pia iliaminiwa kwamba dinosa “hawakuwa na meno ya pekee ya kutafunia nyasi.” Mtaalamu wa mabaki ya kale ya mimea, Caroline Stromberg, aliyeongoza wanasayansi waliofanya ugunduzi huo anasema: “Watu wengi hawangewazia kwamba [dinosa] wanaweza kula nyasi.”
Nyuki Hurukaje?
Mainjinia wamesema kwa mzaha kwamba nyuki hawawezi kuruka. Yaelekea kwamba wadudu “wazito” kama hao wenye mipigo ya mabawa iliyo mifupi hawawezi kutokeza nguvu za kutosha kuwainua. Ili kugundua jinsi wadudu hao wanavyoruka, mainjinia “waliwapiga picha kwa kutumia kamera inayopiga picha 6000 kwa sekunde,” lasema gazeti New Scientist. Mbinu ya nyuki imefafanuliwa kuwa “isiyo ya kawaida.” Bawa la nyuki hujipinda kwa pembe-mraba linapoenda mbele, kisha hugeuka linaporudi, nalo hufanya hivyo mara 230 kwa sekunde. . . . Ni kama propela, ambayo sahani yake pia inazunguka,” akaeleza mmoja wa mainjinia hao. Ugunduzi wao unaweza kuwasaidia mainjinia kubuni upya propela na kuunda ndege zinazoweza kuendeshwa kwa urahisi zaidi.
Panya Wanaoimba
Gazeti New Scientist linaripoti hivi: “Panya wanaweza kuimba, na . . . nyimbo wanazowaimbia wenzi wao watarajiwa ni tata kama zile za ndege.” Panya huimba kwa sauti ya juu sana hivi kwamba sikio la mwanadamu haliwezi kusikia, na huenda hiyo ndiyo sababu iliyofanya isigunduliwe kwamba panya huimba. Watafiti huko St. Louis, Missouri, Marekani, waligundua kwamba sauti za panya wa kiume “zilipangwa kulingana na mfuatano wa sauti, na hivyo kuwa kama ‘wimbo.’” Kwa sababu hiyo panya wamo katika kikundi cha pekee. Wanyama wengine wanaojulikana kuwa wana uwezo wa kuimba ni nyangumi, aina fulani ya popo, pomboo, na bila shaka wanadamu.