Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kwa Nini Tunaamini Kuna Muumba?

Kwa Nini Tunaamini Kuna Muumba?

Kwa Nini Tunaamini Kuna Muumba?

Wataalamu wengi katika nyanja mbalimbali za sayansi wanatambua vitu vilibuniwa kwa akili. Wanaona si jambo linalopatana na akili kuamini kwamba uhai ulio tata sana ulijitokeza wenyewe tu. Hivyo, wanasayansi na watafiti kadhaa wanaamini kuna Muumba.

Baadhi yao wamekuwa Mashahidi wa Yehova. Wanasadiki kuwa Mungu wa Biblia ndiye Mbuni na Mjenzi wa ulimwengu. Kwa nini wamekata kauli hiyo? Mwandishi wa Amkeni! aliwahoji baadhi yao. Huenda ukapendezwa na majibu waliyotoa. *

“Utata Usio na Kifani wa Uhai”

WOLF-EKKEHARD LÖNNIG

MAELEZO YAKE: Kwa miaka 28 iliyopita, nimefanya kazi ya sayansi inayohusu mabadiliko ya chembe za urithi za mimea. Nimeajiriwa na Taasisi ya Utafiti wa Kuzalisha Mimea ya Max Planck huko Cologne, Ujerumani, kwa miaka 21 kati ya miaka hiyo 28. Nimekuwa mzee wa kutaniko la Kikristo la Mashahidi wa Yehova kwa miaka 30 hivi.

Utafiti wangu unaotegemea majaribio na uchunguzi wa chembe za urithi na uchunguzi wangu wa mambo kama vile utendaji na maumbo ya vitu hai, umeniwezesha kutambua utata usio na kifani wa uhai. Kujifunza mambo hayo kumeimarisha usadikisho wangu kwamba uhai umetokana na chanzo chenye akili.

Wanasayansi wanafahamu vizuri utata wa uhai. Lakini mambo ya hakika kuhusu uhai hufafanuliwa kwa njia inayounga mkono mageuzi. Hata hivyo, kwa maoni yangu, sababu zinazotolewa ili kupinga masimulizi ya Biblia kuhusu uumbaji huvunjwa-vunjwa zinapochunguzwa kisayansi. Nimechunguza sababu hizo kwa makumi ya miaka. Nimechunguza kwa makini vitu vilivyo hai na pia jinsi sheria za asili zinavyoendesha ulimwengu wote, nami sina budi kuamini kuna Muumba.

“Kila Jambo Ambalo Nimechunguza Lina Kisababishi”

BYRON LEON MEADOWS

MAELEZO YAKE: Ninaishi Marekani na ninafanya kazi katika idara ya fizikia ya miale ya leza ya shirika la NASA. Kwa sasa ninahusika katika mradi wa kiteknolojia wa kuboresha uwezo wa kuchunguza hali ya hewa ya dunia na matukio katika sayari mbalimbali. Mimi ni mzee wa kutaniko la Mashahidi wa Yehova mjini Kilmarnock, Virginia.

Mara nyingi kazi yangu inahusu sheria za fizikia. Mimi hutafuta visababishi vya mambo fulani na jinsi yanavyotukia. Ninapofanya uchunguzi, ninapata uthibitisho ulio wazi kwamba kila jambo lina kisababishi. Ninaamini kwamba ni jambo linalopatana na sayansi kuamini kuwa Mungu ndiye aliyetokeza vitu vyote. Sheria za asili ni imara sana hivi kwamba sina budi kuamini kuwa ziliwekwa na Msimamizi, yaani, Muumba.

Ikiwa ni rahisi kukata kauli hiyo, mbona wanasayansi wengi wanaamini mageuzi? Je, huenda ni kwa sababu wanamageuzi hufanya uchunguzi wao huku wakishikilia kauli zao? Hilo si jambo geni miongoni mwa wanasayansi. Lakini si lazima uchunguzi wowote, hata uwe wenye kusadikisha jinsi gani, utokeze matokeo sahihi. Kwa mfano, mtu anayefanya utafiti wa fizikia ya leza anaweza kusisitiza kwamba nuru ni mawimbi, kama vile sauti ilivyo mawimbi, kwa kuwa kwa kawaida nuru hutenda kama mawimbi. Lakini, kauli yake si sahihi kwani uthibitisho pia unaonyesha nuru hutenda kama kikundi cha chembe zinazoitwa fotoni. Hali kadhalika, wale wanaosisitiza kwamba mageuzi ni jambo hakika hawakati kauli kwa msingi wa uthibitisho wote uliopo, na maoni yao kuhusu uthibitisho unaotolewa hutegemea kauli wanazoshikilia.

Nashindwa kuelewa jinsi mtu anavyoweza kuamini kwamba nadharia ya mageuzi ni jambo hakika ilhali “wataalamu” wa mageuzi hawaafikiani kuhusu jinsi yalivyotokea. Kwa mfano, je, ungeamini hesabu kuwa jambo hakika iwapo mtaalamu fulani angekuambia kwamba 2 ukiongeza 2 ni 4, huku wataalamu wengine wakisema kwamba jumla yake inaaminika kuwa 3 au hata 6? Ikiwa wanasayansi wanapaswa kuamini mambo yanayoweza kuthibitishwa, kuchunguzwa, na kurudiwa, basi nadharia ya kwamba vitu vyote hai vilitokea kwa njia ya mageuzi kutokana na chanzo kimoja si jambo hakika la kisayansi.

“Kitu Hakiwezi Kutokea Pasipo Kitu Kingine”

KENNETH LLOYD TANAKA

MAELEZO YAKE: Mimi ni mtaalamu wa jiolojia. Kwa sasa nimeajiriwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Jiolojia ya Marekani, iliyoko jijini Flagstaff, Arizona. Kwa miaka 30 hivi, nimetumia wakati mwingi kufanya utafiti katika nyanja mbalimbali za jiolojia, kutia ndani jiolojia ya sayari mbalimbali. Makala zangu nyingi za utafiti na ramani za Mars za jiolojia zimechapishwa katika majarida ya kisayansi yanayoheshimiwa. Nikiwa Shahidi wa Yehova, mimi hutumia saa 70 hivi kila mwezi kuwafundisha watu Biblia.

Nilifundishwa kuamini mageuzi, lakini singeweza kusadiki kwamba nguvu nyingi iliyohitajiwa ili kutokeza ulimwengu ilijitokeza yenyewe tu pasipo Muumba mwenye nguvu. Kitu hakiwezi kutokea pasipo kitu kingine. Isitoshe nimepata katika Biblia, uthibitisho mzuri kwamba kuna Muumba. Kitabu hicho kina mifano chungu nzima ya mambo hakika ya sayansi yanayohusiana na taaluma yangu. Mfano mmoja ni fundisho lake kwamba dunia ni duara nayo imetundikwa “pasipo na kitu.” (Ayubu 26:7; Isaya 40:22) Mambo hayo ya hakika yaliandikwa katika Biblia muda mrefu kabla wanadamu hawajafaulu kuyachunguza na kuyathibitisha.

Fikiria jinsi tulivyoumbwa. Sisi tunaweza kujitambua, kuwaza, kuwasiliana, na tuna hisia mbalimbali. Isitoshe, tunaweza kuhisi tunapendwa, kufurahi kwa sababu tunapendwa, na kuwapenda wengine. Nadharia ya mageuzi haiwezi kueleza jinsi wanadamu walivyopata sifa hizo.

Jiulize, ‘Vyanzo vya habari inayotumiwa kuunga mkono mageuzi ni sahihi na vyenye kutegemeka kadiri gani?’ Habari za kijiolojia si kamili, ni tata, na zenye kukanganya. Wanamageuzi wameshindwa kuthibitisha nadharia zao kuhusu mageuzi kwa kufanya majaribio wakitumia mbinu za kisayansi. Na ingawa wanasayansi hutumia mbinu nzuri kufanya utafiti, mara nyingi wao huongozwa na maoni yao ya ubinafsi wanapofafanua matokeo ya utafiti wao. Inajulikana kwamba wanasayansi hupigia debe maoni yao wakati matokeo ya utafiti yanapopingana au yanapokosa kutoa uthibitisho wa kutosha. Kazi na tamaa yao ya kuheshimiwa ndiyo huwachochea.

Nikiwa mwanasayansi na mwanafunzi wa Biblia mimi hutafuta kweli kamili, inayopatana na mambo yote ya hakika yajulikanayo na inayopatana pia na matokeo ya utafiti, ili niweze kukata kauli iliyo sahihi zaidi. Ninasadiki kwamba ni jambo linalopatana kabisa na akili kuamini kuna Muumba.

“Uthibitisho wa Kwamba Chembe Ilibuniwa”

PAULA KINCHELOE

MAELEZO YAKE: Kwa miaka kadhaa nimekuwa nikifanya utafiti wa chembe, biolojia ya molekuli, na mikrobiolojia. Kwa sasa nimeajiriwa na Chuo Kikuu cha Emory, Atlanta, Georgia, Marekani. Pia mimi hujitolea kufundisha Biblia katika eneo fulani la Warusi.

Kwa miaka minne ya masomo yangu ya biolojia, nilifanya tu utafiti wa chembe na sehemu zake mbalimbali. Kadiri nilivyojifunza kuhusu DNA, RNA, protini, na njia za kuyeyusha chakula, ndivyo nilivyostaajabia utata, utaratibu, na usahihi katika chembe. Na ingawa nilivutiwa na yale ambayo mwanadamu amefaulu kujifunza kuhusu chembe, nilishangazwa hata zaidi kutambua bado kuna mengi sana tusiyoyajua. Ninaamini kuna Mungu kwa sababu kuna uthibitisho kwamba chembe ilibuniwa.

Kwa kujifunza Biblia nimemfahamu Muumba huyo, yaani, Yehova Mungu. Nasadiki kwamba yeye si Mbuni mwenye akili tu, bali pia Baba mwenye upendo na anayenijali. Biblia inafafanua kusudi la uhai na kutoa taraja la maisha yenye furaha ya wakati ujao.

Huenda vijana wanaofundishwa mageuzi shuleni wasijue wataamini nini. Wanaweza kuchanganyikiwa sana wakiwa shuleni. Iwapo wanaamini kuna Mungu, imani yao hujaribiwa wanapofundishwa mageuzi. Lakini wanaweza kushinda jaribu hilo kwa kuchunguza vitu vingi vya asili vinavyotuzunguka na kwa kuendelea kupata ujuzi juu ya Mungu na sifa zake. Mimi binafsi nimefanya hivyo na nimekata kauli kwamba masimulizi ya Biblia kuhusu uumbaji ni sahihi na hayapingani na mambo hakika ya sayansi.

“Sheria Zenye Utaratibu Zilizo Rahisi Sana”

ENRIQUE HERNÁNDEZ-LEMUS

MAELEZO YAKE: Mimi ni mhubiri wa wakati wote wa Mashahidi wa Yehova. Pia mimi ni mtaalamu wa fizikia ya nadharia katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Mexico. Kwa sasa ninafanya utafiti kuhusu ufafanuzi unaofaa wa jinsi joto linavyohusika katika utendaji wa uvutano wa athari ya joto ambao husababisha kupanuka kwa nyota. Pia nimewahi kuchunguza utata wa mifuatano ya DNA.

Uhai ni tata sana hivi kwamba haungeweza kujitokeza wenyewe. Kwa mfano, fikiria habari chungu nzima iliyo katika molekuli ya DNA. Uwezekano wa kromosomu moja tu kujitokeza ni mdogo kuliko 1 ikigawanywa mara trilioni 9. Uwezekano huo ni mdogo sana hivi kwamba jambo hilo halingewezekana. Nafikiri ni upuuzi kuamini kwamba nguvu fulani isiyo na utu ingeweza kuumba si kromosomu moja tu, bali pia vitu vyote hai vilivyo tata sana na vyenye kustaajabisha.

Isitoshe, nichunguzapo utendaji wa vitu, kuanzia vitu vidogo visivyoonekana kwa macho hadi mawingu makubwa angani, ninavutiwa na sheria zenye utaratibu zilizo rahisi sana zinazoviongoza. Uhakika huo unanionyesha kwamba aliyeviumba si Mwanahisabati Stadi tu, bali pia ni Msanii Stadi.

Mara nyingi watu hushangaa ninapowaambia kwamba mimi ni Shahidi wa Yehova. Nyakati nyingine wao huniuliza ninawezaje kuamini kuna Mungu. Ninaelewa kinachowafanya waulize hivyo, kwani dini nyingi haziwahimizi waumini wao watafute uthibitisho wa mambo wanayofundishwa au wafanye utafiti kuhusu imani zao. Hata hivyo, Biblia inatuhimiza tutumie “uwezo wa kufikiri.” (Methali 3:21) Uhakika kwamba vitu vya asili vimebuniwa kwa akili, kutia ndani uthibitisho unaotolewa na Biblia, umenisadikisha kwamba kuna Mungu anayesikiliza sala zetu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Maoni ya wataalamu katika makala hii huenda yasipatane na maoni ya waajiri wao.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 22]

Mars in background: Courtesy USGS Astrogeology Research Program, http://astrogeology.usgs.gov