Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maumbo Yanayovutia ya Mimea

Maumbo Yanayovutia ya Mimea

Maumbo Yanayovutia ya Mimea

JE, UMEGUNDUA kwamba mimea mingi hukua kwa umbo la mzunguko? Kwa mfano, mananasi yanaweza kuwa na safu 8 za magamba zikielekea upande mmoja huku safu nyingine 5 au 13 zikielekea upande tofauti. (Ona picha ya 1.) Ukitazama mbegu za alizeti unaweza kuona safu 55, 89, au zaidi zinazokua kwa mzunguko. Huenda pia ukaona safu kama hizo kwenye koliflawa. Baada ya kugundua kwamba mimea ina safu hizo, huenda ukavutiwa zaidi na matunda na mboga unapoenda sokoni. Kwa nini mimea huwa na maumbo hayo? Je, idadi ya safu hizo ina umuhimu wowote?

Mimea Inakuaje?

Mimea mingi hufanyiza viungo vipya kama vile shina, majani, na maua kutoka kwenye meristemu, ambayo ni sehemu ya mmea iliyo na uwezo wa kujigawanya na kutokeza sehemu mpya. Kila sehemu mpya inayofanyizwa hutokea na kukua kuelekea upande tofauti ikifanyiza pembenukta. * (Ona picha ya 2.) Katika mimea mingi, sehemu mpya hufanyiza pembenukta na hivyo kutokeza safu. Pembenukta hiyo ina ukubwa gani?

Fikiria tatizo hili: Wazia unabuni ua kwa njia ambayo sehemu zake mpya zitakazotokezwa karibu-karibu kuzunguka kiini cha ukuzi bila kuacha nafasi yoyote kati ya safu. Vipi ukitaka kutokeza sehemu mpya za mmea kwa mzunguko ulio pembenukta yenye ukubwa wa sehemu mbili juu ya tano. Utakabili tatizo kila mara sehemu mpya ya tano inapotokezwa mahali hapohapo na kukua kuelekea upande uleule. Sehemu hizo zingefanyiza safu huku kukiwa na nafasi kubwa kati ya safu hizo. (Ona picha ya 3.) Ukweli ni kwamba, tofauti yoyote ndogo katika ukubwa wa pembenukta ya kila mzunguko hutokeza safu huku kukiwa na nafasi kubwa kati ya safu. “Pembenukta bora” iliyo digrii 137.5 hivi ndiyo inayotokeza safu zinazokaribiana zaidi. (Ona picha ya 5.) Ni nini kinachofanya pembenukta hiyo iwe ya pekee sana?

Pembenukta hiyo bora inafaa kwa sababu haiwezi kusababisha badiliko katika sehemu ndogo ya mzunguko. Pembenukta yenye ukubwa wa 5/8 wa mzunguko inaikaribia sana hiyo pembenukta bora, 8/13 inaikaribia hata zaidi, nayo 13/21 inaikaribia kwa ukaribu zaidi. Hata hivyo, hakuna pembenukta nyingine inayoweza kutokeza mzunguko wa safu unaofaa kabisa. Hivyo, sehemu mpya ya mmea inapotokezwa ikiwa kwenye pembenukta ya digrii 137.5 hivi kutoka kwa sehemu iliyoitangulia, hakuna sehemu mbili za mmea zitakazokua kuelekea upande uleule mmoja. (Ona picha ya 4.) Hivyo, badala ya kutokeza umbo lililo sawa na miale ya nuru kutoka chanzo kimoja, sehemu hizo mpya za mmea hufanyiza safu zinazozungukana.

Kwa kushangaza, picha za kompyuta za sehemu za mimea zinazokua kutoka katika kiini kimoja, zinaweza kuonyesha safu hizo za mzunguko ikiwa tu ukubwa wa pembenukta kati ya kila sehemu mpya ni sahihi kabisa. Ukubwa wa pembenukta ukitofautiana hata kwa asilimia kumi na pembenukta bora, safu hazitapangika ifaavyo.—Ona picha ya 5.

Ua Lina Petali Ngapi?

Inapendeza kwamba kwa kawaida idadi ya safu zinazotokana na pembenukta yenye ukubwa wa digrii 137.5 ni idadi inayopatana na mfumo wa nambari unaoitwa Fibonacci. Mfumo huo ulifafanuliwa kwanza katika karne ya 13 na mwanahisabati Mwitaliano aliyeitwa Leonardo Fibonacci. Katika mfumo huo, baada ya nambari 1 kila nambari inayofuata inalingana na jumla ya nambari mbili zinazoitangulia.—1, 1, 2, 3, 5, 8, 13, 21, 34, 55, na kuendelea.

Maua ya mimea mingi inayofanyiza safu huwa na idadi ya petali inayopatana na mfumo wa nambari wa Fibonacci. Kulingana na wataalamu fulani, kombetindi huwa na petali 5, bloodroots petali 8, fireweeds petali 13, asta petali 21, aina fulani ya daisy petali 34, na Michaelmas daisy petali 55 au 89. (Ona picha ya 6.) Mara nyingi, matunda na mboga huwa na umbo linalopatana na mfumo wa nambari wa Fibonacci. Kwa mfano, ndizi huwa na sehemu-mkato yenye pande tano.

“Amefanya Kila Kitu Kiwe Chenye Kupendeza”

Kwa muda mrefu wasanii wamejua kwamba kiwango bora ndicho kinachotuvutia zaidi. Ni nini kinachofanya sehemu mpya ya mimea ikue kwa usahihi katika pembenukta bora? Watu wengi wanakata kauli kwamba huo ni uthibitisho mwingine kwamba vitu hai vilibuniwa na mtu mwenye akili.

Kutafakari jinsi ambavyo vitu hai vilibuniwa na jinsi vinavyofurahisha watu, kumewafanya wengi waamini kwamba kuna Muumba anayetaka tufurahie maisha. Biblia inasema hivi kumhusu Muumba wetu: “Amefanya kila kitu kiwe chenye kupendeza kwa wakati wake.”—Mhubiri 3:11.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Inashangaza kwamba, alizeti ni mmea ulio tofauti kwani maua yake madogo ambayo hubadilika na kuwa mbegu, huanza kufanyiza safu kuanzia sehemu ya nje ya ua la alizeti badala ya sehemu yake ya katikati.

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Picha ya 1

(See publication)

Picha ya 2

(See publication)

Picha ya 3

(See publication)

Picha ya 4

(See publication)

Picha ya 5

(See publication)

Picha ya 6

(See publication)

[Picha katika ukurasa wa 24]

Picha ya meristemu

[Hisani]

R. Rutishauser, University of Zurich, Switzerland

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

White flower: Thomas G. Barnes @ USDA-NRCS PLANTS Database