Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Burudani za Umma Katika Karne ya Kwanza

Burudani za Umma Katika Karne ya Kwanza

Burudani za Umma Katika Karne ya Kwanza

Watu wengi sana walijeruhiwa na kuuawa kutia ndani watoto baada ya ghasia kuzuka kati ya mashabiki wa michezo kutoka majiji mawili jirani huko Italia kusini. Kwa sababu ya msiba huo, wenye mamlaka waliamuru kwamba ukumbi huo wa maonyesho ufungwe kwa miaka kumi.

TUNAPOSOMA habari kama hizo kwenye magazeti ya leo hatushangazwi. Lakini tukio hilo lilitendeka karibu miaka 2,000 iliyopita wakati wa utawala wa Maliki Nero. Mwanahistoria Mroma Tasito alieleza kuhusu ghasia hizo zilizofanyika katika ukumbi wa maonyesho wa Pompeii wakati wa mchezo wa kupigana, ambapo Wapompeii walizozana na mashabiki wa jiji jirani la Nuceria.

Katika karne ya kwanza burudani iliwavutia sana watu. Majiji maarufu ya Milki ya Roma yalikuwa na majumba ya maigizo, kumbi za maonyesho, na viwanja vya maonyesho, na majiji fulani yalikuwa na sehemu hizo zote tatu. Kitabu Atlas of the Roman World kinasema: “Michezo hiyo ilihusisha hatari kubwa na msisimko . . . [na] umwagaji wa damu.” Walioendesha magari ya kukokotwa walivalia nguo zenye rangi tofautitofauti na kila timu iliwakilisha kikundi fulani katika jamii, kiwe kilikuwa cha kisiasa au cha kijamii. Mashabiki walilipuka kwa msisimko timu yao ilipotokea. Waendesha magari ya kukokotwa walikuwa maarufu sana hivi kwamba watu walipamba nyumba zao kwa picha za wachezaji hao, nao walilipwa pesa nyingi sana.

Pia majiji yalikuwa na michezo ya kupigana yenye umwagaji mwingi wa damu na mapigano kati ya wanadamu na wanyama, nyakati nyingine wanadamu wakiwa bila silaha. Kulingana na mwanahistoria Will Durant, “wahalifu waliohukumiwa, nyakati nyingine wakiwa wamevikwa ngozi ili wafanane na wanyama, walitupwa katikati ya wanyama walionyimwa chakula ili wawe wakali kwa ajili ya tukio hilo; wahalifu waliokufa chini ya hali hizo walipata maumivu makali sana.”

Kwa kweli, wale waliofurahia burudani kama hiyo isiyo ya kimungu walikuwa “katika giza kiakili” na walikuwa ‘wameishiwa na ufahamu wote wa maadili.’ (Waefeso 4:17-19) Katika karne ya pili, Tertullian aliandika hivi: “Kati ya [Wakristo] hakuna kitu ambacho husemwa, au kuonwa, au kusikiwa ambacho kinahusiana na kile kichaa cha sarakasi, yale mambo ya aibu katika majumba ya michezo ya kuigiza, [na] ule ukatili wa uwanja wa michezo.” Leo, Wakristo wa kweli vilevile hujitahidi kuepuka burudani zenye jeuri haidhuru ziko katika njia gani, iwe ni kupitia vitabu, televisheni, au michezo ya kompyuta, kwani wanakumbuka kwamba Yehova anamchukia “mtu yeyote anayependa jeuri.”—Zaburi 11:5.

[Picha katika ukurasa wa 30]

Picha ya mwendesha gari la kukokotwa baada ya ushindi

[Picha katika ukurasa wa 30]

Mchoro wa mwanamume akipigana na simba-jike

[Picha katika ukurasa wa 30]

Jumba la maigizo la Kiroma la karne ya kwanza

[Hisani]

Ciudad de Mérida

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 30]

Top and bottom left: Museo Nacional de Arte Romano, Mérida