Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Jaribio Takatifu” la Dini ya Quaker

“Jaribio Takatifu” la Dini ya Quaker

“Jaribio Takatifu” la Dini ya Quaker

MNAMO Julai (Mwezi wa 7) 1656, meli inayoitwa Swallow, kutoka Barbados huko West Indies ilitia nanga kwenye bandari ya Boston, Massachusetts, ambayo leo ni sehemu ya Marekani. Richard Bellingham, aliyekuwa makamu wa gavana wa koloni ya Massachusetts, aliamuru kwamba abiria Mary Fisher na Ann Austin wafungiwe ndani ya meli hiyo. Kati ya vitu vyao kulipatikana vitabu 100 ambavyo vilisemekana kuwa vyenye “mafundisho yaliyofisidika, ya uzushi, na yenye kukufuru.”

Vitabu hivyo vilichomwa sokoni. Kisha wanawake hao walifungwa, wakavuliwa nguo zote, na kuchunguzwa iwapo walikuwa na alama za kichawi. Dirisha la gereza lao lilifunikwa, na kwa majuma matano wanawake hao waliachwa gizani. Mtu yeyote ambaye angethubutu kuzungumza nao angepigwa faini ya pauni tano. Mwishowe, Mary Fisher na Ann Austin wakarudishwa Barbados.

Mwandishi mmoja wa wakati huo aliwauliza mahakimu hivi: “Kwa nini kuja kwa wanawake wawili kuliwatetemesha hivyo, ni kana kwamba jeshi linalotisha lilikuwa limevamia mipaka yenu”? Wanawake hao “hatari” walikuwa wamishonari wa kwanza wa dini ya Quaker (au Watetemekaji) kufika Amerika Kaskazini. Quaker ilikuwa dini ya aina gani, na kwa nini walionwa kuwa tisho?

Jamii ya Marafiki

Dini ya Quaker, au Dini ya Jamii ya Marafiki, iliibuka kule Uingereza katika karne ya 17. Mwanzilishi wa dini hiyo ni George Fox (1624-1691), aliyezaliwa huko Leicestershire, akiwa mwana wa mfumaji. Baada ya kudai kwamba alikuwa amesikia sauti ya kimuujiza, Fox alikata kauli angeweza kuzungumza moja kwa moja na Mungu na kupokea ufunuo bila kupitia mtu mwingine. Kitabu A Religious History of the American People kinasema: “Inadaiwa kuwa Dini ya Jamii ya Marafiki ilianzishwa mnamo 1652.”

Dini ya Quaker ilipataje jina hilo? Chanzo kimoja cha marejeo kinasema kwamba “walitetemeka kabla ya kupata ufunuo wa kimungu.” Chanzo kingine kinasema kwamba “walitetemeka kwa sababu ya utakatifu na utukufu wa Mungu.” Lengo la dini ya Quaker lilikuwa kupata ukweli wa kidini na kufufua Ukristo wa kale.

Walidai kwamba wanapata mwongozo kutoka kwa roho takatifu, manabii wa Biblia, mitume wa Kristo, na “nuru,” au “sauti,” ya walichodai kuwa ukweli wa kiroho. Kwa hiyo, walipokutana walikaa kimya huku kila mmoja akitafuta mwongozo wa Mungu. Mtu yeyote aliyepata ujumbe wa kimungu angezungumza. *

Wafuasi wa Quaker waliamini katika haki, uaminifu usiobadilika, maisha rahisi, na yasiyo na jeuri. Pia waliamini kwamba Wakristo wote, kutia ndani wanawake, wanapaswa kushiriki katika kuhubiri. Kwa sababu ya imani yao wafuasi wa Quaker walisababisha hofu na kuanza kushukiwa kwa kuwa walikataa mpangilio uliopo ndani ya dini, walijitenga na fahari na sherehe, na walidai kuongozwa na sauti fulani ndani yao na si makasisi. Bidii yao ya umishonari iliwaogopesha watu hata zaidi ikachochea hasira, wazusha ghasia, na kuingiliwa na wenye mamlaka.

Huko Uingereza, wafuasi wa Quaker walinyanyaswa na kufungwa, na kule New England walifukuzwa na hata kuuawa. Kwa mfano, kati ya 1659 na 1661, wamishonari Mary Dyer, William Leddra, William Robinson, na Marmaduke Stephenson walinyongwa kule Boston. Wengine walitiwa pingu, wakawekwa alama kwa chuma chenye moto, au kupigwa. Wengine walikatwa masikio. Mtu mmoja aliyeitwa William Brend alipigwa mijeledi 117 mgongoni kwa kamba iliyokuwa imetiwa lami. Licha ya ukatili huo wafuasi wa Quaker waliongezeka.

William Penn na “Jaribio Takatifu”

Kuanzia 1681, maisha ya wafuasi wa Quaker huko Amerika Kaskazini yalibadilika. Kwa sababu ya kile kinachoitwa “jaribio takatifu” la kusimamisha serikali, William Penn (1644-1718), kijana Mwingereza aliyekuwa amejiunga na Jamii ya Marafiki, alianzisha koloni iliyotegemea kanuni na usimamizi wa dini ya Quaker. Ingawa alikuwa mwana wa ofisa mkuu wa jeshi la wanamaji la Uingereza, Penn alikuwa amefungwa gerezani kwa sababu ya kuhubiri na kuandika kuhusu maoni yake.

Ili kulipa deni la baba yake Penn, Mfalme wa Uingereza alimpa Penn sehemu kubwa ya ardhi huko Amerika Kaskazini. Hati ya kifalme ilimpa William Penn mamlaka kamili juu ya koloni hilo jipya, lililoitwa Pennsylvania, jina linalomaanisha “Msitu wa Penn,” kwa kumkumbuka baba yake. Huko, watu wa dini zote walipaswa kuwa na uhuru wa ibada.

Kwanza Penn alimtuma Marekani binamu yake William Markham akajaribu kuwafanya watu waliotoka Ulaya ambao wangekuwa majirani wa koloni lake jipya wawe washikamanifu kwake na kununua mashamba kutoka kwa Wenyeji wa Asili wa Amerika. Mnamo 1682, Penn aliona koloni lake kwa mara ya kwanza baada ya kusafiri kwenye Mto Delaware. Alifanya mkataba wa haki na Wenyeji wa Asili wa Amerika huko Shackamaxon (sasa panaitwa Kensington, sehemu ya Philadelphia). Kisha, kilometa moja hivi kutoka Shackamaxon, alianzisha makazi mapya, ambayo aliyaita Philadelphia, kumaanisha “Upendo wa Kindugu.” Watu waliongezeka haraka.

Penn alirudi Uingereza na kutangaza kuhusu koloni hilo jipya na kuwatia moyo watu wahamie huko. Aliandika kuhusu mashamba na misitu mizuri, mto wenye kuvutia, wanyama wa mwituni, na ngozi. Aliahidi kwamba serikali hiyo mpya ingeendeleza uhuru wa kidini na ushirikiano wa amani. Watu wote walikaribishwa, wafanyabiashara, maskini, na watu waliokuwa na upendezi na maoni ambayo yangechangia kuwa na serikali nzuri.

Wakiwa na matumaini kwamba wangepata kitulizo kutokana na matatizo ya kijamii na kisiasa yaliyokuwa huko Ulaya, wafuasi wengi wa Quaker walihama kutoka Uingereza na Ireland Kaskazini. Wafuasi wa Menno na vikundi vingine walihama kutoka eneo la Mto Rhine huko Ulaya. Wengi wa wakazi wa kwanza walikuwa wafuasi wa Quaker naye Penn alisema kwamba koloni hiyo ingekuwa na wakati ujao mzuri. Mnamo 1683, aliandika hivi: “Tayari kumekuwa na vikao viwili vya bunge, . . . na karibu sheria 70 zimepitishwa bila kuwa na mabishano yoyote.” Hata hivyo, hisia hiyo ya kutarajia mambo mazuri haikudumu.

Jaribio Lagonga Mwamba

Katiba ya koloni la Penn iliruhusu kila mtu kuwa na uhuru wa kujiamulia mambo. Hivyo, ilipokuwa lazima kutumia nguvu ili kudumisha utengamano wa kijamii, mtazamo wa wafuasi wa Quaker wa kuepuka jeuri ulitokeza tatizo ambalo lilizidi kuwa baya kadiri muda ulivyopita. Mwanzoni Penn alijaribu kuhepa tatizo hilo kwa kuweka askari ambao hawakuwa wafuasi wa Quaker ili, kama alivyosema, “kuwaadhibu wanadamu wenzetu ilipohitajika.” Mnamo 1689 uwezekano wa vita dhidi ya Ufaransa uliongeza mizozano kati ya wafuasi wa Quaker.

Kuongezea matatizo hayo, watu wengi sana waliohamia, ambao wengi wao hawakuwa wafuasi wa Quaker, walinyakua mashamba kutoka kwa Wenyeji wa Asili wa Amerika. Hivyo, kadiri watu ambao hawakuwa wafuasi wa Quaker walivyozidi kuwa wengi kuliko wao, uhusiano wao na Wenyeji wa Asili wa Amerika ukazidi kuwa wenye uhasama.

Pigo la mwisho kwa mamlaka ya kisiasa ya wafuasi wa Quaker lilikuja mnamo 1756 wakati gavana na baraza lake walitangaza vita dhidi ya makabila ya Delaware na Shawnee. Wafuasi wa Quaker walijiondoa katika serikali na huo ukawa mwisho wa mfumo huo wa utawala. Hivyo, miaka 75 baada ya kuanzishwa, “jaribio takatifu” la Penn la kutawala likaisha.

Vilevile, baada ya muda, bidii ya kidini ya wafuasi wa Quaker ilianza kupungua kadiri walivyotajirika. Samuel Fothergill ambaye ni mfuasi wa Quaker alisema hivi: “Kwa kuwa mtazamo na mapendezi yao yaliekelezwa kwenye mambo ya ulimwengu huu, [wakazi waliokuwa wafuasi wa dini ya Quaker] hawangeweza kuelimisha watoto wao kuhusu kanuni ambazo wao wenyewe walikuwa wamesahau.” Baada ya muda, madhehebu yakatokea.

Huenda Penn na wafuasi wake walikuwa na malengo na mafanikio ya muda, lakini hawakuelewa au walipuuza mafundisho ya Yesu kwamba yeye na wanafunzi wake “si sehemu ya ulimwengu.” (Yohana 17:16) Hivyo, haidhuru watu wawe na nia nzuri kadiri gani, wakianzisha mradi ambao unachanganya dini na siasa za ulimwengu wanafanya hivyo bila baraka za Mungu au Mwana wake. (Yakobo 4:4; 1 Yohana 5:19) Kwa hiyo, mradi kama huo hauwezi kufaulu.—Zaburi 127:1.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 8 Siku hizi, makanisa mengi ya Quaker yana mhudumu anayelipwa kuongoza ibada kwa utaratibu zaidi.

[Sanduku katika ukurasa wa 12]

“UFALME WANGU SI SEHEMU YA ULIMWENGU HUU”

Kwa nini Yesu alisema maneno hayo yaliyo kwenye Yohana 18:36? Tunaweza kupata jibu tunapoelewa Ufalme wa Mungu ni nini. Ufalme wa Mungu, ambao ulikuwa kichwa kikuu cha mafundisho ya Yesu, ni serikali ya ulimwengu iliyo mikononi mwa Yesu Kristo. (Isaya 9:6, 7; Luka 4:43) Badala ya kutumia serikali za wanadamu, Ufalme huo utaziondolea mbali na kuwa serikali pekee duniani. (Danieli 2:44; 7:13, 14) Hilo ndilo Yesu alitaja katika sala ya mfano aliposema: “Ufalme wako na uje. Mapenzi yako na yatendeke duniani kama ilivyo mbinguni.” (Mathayo 6:9, 10) Raia waaminifu wa Ufalme huo watafurahia maisha mazuri ambayo watu wanyoofu, kama William Penn, hawangeweza kutokeza. Watafurahia afya kamilifu na maisha yasiyo na mwisho katika mazingira yenye amani, ya kiparadiso.—Luka 23:43; Ufunuo 21:3, 4.

[Picha katika ukurasa wa 10]

Mkutano wa wafuasi wa Quaker huko Philadelphia, miaka ya 1800

[Picha katika ukurasa wa 10]

Mfuasi wa Quaker Mary Dyer akipelekwa kunyongwa katika Koloni ya Massachusetts Bay

[Picha katika ukurasa wa 11]

Wafuasi wa Quaker wakiondoka Uingereza, miaka ya 1600

[Picha katika ukurasa wa 11]

William Penn akifanya mapatano na Wenyeji wa Asili wa Amerika, mnamo 1682

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 10]

Both pictures: © North Wind Picture Archives

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 11]

Boats: © North Wind Picture Archives; treaty: Brown Brothers