Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kila siku ulimwenguni pote majaribio milioni 5.7 hufanywa ili kuwadanganya watumiaji wa Intaneti.—MAGAZINE, HISPANIA.

“Mnamo 2005, kwa mwaka wa nane mfululizo, idadi ya watu wanaojiua nchini Japani ilizidi 30,000.” Japani ni mojawapo ya nchi yenye idadi kubwa zaidi ulimwenguni ya watu wanaojiua.—MAINICHI DAILY NEWS, JAPANI.

“Katika miaka 500 iliyopita, utendaji wa wanadamu umesababisha aina 844 za wanyama kutoweka (au kutoweka msituni).”—IUCN, SHIRIKA LA ULIMWENGU LA KUHIFADHI MAZINGIRA, USWISI.

Kulingana na tarakimu zilizotolewa na serikali, asilimia 6 ya Waingereza, wa kiume na kike, hufanya ngono pamoja na watu wa jinsia yao. Sheria iliyopitishwa mnamo 2005 “inawaruhusu wenzi wa jinsia moja ‘kuoana’ na inawapa haki zinazolingana” na zile za wenzi wa ndoa wa jinsia tofauti.—THE DAILY TELEGRAPH, UINGEREZA.

Miamba ya Barafu Yazidi Kuporomoka

Gazeti Science linaripoti kwamba “mwendo wa miamba kadhaa mikubwa ya barafu huko Greenland unaongezeka.” Picha za setilaiti zinadokeza kwamba katika miaka mitano iliyopita, mwendo wa miamba fulani ya barafu huko Greenland umeongezeka mara mbili, kufikia mwendo wa zaidi ya kilometa 12 kwa mwaka. Katika miaka kumi iliyopita, kiwango cha barafu kilichoyeyuka kiliongezeka kila mwaka kwa kiasi kinacholingana na sanduku la barafu lenye urefu wa kilometa 90, upana wa kilometa 90, na kina cha kilometa 90. Hivyo, wanasayansi wanadokeza kwamba “kiwango cha maji baharini kitaongezeka kuliko inavyokadiriwa.”

Makanisa Yasherehekea Sikukuu ya Darwin

Mnamo Februari (Mwezi wa 2) 2006, karibu makanisa 450 yanayodai kuwa ya Kikristo nchini Marekani yalisherehekea mwaka wa 197 tangu kuzaliwa kwa Charles Darwin. Sherehe hiyo ilihusisha “programu na mahubiri yaliyokusudiwa kukazia kwamba nadharia ya mageuzi inapatana na imani yao ya Kikristo na kwamba Wakristo hawahitaji kuchagua kati ya dini na sayansi.” Kulingana na gazeti la Chicago Tribune, Michael Zimmerman, ambaye ni mwanabiolojia na msimamizi wa Chuo cha Fasihi na Sayansi katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Oshkosh, ambaye alipanga sherehe hizo, alisema: “Huhitaji kuchagua. Unaweza kuamini yote mawili.”

Kukosa Adabu Kazini

Gazeti The Wall Street Journal linasema, “kukosa adabu kazini kunaweza kugharimu wakati, jitihada, na uwezo wa shirika lolote lile.” Uchunguzi uliofanywa kwa watu 3,000 ulionyesha kwamba zaidi ya asilimia 90 kati yao “wamewahi kukosewa adabu kazini.” Nusu ya watu hao walisema kwamba “walipoteza wakati wa kufanya kazi kwa sababu ya kuhangaikia tukio hilo,” “asilimia 25 kati yao wakapunguza jitihada zao kazini,” na 1 kati ya 8 akaacha kazi. Kulingana na Christine Porath, profesa wa usimamizi katika Chuo Kikuu cha California Kusini, “kukosa kufanya kazi kwa bidii, kukosa kuja kazini, na hata wizi kunaweza kuwa ishara za kwamba shirika lina watu wasiokuwa na adabu,” linasema gazeti hilo.

Rundo la Takataka Baharini

Mapema mnamo 2006, rundo kubwa sana la takataka “lilisukumwa kusini kuelekea Hawaii, likimwaga vifaa vingi sana vya uvuvi vilivyoachwa na takataka za plastiki kwenye fuo za Kisiwa,” linaripoti The Honolulu Advertiser. Mikondo husukuma takataka nyingi zinazoelea katika Bahari ya Pasifiki Kaskazini kuelekea sehemu tulivu ya bahari, lakini kunapokuwa na aina fulani ya halihewa, takataka hizo husukumwa kuelekea Hawaii. Mnamo 2005 “zaidi ya vipande 2,000 vya takataka vilipatikana,” kutia ndani zaidi ya nyavu 100. Takataka hizo ni hatari kwa viumbe vya baharini. Charles Moore, mwanzilishi wa Shirika la Algalita la Utafiti wa Bahari alisema hivi: “Hakuna samaki wa kiasili waliosalia baharini. Wote wanakula vipande vya plastiki.”