Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Magari Moshi Madogo” Yanayong’aa Gizani

“Magari Moshi Madogo” Yanayong’aa Gizani

“Magari Moshi Madogo” Yanayong’aa Gizani

▪ Katika jioni yenye utulivu huko Brazili mashambani, “gari moshi” dogo linatokea chini ya rundo la takataka msituni. “Taa” mbili za mbele zinaangaza kijia, nazo jozi 11 za taa, zinazotoa mwangaza wa manjano na kijani, zinaangaza kandokando ya kijia hicho. Bila shaka, hilo si gari moshi la kawaida. Badala yake, ni buu la mbawakawa wa jamii ya Phengodidae, anayepatikana Amerika ya Kaskazini na ya Latini. Kwa kuwa mbawakawa wa kike hudumisha umbo la buu, nao hufanana na magari moshi madogo yanayong’aa kwa ndani, nyakati nyingine wao hurejelewa kuwa minyoo wa reli. Wabrazili wanaoishi mashambani huwaita magari moshi madogo.

Mchana, ni vigumu kumwona mbawakawa huyo mwenye rangi ya kahawia. Lakini usiku anaonekana kwa urahisi kwa kuwa anatoa mwangaza wenye rangi mbalimbali za ajabu. Mwangaza huo hutendeshwa na kemikali inayoitwa luciferin ambayo kwa msaada wa kimeng’enya kinachoitwa luciferase huungana na oksijeni kutokeza mwangaza. Mwangaza huo unaweza kuwa mwekundu, wa rangi ya machungwa, manjano, au kijani.

Taa nyekundu za mbele huwaka karibu wakati wote, lakini zile za kando zenye rangi ya manjano na kijani haziwaki nyakati zote. Utafiti umedokeza kwamba taa za mbele husaidia kuwapata jongoo, ambao huliwa sana na mbawakawa, nazo taa za kando huwazuia viumbe wanaowawinda mbawakawa kama vile chungu, vyura, na buibui. Ni kana kwamba mwangaza huo unapitisha ujumbe huu: “Sifai kwa chakula. Nenda zako!” Hivyo, taa hizo za kando hung’aa zaidi mbawakawa anapohisi kuna mwindaji karibu. Pia, hung’aa mbawakawa anapomshambulia jongoo na mbawakawa wa kike anapolalia mayai yake. Kwa kawaida mwangaza wake huendelea kuongezeka hadi unapofikia upeo kisha unazima halafu unawaka tena. Yote hayo huchukua sekunde chache tu.

Naam, hata katika marundo ya takataka msituni, mtu anaweza kustaajabia umaridadi unaotukumbusha maneno haya ya mtunga-zaburi ya kumsifu Muumba: “Dunia imejaa vitu ulivyotokeza.”—Zaburi 104:24.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Robert F. Sisson / National Geographic Image Collection