Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Staajabia Mto Mkubwa Mekong

Staajabia Mto Mkubwa Mekong

Staajabia Mto Mkubwa Mekong

MTO MEKONG hutiririka kupitia nchi sita za Asia, ukitegemeza watu milioni 100 kutoka jamii mia moja za wenyeji. Kila mwaka tani milioni 1.3 hivi za samaki huvuliwa katika mto huo, na hiyo ni mara nne ya kiasi cha samaki wanaovuliwa katika Bahari ya Kaskazini! Ukiwa na urefu wa kilometa 4,350, mto huo ndio mrefu zaidi Kusini-Mashariki mwa Asia. Na kwa sababu mto huo unapita katika nchi kadhaa, una majina mengi, lakini jina lake maarufu ni Mekong, ambalo ni ufupisho wa jina la Kithai Mae Nam Khong.

Mto Mekong huanzia juu katika milima ya Himalaya, ambako mto huo hutiririka kwa kishindo kuelekea chini kupitia mabonde yenye kina. Kufikia wakati maji yake hutoka nchini China, ambako mto huo huitwa Lancang, maji hayo huwa yamekamilisha karibu nusu ya safari yake na huwa yameshuka meta 4,500 kuelekea usawa wa bahari. Nusu ya pili hushuka kwa meta 500 tu na kufikia usawa wa bahari. Kwa sababu hiyo maji katika sehemu hiyo ya mto husonga polepole. Unapotoka China mto huo ndio mpaka kati ya Myanmar na Laos, nao hufanyiza sehemu kubwa ya mpaka kati ya Laos na Thailand. Unapofika Kambodia mto huo hugawanyika na kuingia Vietnam ukiwa mito miwili ambayo hutawanyika na kuingia katika Bahari ya Kusini ya China.

Mwishoni mwa miaka ya 1860 Wafaransa walijaribu kupata njia ya kuingia China kupitia Mto Mekong. Hata hivyo walikatishwa tamaa walipokaribia maporomoko karibu na mji wa Kratie, nchini Kambodia na mfululizo wa maporomoko madogo yanayoitwa Khone, kusini mwa Laos. Maji mengi sana hupitia kwenye hayo Maporomoko ya Khone kuliko maporomoko mengine ulimwenguni, kwani maji hayo huwa mara mbili zaidi ya yale yanayomwagika kwenye Maporomoko ya Niagara yaliyo pande zote mbili za mpaka wa Kanada na Marekani.

Mto Wenye Manufaa Makubwa

Mto Mekong ni muhimu kwa uchumi wa nchi zilizo Kusini-Mashariki mwa Asia. Vientiane, mji mkuu wa Laos, na Phnom Penh, mji mkuu wa Kambodia, ni majiji ya bandarini ya mto huo. Mto huo ni muhimu sana kwa maisha ya watu wa Vietnam. Nchini humo mto huo hugawanyika na kuwa mifereji saba na kufanyiza delta ya kilometa 40,000 za mraba, ambazo zikiunganishwa zinakuwa na urefu wa kilometa 3,200. Mto huo humwagilia mashamba kutia ndani yale ya mpunga nao huzirutubisha kwa mchanga-tope ambao ni muhimu sana kwa mashamba hayo hivi kwamba wakulima hupanda mpunga mara tatu kwa mwaka. Kwa kweli baada ya Thailand, Vietnam ndiyo nchi ya pili kwa uuzaji wa mchele duniani.

Inakadiriwa kwamba kuna aina 1,200 za samaki katika Mto Mekong, na nyingine kati ya hizo, kutia ndani uduvi, hufugwa kwa ajili ya kuuzwa. Samaki anayeitwa trey riel, ni maarufu kwa jambo fulani la pekee. Jina la pesa za Kambodia riel, linatokana na samaki huyo. Mto Mekong pia una aina fulani ya kambare ambao wako hatarini na wanaokua kufikia meta 2.75. Mnamo 2005, wavuvi walimvua kambare aliye na kilo 290, ambaye huenda ndiye samaki mkubwa zaidi kupatikana katika maji safi popote ulimwenguni! Samaki mwingine ambaye yuko hatarini katika mto huo ni pomboo anayeitwa Irrawaddy. Watafiti wanasema kwamba huenda ikawa pomboo hao wanapungua 100 katika mto huo.

Zaidi ya kuwalisha mamilioni ya watu, Mto Mekong ni njia kuu ya usafiri wa meli za aina zote. Mashua ndogo husafirisha watu, mashua kubwa husafirisha mizigo, na meli kubwa huingia na kutoka kuelekea bahari kuu. Mto huo hupendwa na watalii, kwani wengi wao hupenda kusafiri mbele zaidi ya Maporomoko ya Khone ili kutembelea mji wa Vientiane. Mji huo ni maarufu kwa sababu ya mifereji, minara inayoitwa pagoda, na nyumba zake zilizojengwa juu ya milingoti, nao umekuwa na shughuli nyingi za kibiashara, kisiasa, na kidini kwa zaidi ya miaka 1,000. Kutoka Vientiane mtu anaweza kusafiri kuelekea upande wa juu wa mto hadi mji wa Louangphrabang. Wakati mmoja jiji hilo la bandarini lilikuwa mji mkuu wa milki kubwa ya Thai-Lao na kwa wakati fulani, kutia ndani kipindi cha utawala wa Wafaransa, lilikuwa mji mkuu wa kifalme wa Laos. Bado unaweza kuona mambo fulani ya ukoloni wa Wafaransa katika jiji hilo la kihistoria.

Katika nyakati za karibuni kumekuwa na mabadiliko yenye kutia wasiwasi kwenye Mto Mekong. Mabadiliko hayo yanatia ndani mbinu za uvuvi zenye kuharibu, ukataji wa miti, na ujenzi wa mabwawa makubwa ya kutokeza umeme. Kwa watu wengi hali hiyo inaonekana kuwa yenye kukatisha tamaa. Lakini kuna tumaini.

Biblia inaahidi kwamba hivi karibuni Muumba wetu mwenye upendo ataingilia mambo ya wanadamu kupitia Ufalme wake. (Danieli 2:44; 7:13, 14; Mathayo 6:10) Chini ya mwongozo wa serikali hiyo kamilifu ya ulimwengu, dunia yote itarudishwa iwe na hali nzuri, na kwa njia ya kitamathali mito ‘itapiga makofi’ kwa shangwe. (Zaburi 98:7-9) Mto Mekong na ujiunge katika kushangilia huko.

[Ramani katika ukurasa wa 24]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

CHINA

MYANMAR

LAOS

THAILAND

KAMBODIA

VIETNAM

Mto Mekong

[Picha katika ukurasa wa 24]

Mashamba ya mpunga kwenye Delta ya Mto Mekong

[Picha katika ukurasa wa 24]

Aina 1,200 hivi za samaki huishi kwenye Mto Mekong

[Picha katika ukurasa wa 25]

Soko linaloelea, Vietnam

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]

Rice paddies: ©Jordi Camí/age fotostock; fishing: ©Stuart Pearce/World Pictures/age fotostock; background: © Chris Sattlberger/Panos Pictures

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

Market: ©Lorne Resnick/age fotostock; woman: ©Stuart Pearce/World Pictures/age fotostock