“Imetokana na Wazazi Safi Zaidi”
“Imetokana na Wazazi Safi Zaidi”
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BRAZILI
CHUMVI imefafanuliwa kuwa “imetokana na wazazi safi zaidi, yaani, jua na bahari.” Hilo ni kweli hasa kuhusu chumvi inayotokezwa jua linapovukiza maji ya bahari.
Jimbo la Rio Grande do Norte lililo kwenye ufuo wa kaskazini-mashariki mwa Brazili, ni maarufu kwa kutokeza chumvi. Hali ya hewa yenye joto, kiwango cha chini cha mvua, na pepo kavu za kawaida hufanya eneo hilo lifae kutokeza chumvi kwa kuvukiza maji yenye chumvi. Asilimia 95 ya chumvi ya Brazili ambayo haijasafishwa na iliyosafishwa hutokezwa huko. Manispaa ya Areia Branca, ambalo ni jiji dogo la pwani, ni sehemu moja ambako chumvi hutokezwa.
Kutembelea Eneo Linalotokeza Chumvi
Kwa kawaida sehemu ambako chumvi hutokezwa ni kubwa sana, kwa hiyo eneo la kutokeza chumvi huko Areia Branca ni kubwa pia. Kawaida wageni wanapokaribia jiji la Areia Branca, wao hushangazwa na ukubwa wa eneo hilo la kutokeza chumvi. Jua la asubuhi hupiga maji yaliyotengwa na kuyafanya yaonekane kuwa hayana mwisho. Karibu asilimia 90 ya eneo hilo lililotengwa hutumiwa kuvukizia, na eneo linalobaki hutumiwa kufanyiza chembechembe.
Kuna chumvi kila mahali kana kwamba kumefunikwa kwa mablanketi meupe ambayo hung’aa yanapopigwa na jua. Lazima mtu avae miwani ya jua anapotembelea eneo hilo. Chumvi hukusanywa kwa mara ya kwanza maji ya bahari yanaporuhusiwa kuingia kupitia mabwawa yasiyo na kina kirefu yaliyogawanywa kwa kuta na malango ya mbao. Kuna mabwawa 67 kama hayo. Kila sekunde, jua na pepo za eneo hilo lenye joto huvukiza lita 650 hivi za maji! Hata hivyo, inachukua siku 90 hadi 100 hivi kukamilisha uvukizaji wote.
Ingawa sodiamu-kloridi hubaki baada ya kuvukizwa, maji ya baharini yana kiasi kidogo cha kalisi-kaboneti, kalisi-salfeti, magnesi-salfeti, na madini mengine. Mengi kati ya madini hayo hujitenga kabla ya sodiamu-kloridi na hivyo madini hayo huachwa maji ya chumvi yanapohamishwa kutoka kidimbwi kimoja hadi kingine.
Kutoka kwenye mabwawa hayo, maji yaliyojaa chumvi huruhusiwa kuingia katika mabwawa 20 ya kutokeza chembechembe. Katika mabwawa fulani ni kana kwamba maji ya chumvi yameondolewa kabisa na kuacha bonge la chumvi. Mashine kubwa ya kukusanya chumvi inatumiwa kukata chumvi na kuipakia kwenye malori. Malori hayo hubeba chumvi na kuipeleka kwenye kitu kilicho kama lifti, ambako chumvi hiyo huoshwa. Maji hayo yanapoondolewa chumvi husafishwa kwa maji safi.
Mwishowe, chumvi hupelekwa kwa mashua kwenye kisiwa kilichotengezwa na wanadamu cha bandarini huko Areia Branca, kilichojengwa kilometa 12 ndani ya bahari. Kisiwa hicho kina umbo la mstatili wenye upana wa meta 92 kwa urefu wa meta 166 na kinaweza kustahimili uzito wa tani 100,000 za chumvi. Mkanda wa kusafirisha vitu hupeleka chumvi hadi kwenye eneo lingine ambako chumvi hiyo hupakiwa juu ya meli na kusafirishwa hadi sehemu nyingine za Brazili.
Chumvi Ni Muhimu
Ingawa miili yetu inahitaji kiasi kidogo tu, chumvi ni muhimu kwa uhai na afya ya watu na wanyama. Huenda tukafikiria chumvi kuwa ungaunga mweupe unaotumiwa tu kuongeza ladha ya chakula. Hata hivyo, chumvi hutumiwa katika njia nyingine muhimu kama vile, katika viwanda vya kemikali, nguo, na ufuaji wa vyuma. Pia, chumvi hutumiwa kutengeneza kemikali kadhaa na hutumiwa kutengeneza sabuni, vioo, na rangi inayotumiwa kuzuia kutu. Inasemekana kwamba leo, chumvi inaweza kutumiwa katika njia mbalimbali zaidi ya 14,000!
Chumvi haiwezi kwisha kamwe. Kwa kila kilo 100 za maji ya baharini, kuna kilo tatu za sodiamu-kloridi, yaani, chumvi ya kawaida! Hata hivyo, zamani haikupatikana kwa urahisi. Kwa mfano, katika China ya kale thamani ya chumvi ilipitwa tu na dhahabu. Biblia inataja chumvi mara nyingi na inaonyesha njia mbalimbali ambazo ilitumiwa.
Nyakati nyingine watoto walipozaliwa walipakwa chumvi, labda kwa sababu watu walifikiria inaweza kutibu au kuua viini. (Ezekieli 16:4) Pia, Biblia hutumia chumvi kwa njia ya mfano. Kwa mfano, Yesu aliwaambia wanafunzi wake kwamba walikuwa “chumvi ya dunia,” akimaanisha uvutano waliokuwa nao juu ya wengine kwa sababu waliwatolea ujumbe wenye kuhifadhi uhai. (Mathayo 5:13) Vilevile, chumvi ilikuwa ishara ya kuwa imara na hali ya kudumu. Kwa hiyo, “agano la chumvi” lilionwa kuwa makubaliano ya kudumu.—Hesabu 18:19.
Kutembelea kwetu sehemu ya Areia Branca kulitusaidia kuelewa zaidi umuhimu wa chumvi na sababu ambazo zimefanya ionwe kwa miaka mingi kuwa kitu chenye thamani. Kwa kweli, tunashukuru sana kwamba bidhaa hiyo, ambayo “imetokana na wazazi safi zaidi, yaani, jua na bahari,” inapatikana kwa wingi sana.
[Picha katika ukurasa wa 16]
Mashine ya kukusanya chumvi katika bwawa la kutokeza chembechembe
[Picha katika ukurasa wa 16]
Chumvi kabla ya kusafishwa
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Eneo la kusafisha, na kuhifadhi chumvi