Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Sayansi Itamaliza Magonjwa?

Je, Sayansi Itamaliza Magonjwa?

Je, Sayansi Itamaliza Magonjwa?

JE, MAENDELEO ya kisayansi yatamaliza magonjwa? Je, unabii wa Biblia kwenye Isaya na Ufunuo unaonyesha kwamba kuna wakati ambapo mwanadamu ataondoa magonjwa yote ulimwenguni? Kwa sababu ya maendeleo mengi katika nyanja ya kitiba watu fulani hufikiri hilo linawezekana.

Serikali na mashirika ya watu binafsi sasa yanaungana pamoja na Umoja wa Mataifa, katika kampeni kubwa ya kukabiliana na magonjwa. Jitihada moja kubwa inafanywa ili kuwapa chanjo watoto katika nchi maskini. Kulingana na Shirika la Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa, ikiwa nchi zitajitahidi kufikia malengo yao, “kufikia mwaka wa 2015, kila mwaka zaidi ya watoto milioni 70 wanaoishi katika nchi maskini zaidi watapewa chanjo ya magonjwa yafuatayo: kifua kikuu, dondakoo, pepopunda, kifaduro, surua, surua ya rubella, homa ya manjano, mafua ya hemofila ya aina ya B, mchochota wa ini aina ya B, polio, rotavirus, pneumococcus, meningococcus, na uvimbe wa ubongo wa Kijapani.” Vilevile, hatua muhimu zimeanza kuchukuliwa ili kutoa mahitaji ya msingi ya kuwa na afya nzuri kama vile kupatikana kwa maji safi, lishe bora, na elimu kuhusu kutunza usafi.

Hata hivyo, wanasayansi wanajitahidi kutoa mengi zaidi ya mambo ya msingi ya kitiba. Teknolojia ya kisasa inabadili kabisa nyanja ya kitiba. Inasemekana kwamba baada ya kila miaka minane hivi, wanasayansi wanaongeza ujuzi maradufu. Ifuatayo ni orodha ya baadhi ya maendeleo ya kiteknolojia ya kisasa na miradi ya kukabiliana na magonjwa.

Eksirei ya kompyuta Kwa zaidi ya miaka 30 madaktari na hospitali zimekuwa zikitumia kifaa kinachoitwa CT scan. Herufi CT katika Kiingereza zinamaanisha eksirei ya kompyuta (computed tomography). CT scanner zinatokeza picha za eksirei za umbo la nje pamoja na viungo vya ndani. Picha hizi zinasaidia kugundua ugonjwa na kuchunguza kasoro za ndani ya mwili.

Ingawa kuna ubishi kuhusu hatari zinazohusiana na madhara ya miale ya eksirei, wataalamu wa kitiba wanatarajia wakati ujao kutakuwa na manufaa ya teknolojia hiyo. Michael Vannier, mtaalamu wa tiba ya miale ya eksirei katika Chuo Kikuu cha Hospitali ya Chicago, anasema: “Katika miaka michache iliyopita kumekuwa na maendeleo mengi sana ya kitiba.”

Vifaa vya kisasa vya CT scanner hufanya kazi haraka zaidi, ni sahihi zaidi, na havina gharama kubwa. Faida moja muhimu ya mbinu mpya za eksirei hizo za kompyuta ni mwendo wake wa kufanya kazi. Jambo hilo linaonekana hasa inapohusu kupiga moyo picha. Kwa kuwa moyo unapiga kwa kuendelea, picha nyingi za eksirei ya kawaida hazingeweza kuuonyesha waziwazi na hivyo ingekuwa vigumu kuzichunguza. Kama gazeti New Scientist linavyoeleza, eksirei mpya za kompyuta hutumia “chini ya sekunde moja kuchunguza mwili mzima, mwendo ambao ni wa haraka zaidi kuliko mpigo mmoja wa moyo,” na hivyo kutokeza picha nzuri sana.

Kwa kutumia eksirei hizo za kisasa, madaktari wanaweza kuona viungo vya ndani waziwazi na vilevile kuchunguza utendaji wa kemikali katika sehemu fulani hususa. Huenda eksirei hizo zikawezesha kugundua kansa ikiwa katika hatua ya mapema.

Upasuaji wa kutumia roboti Siku hizi kuwapo kwa roboti za hali ya juu si ndoto za kisayansi, hasa katika nyanja ya kitiba. Tayari maelfu ya upasuaji hufanywa kwa kutumia roboti. Nyakati nyingine madaktari hufanya upasuaji kwa kuiongoza roboti ambayo ina mikono mingi. Mikono hiyo hubeba visu, mikasi, kamera, dawa ya kuchoma tishu, na vifaa vingine vya upasuaji. Teknolojia hiyo huwawezesha madaktari kufanya upasuaji mgumu sana kwa usahihi wa ajabu. Gazeti Newsweek linaripoti hivi: “Wapasuaji ambao hutumia mbinu hiyo wameona kwamba wagonjwa hawapotezi damu nyingi, hawana maumivu mengi, hupunguziwa hatari zinazohusiana na upasuaji, hawakai hospitalini muda mrefu nao hupona haraka kuliko wale wanaopasuliwa kwa njia ya kawaida.”

Nanomedicine Hiyo ni mbinu ya kitiba inayotumia nanotechnology, ambayo ni sayansi ya kutumia na kutokeza vitu vidogo sana. Kipimo kinachotumiwa katika teknolojia hiyo kinaitwa nanometa, ambayo ni sawa na sehemu moja ya bilioni ya meta. *

Ili kuelewa kipimo hicho, ukurasa huu unaosoma sasa una unene wa nanometa 100,000 hivi nao unywele wa mwanadamu una unene wa nanometa 80,000 hivi. Chembe nyekundu ya damu ina kipenyo cha nanometa 2,500. Bakteria ina urefu wa nanometa 1,000, na kirusi kina urefu wa nanometa 100. DNA yako ina kipenyo cha nanometa 2.5.

Watu wanaotetea teknolojia hii wanaamini kwamba karibuni wanasayansi watabuni vidude vidogo vinavyoweza kutumiwa wakati wa matibabu ndani ya mwili wa mwanadamu. Roboti hizo ndogo zitabeba kompyuta ndogo sana zilizo na maelekezo hususa. Kwa kushangaza, mashine hizo tata zitatengenezwa kwa kutumia vifaa vyenye ukubwa usiozidi nanometa 100. Hiyo ni ndogo mara 25 ukilinganisha na kipenyo cha chembe nyekundu ya damu!

Kwa sababu ni vidogo sana, inatarajiwa kwamba vifaa vya aina hiyo vitaweza kusafiri kwenye mishipa midogo sana na kupeleka oksijeni kwenye tishu zilizopungukiwa na damu, kuondoa vizuizi katika mishipa ya damu na kuondoa ukoga kwenye chembe za ubongo na hata kutafuta na kuharibu virusi, bakteria, na vitu vingine vinavyoambukiza magonjwa. Huenda mashine hizo zikatumiwa pia kupeleka dawa moja kwa moja kwenye chembe zilizokusudiwa.

Wanasayansi wanatabiri kwamba uwezo wa kugundua kansa utaongezeka kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya kutumia nanomedicine. Profesa wa kitiba, Dakt. Samuel Wickline alisema hivi: “Kuna uwezekano mkubwa sana wa kugundua kansa ndogo sana mapema na kuitibu kwa kutumia dawa zenye nguvu mahali palipoathiriwa, na wakati uleule kupunguza madhara ya dawa.”

Ingawa hilo linaweza kuonekana kuwa ndoto tu, wanasayansi fulani huona kwamba jambo hilo linawezekana. Wale wanaoongoza uchunguzi huo wanatarajia kwamba katika miaka kumi ijayo nanotechnology itatumiwa katika kurekebisha na kupanga upya muundo wa molekuli katika chembe za uhai. Mtetezi mmoja wa teknolojia hiyo anadai: “Nanomedicine hatimaye itaondoa magonjwa yote ya karne ya 20, itaondoa maumivu na kuteseka kote kunakotokana na matibabu, na kuwawezesha wanadamu kupanua uwezo wao.” Hata sasa wanasayansi wanapata matokeo mazuri wanapotumia nanomedicine kwa wanyama walio kwenye maabara.

Genomics Taaluma ya muundo wa chembe za urithi inaitwa genomics. Kila chembe katika mwili wa mwanadamu ina vitu vingi sana ambavyo ni muhimu kwa ajili ya uhai. Moja kati ya vitu hivyo ni chembe za urithi. Kila mmoja wetu ana chembe za urithi 35,000 ambazo huamua rangi ya nywele, rangi ya ngozi na macho, kimo, na mambo mengine kuhusu umbo la kila mmoja wetu. Pia chembe zetu za urithi huamua ubora wa viungo vyetu vya ndani.

Chembe za urithi zinapoharibiwa zinaweza kuathiri afya yetu. Kwa kweli, watafiti fulani wanaamini kuwa magonjwa yote husababishwa na kasoro katika chembe za urithi. Sisi hurithi chembe fulani zenye kasoro kutoka kwa wazazi wetu. Chembe nyingine za urithi huharibiwa na vitu vyenye kudhuru katika mazingira.

Wanasayansi wanatumaini kuwa karibuni wataweza kugundua chembe hususa za urithi zinazosababisha tuwe wagonjwa. Hilo litawawezesha madaktari kuelewa kwa nini ni rahisi kwa watu fulani kupata kansa kuliko wengine au kwa nini aina fulani ya kansa ina madhara zaidi kwa watu fulani kuliko wengine. Huenda pia genomics ikafunua kwa nini dawa fulani hufanya kazi inapotumiwa na wagonjwa fulani ilhali inakosa kufanya kazi kwa wengine.

Habari hizo hususa kuhusu chembe za urithi huenda zikatokeza matibabu ya kibinafsi. Unaweza kufaidikaje na teknolojia hiyo? Wazo la matibabu ya kibinafsi linaonyesha kwamba matibabu yatatolewa kuambatana na maelezo kuhusu chembe zako za urithi. Kwa mfano ikiwa uchunguzi wa chembe zako za urithi utaonyesha kwamba una uwezekano wa kupata ugonjwa fulani, madaktari wanaweza kugundua ugonjwa huo muda mrefu sana kabla ya dalili zozote kuonekana. Watetezi wanadai kuwa kabla ugonjwa haujatokea, matibabu yanayofaa, chakula, na kubadili tabia kunaweza hata kuzuia ugonjwa wenyewe.

Pia chembe zako za urithi zitawajulisha madaktari kuhusu uwezekano wa mwili wako kuathiriwa na dawa. Huenda habari hiyo ikawasaidia madaktari kuamua aina inayofaa zaidi ya dawa na kiasi unachohitaji. Gazeti The Boston Globe linaripoti hivi: “Kufikia mwaka wa 2020 huenda [matibabu ya kibinafsi] yakatumiwa kwa kiwango kikubwa kuliko yeyote kati yetu anavyoweza kufikiria leo. Dawa mpya zinazotegemea chembe za urithi zitatokezwa ili kuzuia kisukari, ugonjwa wa moyo, ugonjwa wa Alzheimer, schizophrenia, na magonjwa mengine ambayo hugharimu sana jamii yetu.”

Teknolojia zilizotajwa juu ni kati ya zile ambazo sayansi inatabiri zitakuwapo wakati ujao. Ujuzi wa kitiba unazidi kuongezeka kwa kasi sana. Lakini wanasayansi hawatazamii kuondoa kabisa magonjwa hivi karibuni. Bado kuna vikwazo vingi ambavyo wanahitaji kukabiliana navyo.

Vikwazo Vikubwa

Tabia ya wanadamu inaweza kusababisha magonjwa yasiondolewe haraka. Kwa mfano, wanasayansi wanaamini kwamba kwa sababu ya wanadamu kuharibu mazingira fulani, magonjwa mapya na yaliyo hatari yametokea. Alipohojiwa katika gazeti Newsweek, Mary Pearl, msimamizi wa shirika la Wildlife Trust alieleza hivi: “Tangu miaka ya katikati ya 1970 zaidi ya magonjwa 30 mapya yameibuka, kutia ndani UKIMWI, Ebola, ugonjwa wa Lyme, na Mafua ya Ndege (SARS). Inaaminika kwamba wanadamu waliambukizwa mengi ya magonjwa hayo kutoka kwa wanyama.”

Isitoshe, watu wanakula matunda na mboga kidogo sana huku wakila sukari, chumvi, na mafuta mengi. Pia, magonjwa ya moyo yameongezeka kwa kuwa watu hawafanyi mazoezi wala kazi zinazohusisha nguvu na wanajihusisha katika mazoea mengine yanayodhuru afya. Kuvuta sigara kumeongezeka na kutokeza madhara kwa afya au hata kifo kwa mamilioni ulimwenguni pote. Kila mwaka, watu milioni 20 hivi wamejeruhiwa au kufa katika aksidenti. Vita na aina nyingine za jeuri vinaua na kujeruhi watu wengi. Mamilioni wengine wana afya mbaya kwa sababu ya matumizi mabaya ya kileo au madawa ya kulevya.

Ijapokuwa kuna maendeleo mengi sana katika teknolojia ya kitiba bado magonjwa fulani yanaendelea kusababisha kuteseka kwingi. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), ‘zaidi ya watu milioni 150 wanakumbwa na mshuko wa moyo, watu milioni 25 hivi wanakumbwa na schizophrenia, na wengine milioni 38 wana kifafa.’ Mamilioni ya watu huambukizwa UKIMWI, magonjwa ya kuharisha, malaria, surua, nimonia na kifua kikuu. Magonjwa hayo huua watoto na vijana wengi sana.

Bado kuna vikwazo vingine vikubwa ambavyo vinazuia kuondolewa kabisa kwa magonjwa. Vikwazo viwili vikubwa ni umaskini na utawala mbaya. Katika ripoti ya karibuni shirika la WHO lilisema kwamba mamilioni ambao hufa kwa sababu ya magonjwa ya kuambukiza wangeweza kuokolewa ikiwa serikali zingefanya kazi vizuri na ikiwa kungekuwa na pesa za kutosha.

Je, elimu ya sayansi na maendeleo ya teknolojia ya kitiba yatatusaidia kuondoa vizuizi hivi? Je, hivi karibuni tutaona ulimwengu usio na magonjwa? Kwa kweli, mambo yaliyotajwa hayatoi jibu la wazi. Hata hivyo, Biblia inajibu swali hilo. Makala inayofuata itazungumzia kile ambacho Biblia inasema kuhusiana na wakati ujao ambapo magonjwa hayatakuwapo tena.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 10 Neno “nano” linatokana na neno la Kigiriki mbilikimo linalomaanisha “sehemu moja ya bilioni.”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

Eksirei ya kompyuta

Picha za mwili wa mwanadamu zilizo wazi na sahihi zaidi zinaweza kusaidia kugundua ugonjwa mapema

[Hisani]

© Philips

Siemens AG

Upasuaji wa kutumia roboti

Roboti zilizo na vifaa vya kufanya upasuaji huwasaidia madaktari kufanya upasuaji mgumu kwa usahihi wa hali ya juu

[Hisani]

© 2006 Intuitive Surgical, Inc.

Nanomedicine

Mashine ndogo sana ambazo huenda zitawasaidia madaktari kutibu magonjwa ndani ya chembe. Picha inaonyesha wazo la mchoraji la “nanomachine,” yaani, roboti ndogo sana ambazo zinaweza kuiga utendaji wa chembe nyekundu za damu

[Hisani]

Artist: Vik Olliver (vik@diamondage.co.nz)/Designer: Robert Freitas

Genomics

Kwa kuchunguza muundo wa chembe za urithi katika mwili wa mtu, wanasayansi wanatazamia kwamba wataweza kugundua na kuzuia ugonjwa mapema kabla mtu hajapatwa na ugonjwa wenyewe

[Hisani]

Chromosomes: © Phanie/Photo Researchers, Inc. ▸

[Sanduku katika ukurasa wa 8, 9]

Maadui Sita Ambao Hawajashindwa

Ujuzi wa kitiba na teknolojia inayohusiana nayo inaendelea kuongezeka kwa kiwango kisichotazamiwa. Licha ya hayo, magonjwa ya kuambukizwa yanaendelea kuikumba dunia. Magonjwa yanayosababisha vifo yaliyoorodheshwa hapa chini bado hayajashindwa.

UKIMWI

Watu milioni 60 wameambukizwa virusi vya UKIMWI na milioni 20 hivi wamekufa kutokana na UKIMWI. Katika mwaka wa 2005 watu milioni tano waliambukizwa na zaidi ya watu milioni tatu walikufa kutokana na UKIMWI. Watoto zaidi ya 500,000 walikuwa kati ya watu waliokufa. Watu wengi kati ya wale walioambukizwa virusi vya UKIMWI hawawezi kupata matibabu yanayofaa.

Kuharisha

Unasemekana kuwa ugonjwa unaowaua maskini kwani kila mwaka watu bilioni nne hivi huambukizwa. Ugonjwa huo unasababishwa na magonjwa mbalimbali ya kuambukiza yanayoweza kupitishwa kwa maji au chakula kilichochafuliwa au kwa sababu ya kutotunza usafi. Watu zaidi ya milioni mbili hufa kila mwaka kutokana na maambukizo hayo.

Malaria

Kila mwaka, watu milioni 300 hivi hupatwa na malaria. Milioni moja hivi kati yao hufa kila mwaka, na wengi wao ni watoto. Kila sekunde 30 mtoto mmoja Afrika hufa kutokana na malaria. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), “bado sayansi haina dawa yenye nguvu ya kukabiliana na malaria na wengi wanashuku ikiwa kutawahi kuwa na dawa kama hiyo.”

Surua

Katika mwaka wa 2003, surua iliua zaidi ya watu 500,000. Ni rahisi sana kuambukizwa ugonjwa huo ambao huwaua watoto wengi. Kila mwaka watu milioni 30 hupatwa na surua. Kwa kushangaza, kwa miaka 40 iliyopita kumekuwa na chanjo ya ugonjwa huo inayofanya kazi na isiyogharimu pesa nyingi.

Nimonia

Shirika la WHO linasema kwamba watoto wengi zaidi hufa kutokana na nimonia kuliko ugonjwa mwingine wa kuambukizwa. Watoto milioni mbili hivi walio na umri usiozidi miaka miwili hufa kila mwaka kutokana na nimonia. Wengi wao hufa Afrika na Kusini-Mashariki mwa Asia. Katika sehemu nyingi ulimwenguni, wagonjwa wengi hawapati matibabu yenye kuokoa uhai kwa sababu ya kukosekana kwa huduma za afya.

Kifua Kikuu

Katika mwaka wa 2003, kifua kikuu kilisababisha vifo vya watu zaidi ya 1,700,000. Kutokea kwa viini vya ugonjwa huo vinavyoweza kustahimili dawa kumewahangaisha sana maofisa wa afya. Bakteria fulani zimesitawisha uwezo wa kujikinga dhidi ya dawa fulani za kupigana na kifua kikuu. Bakteria hizo hujitokeza katika miili ya wagonjwa ambao hawatibiwi inavyofaa au ambao hawatibiwi kikamili.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]

Mbinu za Badala za Matibabu

Kuna njia mbalimbali za matibabu ambazo hazikubaliwi na wataalamu wa kitiba. Kwa kawaida mbinu hizo husemwa kuwa matibabu ya kienyeji au matibabu ya badala. Katika nchi zinazoendelea, watu wengi sana hutegemea matibabu ya kienyeji wanapokuwa wagonjwa. Katika maeneo yenye umaskini watu wengi hawawezi kugharimia matibabu ya kitaalamu, huku watu wengine wakipendelea tu matibabu ya kienyeji.

Matibabu ya badala yanazidi kuongezeka katika nchi zilizoendelea. Kati ya matibabu yanayopendwa kuna kuchoma sindano ili kuamsha fahamu, urekebishaji maungo, kumtia mtu viini vya ugonjwa fulani kabla ya kupatwa na ugonjwa wenyewe ili awe na uwezo wa kukabiliana nao, matibabu ya kiasili, na miti-shamba. Baadhi ya mbinu hizo zimechunguzwa kisayansi na kuthibitishwa kuwa zenye manufaa katika hali fulani. Hata hivyo, hakuna uthibitisho wa kutosha kwamba mbinu fulani kati ya hizo huwa na matokeo. Kuongezeka kwa umaarufu wa mbinu mbalimbali kumefanya watu kadhaa waanze kujiuliza ikiwa mbinu hizo ni salama. Katika nchi nyingi watu wanaotoa matibabu hayo wako huru kufanya lolote watakalo. Hilo huandaa mazingira ambamo watu wanaweza kujitibu, bidhaa bandia, na kuwepo kwa madaktari wasio wa kweli. Ingawa wana nia njema, marafiki na watu wa ukoo ambao hawana ujuzi wowote wa kitiba huanza kutoa mashauri kuhusiana na matibabu. Mambo hayo yote yamechangia watu kuwa na hali mbaya ya afya.

Katika nchi kadhaa ambako kuna sheria za kudhibiti mbinu hizo za matibabu, wataalamu wa afya wanazidi kuzikubali na madaktari fulani hutumia mbinu hizo. Hata hivyo, inaonekana kwamba hakuna uthibitisho kuwa mbinu hizo zitatokeza ulimwengu usiokuwa na magonjwa.