Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kila Mtu Anataka Afya Nzuri!

Kila Mtu Anataka Afya Nzuri!

Kila Mtu Anataka Afya Nzuri!

ZAIDI ya miaka 2,700 iliyopita, nabii fulani alitaja kwamba kuna siku inayokuja ambapo magonjwa hayatakuwapo tena. Unabii huo umehifadhiwa hadi leo hii na unapatikana katika maandishi ya kale ya Isaya. Aliandika kuhusu siku ambayo “hakuna mkaaji atakayesema: ‘Mimi ni mgonjwa.’” Pia aliandika: “Wakati huo macho ya vipofu yatafunguliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa. Wakati huo kilema atapanda juu kama vile paa anavyofanya, na ulimi wa bubu utapaaza sauti kwa furaha.” (Isaya 33:24; 35:5, 6) Unabii mwingine mwingi katika Biblia pia unataja wakati ujao kama huo. Kwa mfano, kitabu cha mwisho katika Biblia, Ufunuo, kinataja wakati ambapo Mungu atayaondoa maumivu.—Ufunuo 21:4.

Je, ahadi hizo zitatimia? Je, kweli kuna siku ambayo wanadamu watakuwa na afya nzuri bila magonjwa yoyote? Ni kweli kwamba siku hizi watu wengi wana afya nzuri kuliko nyakati za zamani. Lakini kuwa na afya nzuri tu hakumaanishi kwamba mtu ana afya inayofaa kabisa. Bado magonjwa yanawalemea watu wengi. Wazo tu lenyewe la kwamba unaweza kushikwa na ugonjwa hufadhaisha sana. Na ukweli mtupu ni kwamba hata katika enzi hizi zetu zenye maendeleo, hakuna mtu anayeweza kuepuka mashambulizi ya magonjwa yanayoathiri mwili na akili.

Gharama ya Ugonjwa

Magonjwa husababisha matatizo mengi. Tatizo moja linalohangaisha sana ni gharama ya kifedha. Kwa mfano, katika mwaka mmoja wa karibuni kule Ulaya, siku milioni 500 za kazi zilipotezwa kwa sababu ya magonjwa. Na ndivyo ilivyo sehemu nyinginezo. Kupungua kwa utendaji wa kazi na gharama inayoongezeka ya kuyatibu magonjwa hutokeza mzigo mkubwa sana wa kifedha unaowalemea watu wote. Mashirika ya kibiashara na serikali hulemewa na gharama hizo. Sasa ili mashirika kama hayo yasipate hasara, yanaongeza bei ya bidhaa zao nayo serikali hupandisha kodi. Ni nani anayelipia mambo hayo yote? Ni wewe mwenyewe!

Kwa kusikitisha, ni vigumu kwa maskini kupata matibabu mazuri au hata kutibiwa. Na hiyo ndiyo hali inayowakumba mamilioni ya watu wanaoishi katika nchi maskini ambao hawana huduma bora za afya. Hata katika nchi zilizo tajiri, wengine wanalazimika kujitahidi sana ili kupata huduma bora za afya. Mara nyingi, wengi kati ya watu milioni 46 kule Marekani ambao hawana bima ya afya wana shida hiyo.

Na magonjwa hayatokezi gharama ya kifedha tu. Madhara makubwa zaidi ni ule mfadhaiko wa mtu anayeugua ugonjwa unaofisha, ule msononeko wa maumivu yasiyokoma, ile huzuni ya kuwaona watu wagonjwa sana, na huzuni ya kufiwa.

Tumaini la kwamba siku moja watu wataishi bila magonjwa linafurahisha sana. Kila mtu anataka afya nzuri! Hata kama inaonekana jambo hilo haliwezekani, wengi wanaamini kwamba litatendeka. Kuna wengine wanaoamini kwamba hatimaye teknolojia itaondoa maradhi yote na magonjwa yote. Na wengine wanaoweka imani katika Biblia wanaamini Mungu atatimiza unabii wake wa zamani kuhusu ulimwengu usio na magonjwa. Je, mwanadamu ataweza kuyaondoa magonjwa? Vipi Mungu? Tutarajie nini wakati ujao?