Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kwa kipindi cha miezi 15, watoto wachanga 82 walipatikana wakiwa wametupwa kwenye mitaa ya jiji la Mexico City, na 27 kati yao walikuwa wamekufa.—EL UNIVERSAL, MEXICO.

Uchunguzi uliofanywa katika mapango mawili katika mbuga ya kitaifa ya California, Marekani, umeonyesha aina 27 mpya za wanyama. “Hii inaonyesha jinsi tusivyojua mengi kuhusu ulimwengu unaotuzunguka,” anasema Joel Despain mtaalamu wa mapango katika mbuga hiyo.—SMITHSONIAN, MAREKANI.

Asilimia 20 ya watu duniani wanakosa maji ya kunywa yanayofaa. Asilimia 40 nao wanakosa mfumo wa maji safi.—MILENIO, MEXICO.

Wawindaji haramu wanaua kati ya wanyama 20,000 na 30,000 kwa mwaka katika Mbuga ya Kitaifa ya Serengeti pekee.—THE DAILY NEWS, TANZANIA.

Uchunguzi uliofanywa Barcelona, Hispania, unaonyesha kwamba mwanafunzi 1 kati ya 3 walio na umri wa miaka 16 anavuta bangi kwa kawaida.—LA VANGUARDIA, HISPANIA.

Viini Ofisini

Wanabiolojia katika Chuo Kikuu cha Arizona walipima bakteria katika ofisi za majiji kadhaa huko Marekani. Gazeti Globe and Mail linasema waligundua kwamba “sehemu tano zilizo na viini vingi zaidi ni (kwa mpangilio) simu, kompyuta, vishikio vya mabomba ya maji, vishikio vya milango ya mikrowevu, na kibodi.” Kulingana na ripoti hiyo, “kompyuta ya kawaida ina bakteria 100 zaidi ya zile zilizo juu ya meza ya jikoni na bakteria 400 zaidi ya zile zilizo juu ya choo cha kukalia.”

“Wakristo kwa Jina Tu”

Inasemekana kwamba Filipino ndiyo nchi pekee ya “Kikristo” katika bara lote la Asia. Hata hivyo, Askofu Efraim Tendero wa Baraza la Makanisa ya Kiinjilisti la Filipino alisema hivi: “Wengi wetu ni Wakristo kwa jina tu bali si kwa vitendo.” Kama ilivyosemwa katika gazeti Manila Bulletin, viongozi wa kidini wanapaswa kulaumiwa kwa kiasi fulani kwani wao ndio wameshindwa “kuwafunza na kuwasaidia watu waithamini Biblia.” Inasemekana kwamba misa fulani za kanisa hukazia hasa siasa badala ya Maandiko.

Watu na Wanyama Wanapigania Chakula

Gazeti The East African la Nairobi linaripoti hivi: “Limekuwa jambo la kawaida kusikia kuhusu nyani na fisi wanaovamia vijiji vilivyokumbwa na ukame huko Somalia.” Pigano moja lilisababisha vifo vya nyani kadhaa na kuwajeruhi wafugaji fulani. Inasemekana kwamba makundi ya tumbili husubiri “mahali panapofaa zaidi kwenye njia panda au juu ya madaraja” ili wavamie malori yanayopeleka chakula sokoni. “Ni jambo la kawaida kuwaona wanyama hao wakikimbia huku wamebeba mafungu ya ndizi au matikiti-maji [makubwa],” linasema gazeti hilo.

Usafiri wa Meli Unaathiri Hewa ya Pwani

Gazeti Kölner Stadt-Anzeiger la Ujerumani, linaripoti kwamba msongamano wa meli kwenye bandari zenye shughuli nyingi unaweza kuathiri hali ya hewa ya pwani. Wachunguzi katika Taasisi ya Max Planck ya Hali ya Hewa ya Hamburg, walichunguza kufanyizwa kwa mawingu katika Mlango-Bahari wa Uingereza. Waligundua kwamba mawingu katika maeneo ya pwani yalikuwa mepesi zaidi ilhali mawingu yaliyo juu ya maji yalikuwa mazito zaidi. Inasemekana kuwa hilo linasababishwa na moshi wa meli. Imegunduliwa kwamba chembe-chembe za masizi zilizotokana na moshi wa meli hufanyiza mvuke ambao unasaidia kutengeneza matone ya mvua. Gazeti hilo linasema hivi: “Kwa miaka 50 iliyopita, matumizi ya mafuta katika meli yameongezeka mara nne zaidi.”