Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ladybird—Rafiki ya Mtunza-Bustani

Ladybird—Rafiki ya Mtunza-Bustani

Ladybird—Rafiki ya Mtunza-Bustani

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

INGAWA mbawakawa hawapendwi na kila mtu, mdudu huyu mwekundu mwenye madoadoa meusi anayeitwa ladybird (coccinelle katika Kifaransa) hupendwa na wengi. Wadudu hao huwasisimua watoto, nao watunza-bustani na wakulima huwakaribisha kwa mikono miwili. Kwa nini wanapendwa sana?

Kwa Nini Wanapendwa?

Jamii nyingi za mdudu huyu mwenye faida hupenda kula aphids (puceron) (wanaoonyeshwa kushoto), wadudu wadogo wenye miili laini ambao hufyonza umajimaji kwenye mimea. Ladybird waliokomaa wanaweza kula maelfu ya aphids maishani. Navyo viwavi vya ladybird hula sana pia. Isitoshe, mbawakawa huyu hula wadudu wengine wengi waharibifu, na wengine hupenda sana kula kuvu. Basi haishangazi kwamba watunza-bustani na wakulima huwakaribisha kwa mikono miwili!

Katika miaka ya mwishoni ya karne ya 19, wadudu wanaojulikana kama cottony-cushion scale waliingizwa kimakosa huko California, Marekani kutoka Australia. Wadudu hao waharibifu waliongezeka kwa haraka sana hivi kwamba walitisha kuharibu jamii yote ya michungwa. Kwa kuwa alijua kwamba huko Australia mdudu huyo hakutishia kuharibu mimea, mtaalamu mmoja wa elimu ya wadudu alienda Australia ili kutafuta adui wake wa asili. Aligundua adui wake kuwa ladybird anayeitwa vedalia. Ladybird 500 hivi kati yao walipelekwa huko California, na katika mwaka mmoja tu mdudu huyo mharibifu alikuwa karibu kuangamizwa. Mashamba ya michungwa ikaokolewa.

Maisha ya Ladybird

Mbawakawa huyo mdogo mwenye kupendeza ana mwili wenye umbo la mviringo au la yai na sehemu ya chini iliyo bapa. Licha ya kwamba wao hula sana, jamii nyingi za mdudu huyo zina urefu usiozidi milimeta 12. Vifuniko vigumu vya mabawa na vyenye kumetameta hufunika mabawa yake mororo ili kuyalinda na kumfanya awe na rangi zinazopendeza. Mdudu huyo anaporuka vifuniko hivyo hufunguka. Ingawa mara nyingi mdudu huyo huonyeshwa akiwa na rangi nyekundu na madoadoa meusi, jamii 5,000 hivi za ladybird zina rangi na madoadoa mbalimbali. Wengine wana rangi ya machungwa au manjano na madoadoa meusi. Wengine ni weusi na madoadoa mekundu. Wachache hawana madoadoa. Nao wengine wana rangi za mistarimistari.

Jamii nyingi huishi kwa mwaka mmoja. Wakati wa majira ya baridi kali, ladybird waliokomaa hukaa bila kufanya kazi katika sehemu kavu iliyokingwa na baridi. Wanapoamka baada ya joto kuanza, wao huruka wakitafuta mimea inayoliwa na aphids. Baada ya kujamiiana, ladybird wa kike hutaga mayai yake madogo yenye rangi ya manjano (yaliyoonyeshwa kulia) chini ya jani karibu na eneo lenye aphid wengi. Kila yai huangua kiwavi aliye na miguu sita ambaye huonekana kama mamba mdogo (anayeonyeshwa kushoto). Kwa kuwa kiwavi hutumia wakati mwingi akila aphids, baada ya muda fulani yeye huwa mkubwa kuliko ngozi yake. Baada ya kuambua ngozi yake mara kadhaa, yeye hujishikilia kwenye mmea na kutokeza ngozi ya pupa. Ndani ya pupa, kiwavi huendelea kukua hadi ladybird aliyekomaa anapotokea. Kwa kuwa mwanzoni yeye huwa na mwili mwororo na mwenye rangi hafifu, yeye hubaki kwenye mmea huo hadi mwili wake unapokuwa mgumu. Katika siku moja alama zake za pekee hutokea.

Maadui hujifunza kumwepuka mdudu huyo mwenye rangi ya kuvutia. Anapotishwa, mdudu huyo hutoa umajimaji wa rangi ya manjano unaonuka na wenye ladha mbaya unaotoka katika viungio vyake. Wawindaji, kama vile ndege au buibui, hawasahau mara ya kwanza walipokutana na wadudu hao, na rangi yao ya kuvutia huwakumbusha jambo hilo.

Ladybird Mwenye Tatizo

Jamii moja ya ladybird iliyotumiwa kuharibu aphids, imekuwa tatizo pia. Ladybird anayeitwa harlequin, anaishi kwa furaha pamoja na jamii nyingine katika eneo lake la kiasili huko kaskazini-mashariki mwa Asia. Kwa sababu yeye hula sana aphids na wadudu wengine waharibifu, hivi karibuni aliingizwa Amerika Kaskazini na Ulaya. Kwa kusikitisha, harlequin amehatarisha ladybird wengine wa kiasili kwa kula chakula chao chote. Isitoshe, chakula chake kikiisha, na bila wawindaji wake wa asili, yeye huwageukia ladybird wengine na wadudu wengine wenye manufaa. Wataalamu wa wadudu wana wasiwasi kuhusu wakati ujao kwa sababu wanaona kwamba jamii fulani za ladybird zitatoweka. Harlequin pia huchukiwa kwa sababu ya kula matunda mabivu ambayo yako tayari kuvunwa na kwa sababu wao huvamia nyumba kwa wingi kabla ya majira ya baridi kali kuanza.

Jamii nyingine za ladybird hula mimea yenye thamani badala ya kula wadudu waharibifu. Hata hivyo, inapendeza kwamba jamii nyingi huwafurahisha watunza-bustani.

Mkaribishe Ladybird

Unaweza kuwavutiaje ladybird katika shamba lako? Maua huwavutia kwa kutoa chavua na nekta. Magugu na maji kwenye bakuli pia yaweza kuwavutia. Ikiwezekana, epuka kutumia kemikali kuua wadudu. Majani yaliyokauka yakiachwa kwenye mimea au juu ya ardhi wakati wa majira ya baridi kali yanaweza kuwa mahali panapofaa pa kujificha. Usikanyage wadudu au mayai yoyote unayoona shambani. Huenda ukawa unaua kizazi kinachofuata cha ladybird.

Kumbuka, wadudu wachache tu kati ya hawa wanaweza kukusaidia kuondoa wadudu waharibifu bila kutumia kemikali zenye kudhuru. Ukiwatunza watakutunza pia. Ladybird ni uthibitisho mwingine wa hekima ya Muumba wetu, kama mtunga-zaburi alivyosema: “Jinsi kazi zako zilivyo nyingi, Ee Yehova! Zote umezifanya kwa hekima. Dunia imejaa vitu ulivyotokeza.”—Zaburi 104:24.

 

 

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Top: © Waldhäusl/Schauhuber/Naturfoto-Online; left two: Scott Bauer/Agricultural Research Service, USDA; middle: Clemson University - USDA Cooperative Extension Slide Series, www.insectimages.org; eggs: Bradley Higbee, Paramount Farming, www.insectimages.org

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Left: Jerry A. Payne, USDA Agricultural Research Service, www.insectimages.org; 2nd from left: Whitney Cranshaw, Colorado State University, www.insectimages.org; 3rd from left: Louis Tedders, USDA Agricultural Research Service, www.insectimages.org; 4th from left: Russ Ottens, The University of Georgia, www.insectimages.org; ladybirds on a leaf: Scott Bauer/Agricultural Research Service, USDA