Safina ya Noa na Uundaji wa Meli
Safina ya Noa na Uundaji wa Meli
KWA zaidi ya miaka 40 sasa, nimekuwa nikifanya kazi ya kuchora ramani za ujenzi wa meli na uhandisi wa vyombo vya baharini. Kazi yangu inahusisha kubuni vyombo mbalimbali vyenye ukubwa na muundo tofauti-tofauti, kutia ndani mitambo na mifumo mingine inayotumiwa kuiendeshea. Mnamo 1963, nilipokuwa nikiishi huko British Columbia, Kanada, mmoja wa Mashahidi wa Yehova alinionyesha kwamba kitabu cha Biblia cha Mwanzo kinaeleza kuwa safina ya Noa ilikuwa kama boksi ndefu au sanduku. Maelezo hayo yalinipendeza sana na nikaamua kuyachunguza zaidi.
Simulizi la Mwanzo linaonyesha kwamba Mungu alikusudia kuondoa uovu duniani kupitia gharika. Alimwamuru Noa ajenge safina ili kujihifadhi yeye mwenyewe, familia yake na baadhi ya wanyama kutokana na Gharika. Mungu alimwambia Noa ajenge safina yenye urefu wa mikono 300, upana wa mikono 50, na kimo cha mikono 30. (Mwanzo 6:15) Kulingana na makadirio ya watu fulani, hilo lina maana kwamba safina ilikuwa na urefu wa meta 134, upana wa meta 22, na kimo cha meta 13 hivi. *
Muundo wa Safina
Safina ilikuwa na ghorofa tatu ambazo ziliiimarisha na kuifanya kuwa na ukubwa wa meta 8,900 za mraba. Ilijengwa kwa mbao zenye utomvu ambazo huenda zilikuwa za mvinje kwa hiyo hazingeweza kupenya maji nayo ilifunikwa ndani na nje kwa lami. (Mwanzo 6:14-16) Hatuambiwi jinsi ambavyo Noa aliunganisha mbao hizo. Lakini hata kabla ya simulizi la Gharika, Biblia inawataja wafuaji wa vifaa vya shaba na chuma. (Mwanzo 4:22) Vyovyote vile, hadi leo hii, misumari ya mbao hutumiwa kujenga meli zilizojengwa kwa mbao.
Safina ilikuwa na vyumba, mlango upande mmoja, na tsohari mkono mmoja kwenda juu, ambayo huenda ilikuwa paa yenye mwinuko wa pembe tatu, labda ilikuwa na mianya ya kuingizia hewa na mwangaza. Hata hivyo, simulizi la Mwanzo halisemi kwamba kwenye safina kulikuwa na mkuku, omo, matanga, makasia, au usukani. Kwa kweli, neno “safina” la Kiebrania hutumiwa pia kuwakilisha kikapu chenye bereu kinachoweza kuelea ambacho mama ya Musa alitumia kumhifadhi juu ya Mto Nile.—Kutoka 2:3, 10.
Uwezo Mzuri wa Kuelea
Urefu wa safina ulikuwa mara sita zaidi ya upana wake na mara kumi zaidi ya kimo chake. Meli nyingi za kisasa zina vipimo kama hivyo, ingawa mara nyingi tofauti kati ya urefu na upana wake huamuliwa kwa kutegemea nguvu zinazohitajika ili meli isonge majini. Kwa upande ule mwingine safina ilihitaji tu kuelea. Uwezo wake wa kuelea ulikuwaje?
Uwezo wa chombo cha majini kukabiliana na upepo na mawimbi unahusiana sana na upatano katika vipimo vyake. Biblia inafafanua mvua kubwa iliyotokeza Gharika na pia inasema kwamba baadaye Mungu alitokeza upepo. (Mwanzo 7:11, 12, 17-20; 8:1) Maandiko hayasemi kuhusu nguvu ya mawimbi na upepo uliovuma lakini inawezekana kwamba yalikuwa yenye nguvu na yenye kubadilika-badilika, kama ilivyo leo. Upepo ukivuma kwa muda mrefu na kwa nguvu sana mawimbi huinuka zaidi na kusukumwa mbali zaidi. Isitoshe, utendaji wowote chini ya bahari ungeweza kutokeza mawimbi makubwa.
Vipimo vyenye upatano vya safina viliisaidia iwe imara. Vilevile safina iliundwa kwa njia ambayo ingeweza kukabiliana na nguvu ambazo zingeiinua na kuifanya ipige maji kwa mbele au nyuma wimbi linapopita. Halingekuwa jambo lenye kustarehesha kwa watu na wanyama iwapo wimbi lingeinua upande mmoja wa safina na kuiruhusu ipige maji kwa nguvu. Kupiga maji kwa njia hiyo hutahini uimara wa chombo. Chombo kinapaswa kuwa na nguvu za kutosha ili kisijipinde upande wa chini iwapo mawimbi mawili makubwa yangeinua miisho yote miwili kwa wakati uleule. Hata hivyo, wimbi kubwa linapoinua sehemu ya katikati ya chombo bila kuwa na kitu cha kushikilia miisho yake, huenda omo na tezi zikajipinda. Mungu alimwambia Noa ajenge safina kwa kutumia urefu unaozidi kina kwa mara 10. Baada ya mikasa mingi, watengeneza-meli wa baadaye walijifunza kuwa vipimo hivyo vinaweza kuhimili mikazo hiyo.
Salama na Yenye Kustarehesha
Kwa sababu safina ilikuwa na umbo kama la sanduku, nguvu zinazofanya meli ielee zingekuwa zilezile kutoka mwisho mmoja wa safina hadi ule mwingine. Vilevile uzito wake ungepatana. Inaelekea Noa alihakikisha kwamba mizigo ilisawazishwa vizuri, kutia ndani wanyama na chakula cha mwaka mzima. Kusawazisha uzito vizuri hupunguza mkazo wa ziada unaoletwa na mizigo. Kwa hiyo mambo mawili muhimu yaliyochangia uwezo wa safina na abiria wake kustahimili Gharika ya ulimwenguni pote kwa usalama, yalikuwa muundo wake uliotolewa na Mungu na ulinzi wa Yehova. Bila shaka, Mungu alihakikisha kwamba safina ilitua mahali salama na panapofaa.
Uchunguzi wangu makini kuhusu hilo ulinifanya nifikie mkataa kwamba yale ambayo Biblia inasema kuhusu safina ya Noa ni halisi na yanapatana na ujenzi wa leo wa meli. Bila shaka, kuna mambo mengi kuhusu safina na Gharika ambayo hayatajwi katika simulizi la Mwanzo. Ninatumaini kwamba siku moja, baada ya ufufuo, nitakutana na Noa hapa duniani katikati ya familia za wanadamu na wanyama ambao wako hai kwa sababu ya safina aliyofanya kazi nyingi na ngumu ili kujenga. (Matendo 24:15; Waebrania 11:7) Kwanza, nitamshukuru yeye na familia yake. Kisha nitambwagia maswali chungu nzima.—Tumetumiwa makala hii.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Mkono ni kipimo cha kale kinacholingana na urefu kutoka kwenye kiwiko cha mkono hadi kwenye ncha ya vidole. Nyakati za Waisraeli, kipimo cha mkono kwa ujumla kilikuwa sawa na sentimeta 44.5.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 22]
MFANO WA SAFINA
Kwa kutumia vipimo vilivyoonyeshwa unaweza kutengeneza na kujaribu mfano wa safina. (Unaweza kuongeza ukubwa wa mfano huo kwa kuongeza vipimo vilivyoonyeshwa hapa chini kwa upatano.) Ili karatasi ya kawaida isipitishe maji unaweza kuipaka nta au penseli ya rangi (crayon). Kisha unaweza kuikunja karatasi hiyo na kushikanisha kona zake kwa gundi. Ongeza uzito wa safina yako kwa kubandika kwa gundi vitu vyenye uzito ndani ya safina kama vile sarafu, na usizirundike sarafu hizo mahali pamoja. Endelea kuongeza uzito huo mpaka karibu nusu ya safina hiyo iwe ndani ya maji.
Ili kuona uwezo wa safina kusafiri juu ya maji, weka safina uliyotengeneza katikati ya beseni lililojaa maji, sambamba na urefu wa beseni. Jaribu kufanyiza mawimbi madogo kwa kushikilia boksi ndogo mwishoni mwa beseni na kuididimiza ndani ya maji polepole na kurudiarudia kwa utaratibu.
[Picha]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
KUNJA NDANI KUNJA NDANI
KUNJA NDANI KUNJA NDANI
[Picha]
Upatano wa vipimo vya vyombo vinavyosafiri baharini ni sawa na ule wa safina
[Picha katika ukurasa wa 20, 21]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Mbele
Upande
Juu
Mbele
Upande
Juu
[Picha]
Safina ilikuwa na ukubwa kama ule wa “Titanic”
[Hisani]
Titanic plan: Courtesy Dr. Robert Hahn/www.titanic-plan.com; photo: Courtesy of The Mariners’ Museum, Newport News, VA