Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Tumbawe Kubwa la Belize—Eneo Linalostahili Kuhifadhiwa

Tumbawe Kubwa la Belize—Eneo Linalostahili Kuhifadhiwa

Tumbawe Kubwa la Belize—Eneo Linalostahili Kuhifadhiwa

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO

“Kuzorota au kutoweka kwa kitu chochote cha kitamaduni au cha kiasili huchangia uharibifu wa urithi wa mataifa yote ulimwenguni. . . . Ni jukumu la jumuiya ya kimataifa kushiriki katika kuhifadhi urithi wa kitamaduni na wa kiasili ulio na thamani isiyo na kifani.” —Imetolewa katika Kongamano la Shirika la UNESCO la Maeneo Yanayostahili Kuhifadhiwa.

KUPATANA na maneno yaliyotajwa juu, katika mwaka wa 1996, Hifadhi ya Tumbawe Kubwa la Belize iliorodheshwa kati ya Maeneo Yanayostahili Kuhifadhiwa Ulimwenguni. Iliwekwa kati ya maeneo kama vile, Machu Picchu huko Peru, Korongo Kuu huko Marekani, na maeneo mengine ya ajabu kama hayo ulimwenguni. Ni nini hufanya eneo hilo liwe na “thamani isiyo na kifani”?

Urithi Unaostahili Kuhifadhiwa

Tumbawe Kubwa la Belize ni tumbawe la pili kwa ukubwa ulimwenguni, baada ya Tumbawe Kubwa la Australia, nalo ndilo ndefu zaidi katika Kizio cha Magharibi. Likiwa na urefu wa kilomita 300, linapatikana kwenye Rasi ya Yucatán nalo limechukua sehemu kubwa ya pwani ya Belize, nchi inayopatikana Amerika ya Kati. Mbali na matumbawe haya, hifadhi hiyo ina visiwa vidogo 450 vya mchanga, visiwa vitatu vya matumbawe, na miamba yenye umbo la pete iliyo na nyangwa zenye kuvutia. Kuna maeneo saba ya bahari katika hifadhi hiyo yaliyo na ukubwa wa kilomita 960 za mraba ambayo yanalindwa na mkataba wa Kongamano la Maeneo Yanayostahili Kuhifadhiwa.

Umuhimu wa kuhifadhi matumbawe unaonekana wazi kwa kuwa robo moja ya mimea na wanyama wa baharini huishi humo. Kwa kweli, ni misitu ya mvua pekee iliyo na viumbe wengi zaidi ya wale wanaopatikana katika matumbawe. Hata hivyo, wanasayansi wanaonya kwamba asilimia 70 ya matumbawe yote duniani yatakuwa yameharibiwa katika miaka 20 au 40 inayokuja isipokuwa tu wanadamu waache tabia zisizofaa kama vile, uchafuzi, kumwaga maji-taka baharini, uvuvi wa kutumia sumu, na kuharibu matumbawe kwa utalii usiodhibitiwa.

Jamii 70 za matumbawe magumu, 36 za matumbawe laini, na jamii 500 za samaki zimegunduliwa katika Hifadhi ya Tumbawe Kubwa la Belize. Ni makao ya wanyama wa baharini wanaokabili hatari ya kutoweka kama vile, kasa wanaoitwa loggerhead, green, na hawksbill, na pia nguva na mamba wa Amerika. Akieleza kuhusu unamna-namna wa ajabu wa viumbe vya baharini katika eneo hilo, mchunguzi wa matumbawe Julianne Robinson anasema: “Huwatolea wachunguzi na watalii nafasi ya kujionea mambo mengi ya kipekee. . . . Eneo hilo ni kati ya maeneo machache ambayo unaweza kujionea vitu vya asili vikiwa katika mazingira yake ya asili, lakini linakabili hatari.”

Labda hatari kubwa zaidi ambayo tumbawe la Belize linakabili ni kupoteza rangi kwa matumbawe, kwani matumbawe yenye rangi mbalimbali hubadilika na kuwa meupe kwa kiasi fulani. (Ona sanduku katika ukurasa wa 26.) Ripoti ya National Geographic News ilisema kwamba mnamo 1997 na 1998 Tufani Mitch ilipokuwa ikipiga, matumbawe mengi yalipoteza rangi sana hivi kwamba asilimia 48 kati ya matumbawe hayo yaliharibiwa. Uharibifu huo ulisababishwa na nini? Ingawa bado utafiti unaendelea, mtaalamu wa matumbawe Melanie McField anasema hivi: “Huku kupoteza rangi kwa matumbawe kunahusiana sana na kuongezeka kwa joto baharini. . . . Miale ya jua pia husababisha matumbawe kupoteza rangi na mambo hayo mawili yanapotokea wakati mmoja yanasababisha matumbawe kupoteza rangi sana.” Kwa kupendeza, inaonekana kwamba tumbawe la Belize linajirekebisha polepole. *

Paradiso Ndani ya Bahari

Maji safi ya tumbawe la Belize yana kiwango cha joto la nyuzi 26 Selsiasi, ni mahali pazuri pa kupiga mbizi. Asilimia 90 ya tumbawe hilo halijachunguzwa. Mtu anaweza kulifikia kwa urahisi kupitia San Pedro katika Kisiwa cha Ambergris, kilicho umbali wa zaidi ya mita 100. Kilomita sita kusini-mashariki ya San Pedro kuna Hifadhi ya Bahari ya Hol Chan, bustani iliyo chini ya maji yenye ukubwa wa kilomita nane za mraba ambayo ni mwingilio wa kuelekea kwenye tumbawe.

Miongoni mwa maeneo yanayovutia zaidi kwa kupiga mbizi ni Blue Hole linalopatikana katika hifadhi hiyo ambalo ni moja kati ya Maeneo Yanayostahili Kuhifadhiwa. Blue Hole liko katikati ya Tumbawe la Lighthouse, kilomita 100 kutoka pwani ya Belize. Eneo hilo lilifanywa kuwa maarufu na mtaalamu wa bahari Mfaransa Jacques-Yves Cousteau alipolitembelea mwaka wa 1970 akitumia meli ya utafiti iitwayo Calypso. Likiwa katikati ya bahari yenye rangi ya feruzi, Blue Hole ni kisima cha chokaa chenye rangi ya buluu iliyokolea, kilichozungukwa na matumbawe. Kipenyo chake ni cha mita 300 hivi na kina cha zaidi ya mita 120. Kabla ya maji kuongezeka baharini lilikuwa pango kavu lakini baadaye paa lake likaporomoka. Kuta zake zimesimama wima hadi unapofikia mita 35 ambapo kuna mawe ya chokaa yaliyochongoka ambayo yananing’inia. Mandhari ya chini ya bahari ni yenye kustaajabisha sana na unaweza kuona sehemu zote zinazokuzunguka kwa umbali wa mita 60. Kuna wanyama wa baharini wachache sana hapo isipokuwa papa. Kwa kuwa kupiga mbizi katika eneo hilo kunahitaji ustadi wa hali ya juu, wale wasio na uzoefu wa kupiga mbizi hawapaswi kupiga mbizi katika eneo hilo. Hata hivyo, inafurahisha sana kupiga mbizi kwenye maji maangavu yanayozunguka tumbawe hilo.

Karibu na hapo kuna kisiwa cha mchanga kinachoitwa Half Moon, ambacho ni moja kati ya Maeneo saba Yanayostahili Kuhifadhiwa. Eneo hilo linafaa hasa kwa kumlinda ndege anayeitwa red-footed booby ambaye anakabili hatari ya kutoweka. Jamii nyingine 98 hivi za ndege zimepatikana hapa pia. Inapendeza kama nini kupiga mbizi katika kisiwa hicho cha mchanga cha Half Moon kilicho na kina cha mita 1,000 na matumbawe laini yaliyo maridadi.

Kama vile ambavyo tumeona kwa kutembelea Tumbawe Kubwa la Belize, tuna kila sababu ya kuhifadhi hazina hii kwa ajili ya vizazi vinavyokuja. Kweli, kupotezwa kwake kungetokeza “uharibifu wa urithi wa mataifa yote ulimwenguni.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 9 Huenda hakuna mengi yanayoweza kufanywa kuhusu ongezeko la joto duniani linalofanya maji ya bahari yawe na joto jingi, lakini tangu tumbawe hilo liorodheshwe kati ya Maeneo Yanayostahili Kuhifadhiwa watu wa Belize wamechochewa kutunza eneo hilo.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26]

Marijani Kupoteza Rangi

Tumbawe limefanyizwa kutokana na chechevule ambao ni wanyama wadogo sana wanaokula nyama. Sehemu yao ya nje ni ngumu nayo imefanyizwa kwa kalisi-kaboneti au chokaa. Matumbawe hufanyizwa kutokana na mabaki ya kale ya matumbawe yaliyokufa. Mwani wa aina fulani (zooxanthellas) hukua ndani ya tishu za matumbawe nao hushirikiana, kwani mwani hutoa oksijeni na virutubishi ambavyo hutumiwa na chechevule, nao chechevule hutoa kaboni-dioksidi ambayo hutumiwa na mwani. Chechevule huathiriwa na mabadiliko ya kiwango cha joto majini, kwa hiyo kiwango cha joto kinapopanda wao huanza kuwafukuza mwani, na hivyo kupoteza chanikiwiti na kupoteza rangi. Katika hali hiyo dhaifu, matumbawe yanaweza kupatwa na magonjwa na hata kufa. Hata hivyo, yanaweza kupona yakilindwa kutokana na uharibifu.

[Hisani]

Background: Copyright © 2006 Tony Rath Photography - www.trphoto.com

[Ramani katika ukurasa wa 23]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Mexico

BELIZE

Bahari ya Karibea

Bahari ya Pasifiki

[Picha katika ukurasa wa 23]

Picha ya satelaiti ya Belize ikionyesha tumbawe hilo lenye urefu wa kilomita 300

[Picha katika ukurasa wa 24]

Kisiwa cha mchanga kinachoitwa Rendezvous

[Hisani]

©kevinschafer.com

[Picha katika ukurasa wa 24]

Kasa anayeitwa Hawksbill

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Kisima cha Blue Hole kwenye Tumbawe la Lighthouse, lililotokezwa na kuporomoka kwa pango la chokaa

[Hisani]

©kevinschafer.com

[Picha katika ukurasa wa 25]

Tumbawe Kubwa la Belize lina jamii 500 za samaki

[Hisani]

Inset: © Paul Gallaher/Index Stock Imagery

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]

Satellite view: NASA/The Visible Earth (http://visibleearth.nasa.gov/); divers: © Paul Duda/Photo Researchers, Inc.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]

Copyright © Brandon Cole