Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jinsi ya Kukabiliana na Msongamano wa Magari

Jinsi ya Kukabiliana na Msongamano wa Magari

Jinsi ya Kukabiliana na Msongamano wa Magari

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA

UNAENDA kumwona daktari, kwa hiyo unatoka nyumbani ukifikiri una wakati mwingi. Lakini hukutarajia kukuta msongamano wa magari njiani. Kadiri wakati unavyosonga na gari lako linasonga polepole, unaanza kuhangaika. Mwishowe, unafika kwa daktari lakini umechelewa kwa nusu saa.

Mojawapo ya mambo yanayosumbua watu mijini ni msongamano wa magari, hasa wakati magari yanaposonga polepole sana, yakifunga njia na kuchafua hewa. Inasikitisha kwamba hakuna dalili za tatizo hilo linalowakumba mamilioni ya wakaaji wa majiji kubadilika.

Uchunguzi uliofanywa Marekani na Taasisi ya Usafiri ya Texas unaonyesha kwamba “Msongamano uko kila mahali katika maeneo makubwa na madogo.” Ripoti hiyo ilionyesha pia kwamba wenye mamlaka hawawezi kupata suluhisho la kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka ya wasafiri mijini. Hali iko vivyo hivyo duniani kote. Hivi karibuni maelfu ya wasafiri huko China walijikuta kwenye mlolongo wa magari wenye urefu wa kilomita 100 ambao ulichukua polisi siku kadhaa kuuondoa. Mara nyingine kusafiri umbali wa kilomita 20 kupitia Mexico City, kunaweza kuchukua saa nne ukiendesha gari, muda mrefu zaidi kuliko ukitembea.

Si vigumu kujua sababu inayofanya kuwe na msongamano wa magari katika barabara za majiji. Watu wanazidi kuongezeka katika majiji, na sasa karibu nusu ya watu ulimwenguni huishi huko. Kadiri majiji yanavyoendelea kukua, ndivyo idadi ya magari inavyozidi kuongezeka. Mwandishi mmoja alisema hivi: “Watu wengi sana wana magari, nao hulazimika kuyaendesha katika barabara zilezile.”

Ugumu wa Kutatua Tatizo la Msongamano wa Magari

Kwa kuwa wanadamu hutegemea sana magari basi lazima majiji yakabiliane na kuongezeka kwa magari. Jiji la Los Angeles, Marekani, lina watu milioni nne hivi. Lakini sasa kuna magari mengi kuliko watu katika jiji hilo! Ingawa majiji mengine hayana magari mengi kama jiji hilo, ni machache tu yanayoweza kukabiliana na kuongezeka kwa magari. “Majiji yalipoanzishwa hakukuwa na wazo la kuendesha magari humo,” anasema Carlos Guzmán, msimamizi wa Tume ya Jiji la Madrid. Majiji ya kale yaliyo na vijia vyembamba ndiyo hupata matatizo zaidi, lakini hata katika majiji makubwa ya kisasa, kunakuwa na msongamano katika barabara pana, hasa asubuhi na jioni. “Siku hizi kunakuwa na msongamano wa magari siku nzima katika majiji makubwa, nao unazidi kuwa mbaya,” anasema Dakt. Jean-Paul Rodrigue katika ripoti yake “Matatizo ya Kusafiri Jijini.”

Kwa kuwa watu hununua magari haraka kuliko serikali zinavyoweza kujenga barabara, kuongezeka haraka kwa idadi ya magari kunaweza kulemea mtandao bora zaidi wa barabara. “Hatimaye,” kinaeleza kitabu Stuck in Traffic—Coping With Peak-Hour Traffic Congestion, “kujenga barabara mpya au kupanua zile zilizopo hakupunguzi hata kidogo tatizo la msongamano wa magari asubuhi na jioni.”

Pia ukosefu wa maeneo ya kuegesha magari huongeza tatizo hilo. Wakati wowote ule, utakuta magari mengi sana katika barabara za jiji ambayo huenda yanatafuta tu mahali pa kuegesha. Inakadiriwa kwamba uchafuzi wa hewa unaosababishwa na msongamano wa magari, hasa katika majiji, husababisha vifo vya watu 400,000 hivi kila mwaka. Kulingana na ripoti moja, kuna uchafuzi mbaya sana wa hewa jijini Milan, Italia, hivi kwamba kupumua hewa ya jiji hilo kwa siku moja tu ni sawa na kuvuta sigara 15.

Matatizo yanayotokana na msongamano wa magari yanatia ndani saa zinazopotezwa na mfadhaiko ambao madereva hukabili. Ni vigumu kukadiria gharama ya kihisia inayoletwa na tatizo hilo, lakini uchunguzi mmoja nchini Marekani ulikadiria kwamba msongamano wa magari katika majiji 75 makubwa zaidi nchini humo hugharimu dola bilioni 70 kila mwaka. Je, kuna jambo lolote linaloweza kufanywa ili kutatua tatizo hilo?

Njia za Kupunguza Tatizo Hilo

Tayari majiji mbalimbali yamechukua hatua za kukabiliana na hali hiyo. Kwa mfano, Singapore, ambayo ni moja kati ya nchi zenye magari mengi zaidi ulimwenguni, hudhibiti idadi ya magari yanayonunuliwa. Majiji ya kihistoria, kutia ndani majiji fulani nchini Italia, yamepiga marufuku kuendesha magari katikati ya jiji karibu siku nzima.

Njia moja ya kutatua tatizo hilo katika majiji fulani ni kuwepo kwa “ada ya msongamano,” ambayo lazima madereva walipe ili waingie jijini. Huko London mpango huo umefaulu kupunguza msongamano wa magari kwa asilimia 30, na inaonekana majiji mengine yangependa kuiga mfano huo. Katika maeneo kama vile Mexico City, Mexico, magari huruhusiwa kuingia jijini siku fulani tu, ikitegemea nambari ya gari ya usajili.

Mabaraza ya jiji yametenga pesa nyingi ili kuboresha mifumo ya usafiri wa umma, kuboresha barabara kuu, na kujenga barabara kuu zinazopita nje ya jiji. Wao hutumia mifumo ya kompyuta kuongoza taa za barabarani na kuwajulisha polisi kuhusu aksidenti ili wazishughulikie haraka. Njia nyingine za kutatua msongamano ni kuwa na barabara za pekee kwa ajili ya mabasi au kutumia pande zote mbili za barabara ili kuelekeza magari upande mmoja kunapokuwa na msongamano upande mmoja ilhali upande ule mwingine hauna magari mengi. Lakini kufanikiwa kwa mbinu zote hizo kunategemea hasa kushirikiana kwa wakazi.

Unaweza Kufanya Nini?

Yesu Kristo alisema “yoyote munayotaka watu wawatendee ninyi, ninyi muwatendee vivyo hivyo.” (Mathayo 7:12, Zaire Swahili Bible) Mashauri hayo yenye hekima yanaweza kusaidia kupunguza msongamano wa magari. Lakini, ikiwa kila mtu atajifikiria tu, hata miradi bora zaidi haiwezi kufaulu. Tumeorodhesha mapendekezo machache yanayoweza kukusaidia kukabiliana na msongamano wa magari katika jiji lenu.

Ikiwa husafiri mbali, huenda kutembea au kuendesha baiskeli kukawa njia bora ya usafiri. Katika hali nyingi, huenda njia moja kati ya hizo ikawa ya haraka, rahisi, na yenye kuboresha afya. Ikiwa unasafiri mbali zaidi, huenda ikafaa kutumia usafiri wa umma. Majiji mengi yanajaribu kuboresha usafiri wa basi au tramu ili kushawishi watu waache magari yao nyumbani. Huenda kutumia huduma hizo kukasaidia kupunguza gharama. Ingawa unaweza kuwa umetumia gari lako sehemu fulani ya safari yako, unaweza kutumia usafiri wa umma kuingia katikati ya jiji.

Ikiwa ni lazima kutumia gari, fikiria ikiwa unaweza kuwabeba watu wengine. Hiyo ni njia moja inayofaa zaidi ya kupunguza msongamano wa magari asubuhi na jioni. Nchini Marekani, asilimia 88 ya wasafiri wote hutumia magari ya kibinafsi, na karibu asilimia 66 kati yao husafiri peke yao. Ikiwa watu wengi wangekubali kusafiri pamoja wanapoelekea kazini “kufanya hivyo kungepunguza sana wakati unaopotezwa na msongamano asubuhi na jioni,” kinasema kitabu Stuck in Traffic. Isitoshe, katika maeneo mengi kuna pande za barabara zilizotengwa hasa kwa ajili ya magari yaliyo na watu wawili au zaidi. Magari yaliyo na mtu mmoja tu hayaruhusiwi kutumia upande huo.

Ikiwa unaweza kuchagua wakati wa kusafiri, jaribu kuepuka kusafiri wakati kuna msongamano mwingi. Hilo litarahisisha maisha yako na ya madereva wengine. Pia ukiegesha kwa njia inayofaa, gari lako halitazuia magari mengine. Bila shaka, hata mipango bora zaidi haiwezi kuhakikisha kwamba hutajikuta katika msongamano. Nyakati kama hizo, kuwa na mtazamo unaofaa kunaweza kupunguza kukatishwa tamaa.—Ona sanduku.

Ni wazi, ikiwa unaishi katika jiji kubwa, ni lazima utakabiliana na msongamano wa magari. Hata hivyo, kwa kuchukua hatua fulani, kuonyesha fadhili na kuwa na subira kuelekea madereva wengine, utajifunza kukabiliana na msongamano wa magari.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]

Kuwa Mtulivu Kunapokuwa na Msongamano wa Magari

Jaime, dereva wa teksi huko Madrid, Hispania, amekabiliana na msongamano wa magari kwa zaidi ya miaka 30. Yafuatayo ni maelezo yake kuhusu anavyodumisha utulivu chini ya hali zenye kuudhi:

▪ Mimi huhakikisha nina kitu cha kusoma. Hivyo, kunapokuwa na msongamano wa magari, sikati tamaa.

▪ Magari yanaposonga polepole sana, mimi husikiliza habari kwenye redio au kaseti ya Biblia. Hivyo mimi huwa na mambo mengine akilini badala tu ya kufikiria jinsi magari yalivyosongamana.

▪ Mimi sipigi honi kamwe. Kufanya hivyo ni kuwasumbua wengine na hakusaidii chochote. Kwa kuwaonyesha wengine fadhili, mimi huepuka mfadhaiko na kuwasaidia wengine kufanya hivyo.

▪ Mimi hujaribu kutulia ninapokutana na madereva wakali, nami huwapa nafasi ya kutosha. Subira ni jambo la maana sana.

▪ Ingawa mimi hutafuta barabara zisizo na msongamano, mimi huwajulisha wateja kwamba huenda kutakuwa na mabadiliko katika ratiba yao kwa sababu ya msongamano. Huwezi kuwa na hakika kwamba utafika kwa wakati ikiwa unatumia gari jijini.