Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Svalbard—Eneo Lenye Pwani Baridi

Svalbard—Eneo Lenye Pwani Baridi

Svalbard—Eneo Lenye Pwani Baridi

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI NORWAY

TUNASAFIRI kwa ndege katikati ya mawingu mazito na hivyo hatuwezi kuona chochote. Kwa ghafula, ndege yetu inatoka kwenye mawingu na chini yetu tunaona eneo la Aktiki lililofunikwa kwa theluji. Mandhari hiyo inapendeza kama nini! Tunapotazama mabamba ya barafu, mikono ya bahari, na milima iliyofunikwa kwa theluji, tunastaajabu. Ni kana kwamba eneo hilo lisilo na mimea lililofunikwa kwa theluji na barafu halina mwisho. Tumekuja kutembelea Svalbard, visiwa vilivyo karibu na Ncha ya Kaskazini, kati ya digrii 74 za latitudo na digrii 81 kuelekea kaskazini!

Jina Svalbard, linalomaanisha “Pwani Baridi,” lilionekana kwa mara ya kwanza mnamo 1194 katika maandishi ya Waiceland. Lakini eneo hilo “liligunduliwa” miaka 400 baadaye, mnamo 1596 na hivyo likajulikana ulimwenguni pote. Mwaka huo kikundi cha wagunduzi Waholanzi kikiongozwa na Willem Barents kilikuwa kikisafiri kwa meli kuelekea kaskazini wakati ambapo mmoja kati yao aliona kwenye upeo wa macho yake eneo lisilojulikana, safu ya milima yenye ncha. Wagunduzi hao walikuwa kwenye eneo la kaskazini-magharibi mwa Svalbard, naye Barents aliita eneo hilo “Spitsbergen” jina linalomaanisha “Milima Iliyochongoka.” Hilo ndilo jina la kisiwa kikubwa zaidi kati ya visiwa hivyo. Ugunduzi wa Barents ulianzisha kipindi chenye utendaji mwingi huko Svalbard. Utendaji huo ulitia ndani kuvua nyangumi, sili, kuwakamata wanyama, kugundua maeneo mapya, kuchimba makaa ya mawe, kufanya utafiti wa kisayansi, na utalii. Kwa miaka mingi, nchi kadhaa zimeshiriki katika utendaji huo, lakini kuanzia mwaka wa 1925 visiwa hivyo vimekuwa chini ya utawala wa Norway.

Udongo Ulioganda na Mwanga wa Ajabu

Ndege yetu inashuka kupitia eneo linaloitwa Ice Fjord na kutua katika Uwanja wa Ndege wa Svalbard. Tunapanda gari tulilokodisha na kuelekea Longyearbyen, mji unaoitwa kwa jina la mfanyabiashara mkubwa Mmarekani, John M. Longyear, aliyefungua migodi ya kwanza ya makaa ya mawe katika eneo hilo mnamo 1906. Longyearbyen ndio mji mkubwa zaidi huko Svalbard, wenye idadi ya watu karibu 2,000. Katika eneo hilo ambalo mazingira yake ya kiasili hayajabadilika, tunakuta mji wa kisasa wenye vitu vya kawaida kama duka kubwa, posta, benki, maktaba, shule ya watoto, hoteli, mikahawa, hospitali, na hata wana gazeti lao. Kwa kuwa uko zaidi ya digrii 78 kuelekea upande wa kaskazini, Longyearbyen ndio mji ulio kaskazini zaidi duniani wenye watu wengi hivyo.

Tunakodi mahali pa kulala ambapo zamani palikuwa ni makao ya wachimbaji wa makaa ya mawe. Vyumba vyake vimejengwa kuelekeana na Longyearbyen, na unaweza kuona mandhari ya mlima wenye kuvutia unaoitwa Hiorthfjellet. Ni Oktoba (Mwezi wa 10) na milima imefunikwa kwa theluji. Eneo la chini la bonde hilo halina theluji, lakini udongo umeganda. Katika eneo hilo udongo huwa umeganda daima. Ni udongo wa juu tu ambao huachana kwa muda mfupi wakati wa kiangazi. Lakini kwa sababu ya upepo na mikondo ya bahari, hali ya hewa ni afadhali katika eneo hilo kuliko maeneo mengine ya latitudo hiyo. Kutoka mahali tunapoishi, tunaweza kuona jua linapotokea kwenye milima, huku bonde likiwa na rangi ya bluu. Kati ya Oktoba tarehe 26 na Februari (Mwezi wa 2) tarehe 16, jua halichomozi hata kidogo juu ya eneo la Longyearbyen. Lakini mara nyingi kunakuwa na mwangaza wa ajabu usiku wakati wa majira ya baridi kali. Miezi fulani baadaye kunakuwa na mwangaza wa jua usiku wa manane huko Svalbard, na katika Longyearbyen hilo hutukia kutoka Aprili (Mwezi wa 4) tarehe 20 hadi Agosti (Mwezi wa 8) tarehe 23.

Mimea na Wanyama

Kuna baridi ya nyuzi 8 Selsiasi chini ya sufuri na upepo mkali; lakini hakuna mawingu. Tuko tayari kwenda kutalii. Mwenye kututembeza anatupeleka hadi kwenye Mlima Sarkofagen na kututeremsha kwenye mwamba wa barafu wa Longyearbreen. Tunapopanda milima hiyo iliyofunikwa na theluji, anatuambia kuhusu maua maridadi ambayo hukua katika eneo hilo katika miezi yenye joto zaidi. Kwa kweli, kuna mimea mingi sana huko Svalbard kwani kuna aina 170 za mimea inayotoa maua. Maua ya asili ya eneo hilo ni kama vile ua lenye rangi nyeupe au manjano linaloitwa mpopi wa Svalbard na ua la zambarau lenye harufu nzuri liitwalo saxifrage.

Tunapopanda juu zaidi kwenye mlima huo, tunakuta alama za miguu za ndege anayeitwa ptarmigan wa Svalbard, ambaye ndiye ndege pekee wa kiasili huko Svalbard. Ndege wengine wote, kama vile Brünnich’s guillemot, auk mdogo, shakwe wa aina fulani, na chamchanga wa rangi ya zambarau, huhamahama. Ndege wa pekee sana ni membe wa aktiki. Membe wengi husafiri hadi upande ule mwingine wa dunia, yaani hadi Antaktika.

Pia tunaona alama za miguu za mbweha wa aktiki. Mnyama huyo mjanja hula mizoga, lakini pia yeye hula ndege wachanga na mayai. Mbweha huyo ni mmoja kati ya wanyama wa asili wa Svalbard. Mnyama mwingine wa asili ni mbawala wa Svalbard. Mara kadhaa tulimwona mbawala huyo akiwa karibu. Alitutazama kwa utulivu na kuturuhusu tumkaribie kwa kiasi fulani na tumpige picha kabla ya kukimbia. Mbawala huyo ana miguu mifupi na manyoya mengi. Kabla ya majira ya baridi kali yeye huongeza mafuta. Mafuta hayo ya ziada ni akiba ya chakula ambacho anahitaji kwa ajili ya majira ya baridi kali.

Dububarafu, ambaye anasemekana kuwa mfalme wa Aktiki, huonwa na wengi kuwa mnyama wa baharini kwa kuwa yeye huishi muda mrefu juu ya barafu ya bahari akiwinda sili. Lakini unaweza kukutana na dubu hao wakitembea mahali popote huko Svalbard. Anayetuongoza anatumaini kwamba hatutakutana na dubu yeyote. Dububarafu anaweza kuwa mkali sana, kwa hiyo anayetutembeza amebeba bunduki. Tangu 1973 kuwinda dububarafu kulipigwa marufuku, na lazima uchunguzi ufanywe iwapo mtu amemuua dububarafu. Ingawa sasa kuna dububarafu wengi huko Svalbard, bado kuna wasiwasi mwingi kama wataendelea kuwapo kwa muda mrefu. Eneo la Aktiki linaweza kuonekana kuwa jeupe na lisilo na uchafu, lakini mazingira yake yamechafuliwa sana na sumu fulani zinazoitwa PCB. Sumu hiyo hujazana ndani ya dububarafu, kwani wao ndio wawindaji wakuu katika eneo hilo, na hilo huathiri uwezo wao wa kuzaliana.

Tunapofika kwenye kilele cha Mlima Sarkofagen tunaona kwa mbali mandhari nzuri sana ya vilele vyeupe. Upande wa kusini-magharibi, tunaona mlima wenye umbo la mviringo unaoitwa Nordenskiöldfjellet, uking’aa kwenye jua. Tunaona Longyearbyen ikiwa kule chini; juu yetu tunaona anga la bluu la Aktiki. Kwa kweli tunajihisi kama tuko juu ya dunia. Tunakula mkate na kuuteremsha kwa maji ya zabibu yaliyotiwa sukari na maji moto, kinywaji ambacho hupendwa na watu wengi ambao hupanda milima. Tunapomaliza tunahisi tumeburudika na tunakuwa tayari kushuka mlima kupitia mwamba wa barafu wa Longyearbreen.

Uchimbaji wa Makaa ya Mawe na Wanyama Walio Hatarini

Tunafurahi pia tunapotembelea mgodi fulani wa makaa ya mawe. Hapo zamani, anayetutembeza alikuwa mchimba-migodi, kwa hiyo anatuonyesha Mgodi wa 3 ulio nje kidogo ya Longyearbyen. Tukiwa tumevaa ovaroli, na kofia ngumu zenye taa, tunaingia katika mgodi ulio ndani ya mlima. Tunaambiwa kwamba kuchimba makaa ya mawe kumekuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Svalbard tangu miaka ya 1900. Kwa miaka mingi, wachimbaji walikuwa na hali ngumu sana. Mara nyingi walitambaa kwa mikono na miguu kupitia vijia vilivyofanyizwa kati ya mabamba ya makaa ya mawe. Katika sehemu nyingine vijia hivyo vilikuwa na kimo cha sentimita 70. Tulipata nafasi ya kupitia vijia hivyo na kusema kweli hatukutamani kazi ambayo wachimba-migodi walikuwa wakifanya. Kazi yao ilikuwa ngumu sana, hewa ilikuwa imejaa vumbi ya makaa ya mawe, kulikuwa na kelele nyingi, na kulikuwa na hatari za milipuko na maporomoko ya ardhi kutokea wakati wowote. Sasa mbinu za kisasa zaidi zinatumiwa. Bado uchimbuaji wa makaa ya mawe ni muhimu kwa uchumi wa Svalbard, lakini kwa miaka kadhaa ambayo imepita utalii umekuwa muhimu zaidi.

Kwa wakati fulani, hatari zinazokabili wanyama wa mwituni wa eneo la Aktiki hazikufikiriwa sana. Kulikuwa na wakati ambapo watu hawakuzuiwa kuwinda nyangumi, sili wenye pembe, mbawala, dububarafu, na wanyama wengine na hivyo jamii fulani zikabili hatari ya kutoweka huko Svalbard. Hata hivyo, kupiga marufuku uwindaji kumesaidia kuongezeka kwa jamii fulani za wanyama waliokuwa wakikabili hatari ya kutoweka.

Mahali Panapowafaa Wataalamu

Svalbard imesemekana kuwa “paradiso ya wataalamu wa kuchunguza mawe.” Kwa kuwa kuna mimea michache, sehemu kubwa ya eneo hilo imejaa mawe. Tunaona muundo wa mawe katika milima, ambao una matabaka yanayoonekana waziwazi yanayofanana na keki yenye safu. Eneo hilo lina mawe ya zamani. Mengine yalitokana na mchanga na matope, nayo mengine yakatokana na mabaki ya wanyama na mimea. Kwa karne nyingi, mimea na wanyama waliokufa walifunikwa kwa matope na kuhifadhiwa. Kwa kweli, kuna mabaki ya wanyama na mimea kutoka karne zote.

Katika jumba la makumbusho la Svalbard, tunaona mabaki ya mimea na wanyama inayoonyesha kwamba hali ya hewa katika visiwa hivyo ilikuwa yenye joto kuliko ilivyo leo. Katika sehemu fulani za Svalbard, mabamba ya makaa ya mawe yana upana wa mita 5! Katika mabamba hayo, mabaki ya miti mbalimbali yamepatikana. Kupatikana kwa alama za miguu ya dinosa ambaye hula mimea ni uthibitisho mwingine kwamba hapo awali hali ya hewa ilikuwa yenye joto na kulikuwa na mimea mingi.

Kwa nini kuna badiliko kubwa hivyo katika hali ya hewa? Tunamwuliza Torfinn Kjaernet, mtaalamu wa kuchunguza mawe, ambaye anawakilisha Halmashauri ya Uchimbaji Migodi huko Longyearbyen. Anatuambia kwamba wataalamu wengi wa kuchunguza mawe wanafikiri kwamba sababu kuu ni kusonga kwa miamba ya dunia. Wataalamu hao wanasema kuwa visiwa vya Svalbard viko juu ya mwamba wa dunia ambao umekuwa ukisonga kwa muda mrefu sana kuelekea kaskazini, na huenda ulitoka kusini karibu na ikweta. Kulingana na picha za setilaiti za kisasa, bado visiwa vya Svalbard vinasonga kuelekea kaskazini-mashariki kwa sentimita kadhaa kila mwaka.

Ndege yetu inapoondoka Svalbard, tunahisi kwamba safari yetu imetupa mengi ya kutafakari. Eneo kubwa la Aktiki, wanyama wanaoishi humo, na mimea mbalimbali hutufanya tufikiri kuhusu unamna-namna wa uumbaji, hali duni ya wanadamu, na jinsi wanadamu wametunza mali ya asili waliyokabidhiwa. Tunapoelekea kusini, tunaona kwa mara ya mwisho eneo hilo lenye pwani baridi, ambako ncha za milima zilizofunikwa kwa theluji zinajitokeza juu ya mawingu na kung’aa kwa rangi hafifu ya waridi zinapopigwa na jua la alasiri.

[Ramani katika ukurasa wa 24]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Ncha ya Kaskazini

GREENLAND

SVALBARD

Longyearbyen

75°K

ICELAND

NORWAY

60°K

URUSI

[Picha katika ukurasa wa 25]

Mji wa Longyearbyen

[Picha katika ukurasa wa 25]

Mimea mingi inayotokeza maua, kama vile ua la zambarau linaloitwa “saxifrage,” huendelea kuishi katika hali mbaya ya hewa ya Aktiki

[Hisani]

Knut Erik Weman

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mnyama wa Svalbard anayeitwa “ptarmigan,” na mbawala wa Svalbard

[Hisani]

Knut Erik Weman