Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kulingana na uchunguzi mmoja, “watu wanaozungumza kwenye simu za mkononi wanapoendesha magari, hata ikiwa wanatumia vifaa vya kuzungumza bila kushika simu, hawana uwezo kamili wa kudhibiti gari kama tu dereva anayeendesha akiwa amelewa.”—SHIRIKA LA HABARI LA REUTERS, MAREKANI.

Katika miezi mitano ya kwanza ya mwaka wa 2006, kulikuwa na visa 30,200 vya wizi wa kutumia silaha kwenye mabasi ya umma huko Guatemala City. Madereva 14 au wasaidizi wao na abiria 10 waliuawa. —PRENSA LIBRE, GUATEMALA.

Kati ya nchi 124 zilizoshiriki katika utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Ulimwenguni kuhusu jinsi damu hukusanywa na kupimwa, nchi 56 “hazikupima damu yote iliyokusanywa kuona kama ina virusi vya UKIMWI, mchochota wa ini aina ya B na C, na kaswende.”—SHIRIKA LA AFYA ULIMWENGUNI, USWISI.

Idadi ya Waaustralia ambao wanaishi pamoja bila kufunga ndoa iliongezeka kutoka asilimia 5 hivi miaka ya 1960 hadi asilimia zaidi ya 70 mwaka wa 2003.—CHUO KIKUU CHA MELBOURNE, AUSTRALIA.

Kisukari—Ugonjwa Unaozidi Kuongezeka

Gazeti The New York Times linasema kwamba takwimu zilizotolewa na Shirika la Kimataifa la Ugonjwa wa Kisukari, zinaonyesha kwamba katika miaka 20 iliyopita, idadi ya watu ulimwenguni walio na ugonjwa wa kisukari imeongezeka kutoka milioni 30 hadi milioni 230. Kati ya nchi kumi zenye idadi kubwa ya watu wenye ugonjwa huo, saba ni nchi zinazoendelea. “Kisukari ni mojawapo ya matatizo makubwa ya afya ambayo yamekumba ulimwengu,” anasema Dakt. Martin Silink, msimamizi wa shirika hilo. Ripoti hiyo inasema kwamba “katika nchi maskini zaidi ulimwenguni, watu hawaishi muda mrefu baada ya kupata ugonjwa huo.”

Reli Iliyo Juu Kuliko Zote Duniani

Reli iliyo juu kuliko zote duniani, yenye urefu wa kilomita 4,000 hivi ambayo inaunganisha Jiji la Beijing na Lhasa, mji mkuu wa Tibet, ilizinduliwa Julai (Mwezi wa 7) 2006. Gazeti The New York Times linasema kwamba “reli hiyo ni uhandisi wa hali ya juu kwani inapita kwenye udongo ulioganda, na iko mita zaidi ya 4,800 juu ya usawa wa bahari.” Miongoni mwa changamoto ambazo wahandisi walihitaji kuzitatua ilikuwa ni jinsi ya kuufanya msingi ambao reli itatandikwa, uwe umeganda kwa mwaka mzima ili kuuimarisha. Kwa sababu reli hiyo iko kwenye mwinuko, ni lazima mabehewa yajazwe hewa. Mabehewa hayo pia yana vifaa vya hewa ya oksijeni kwa ajili ya kila abiria.

“Wanafunzi Mizuka”

Kati ya asilimia 10 hadi 20 ya wanafunzi walioandikishwa kusomea fasihi katika chuo kikuu kimoja cha Ufaransa “hawaendi darasani,” linataarifu gazeti Le Figaro. Wengine wamejiunga na chuo hicho ili kufaidika na huduma ambazo wanafunzi hupata kama vile huduma za kijamii, kupunguziwa nauli za ndege na usafiri wa umma, ada ya hoteli na filamu. Ili kupata faida hizo, “wanafunzi mizuka” hujiandikisha kwa ajili ya masomo ya lugha kama, Kibelarusi, Kifini, au Kiswahili, ambayo ni wanafunzi wachache sana kati ya wale waliotarajiwa hujiandikisha. Ulaghai kama huo kwenye usajili wa wanafunzi ni jambo la kawaida kwa sababu wanaohudhuria darasani hawahesabiwi. Ripoti hiyo inasema kwamba “wanafunzi” hao hujisajili kwenye mtandao na baada ya muda mfupi hutumiwa vitambulisho vyao vya uanafunzi.

“Lilikuwa Bado Halijagunduliwa”

Wanasayansi wa Israel wanaamini kwamba wamegundua aina mpya nane za wadudu wasio na uti wa mgongo kwenye pango ambalo “lilikuwa bado halijagunduliwa” kwa karne nyingi, linasema gazeti The Jerusalem Post. Wachimbuzi waliokuwa wakifanya kazi katika eneo la kuchimba mawe, waligundua shimo dogo lililoelekea kwenye pango lenye urefu wa kilomita 2.5, ambalo lilikuwa na ziwa la chini ya ardhi. Wadudu hao waliogunduliwa ambao baadhi yao wanafanana na nge, walitia ndani krasteshia wawili wa maji chumvi, wawili wa maji baridi, na viumbe wanne wa nchi kavu.