Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Chavua Vumbi Linaloendeleza Uhai

Chavua Vumbi Linaloendeleza Uhai

Chavua Vumbi Linaloendeleza Uhai

MAJIRA ya kuchipua yanapofika, nyuki huanza kufanya kazi nayo hewa hujawa na chavua. Kwa watu walio na mizio, chavua ni adui. Lakini kabla ya kukata kauli kwamba chavua ni kitu cha kuchukiza, tunapaswa kuzingatia umuhimu wa vumbi hilo la pekee. Huenda tukashangaa kujua jinsi ambavyo maisha yetu yanategemea chavua.

Chavua ni nini hasa? Kitabu The World Book Encyclopedia kinaeleza: “Chavua ina punje ndogo ambazo hutokezwa na viungo vya uzazi vya kiume katika mimea inayotokeza maua na sonobari.” Kwa ufupi, mimea hutokeza chavua ili iweze kuzaa. Kama tunavyojua, kwa wanadamu, lazima mbegu ya uzazi ya kike itungishwe na mbegu ya kiume ili mtoto atokezwe. Vivyo hivyo, kiungo cha uzazi cha kike katika ua (pistili) kinahitaji chavua kutoka kwenye kiungo cha kiume (stameni) ili kitungishwe na kutokeza matunda. *

Chembe za chavua ni ndogo sana hivi kwamba hatuwezi kuziona kwa macho; hata hivyo zinaweza kuonekana kwa hadubini. Kwa kweli, mtu anapozitazama anaweza kuona kwamba kila aina ya chavua ina ukubwa na umbo lake la kipekee. Kwa kuwa chavua haiwezi kuoza, wanasayansi huchunguza mara nyingi sifa za kipekee za chembe za chavua wanazogundua. Hivyo, wanaweza kutambua mimea ambayo watu walikuza karne nyingi zilizopita. Jambo muhimu hata zaidi ni kwamba sifa za kipekee za kila chavua zinawezesha maua kutambua chavua kutoka kwa maua mengine ya jamii yake.

Jinsi Chavua Zinavyosafiri

Mimea mingi hutegemea hewa kusafirisha chavua wakati sonobari au vishada vilivyoibeba vinapopigwa na upepo. Pia maji hutumika kusafirisha chavua ya mimea fulani ya majini. Kwa kuwa uchavushaji wa kutumia upepo hautegemeki, miti na mimea inayotegemea mbinu hiyo hutokeza kiasi kikubwa sana cha chavua. * Watu ambao huathiriwa na homa inayosababishwa na vumbi, husumbuka sana kipindi hicho ambapo chavua husambaa kwa wingi.

Ingawa upepo unasaidia sana kuchavusha aina mbalimbali za miti na nyasi, mimea inayotokeza maua ambayo haikui kwa wingi mahali pamoja inahitaji mbinu bora zaidi za usafirishaji. Chavua za mimea kama hiyo husafirishwaje hadi kwenye mimea mingine kama hiyo iliyo mbali sana? Kwa kutumia mbinu za usafirishaji wa hali ya juu zinazotolewa na popo, ndege, na wadudu! Lakini hawasafirishi tu chavua kutoka ua moja hadi lingine bila malipo.

Maua huwapa viumbe hao nekta, umajimaji mtamu ambao wao hufurahia sana. Wanapojaribu kufyonza nekta hiyo, chavua hunasa kwenye miili yao. Wakitafuta kuonja tena nekta kutoka kwenye ua lingine, wao husafirisha chavua kwenye ua hilo.

Wadudu ndio hufanya kazi kubwa zaidi ya kuchavusha, hasa katika maeneo yenye joto. Wao hutembelea maua mengi kila siku ili kula nekta na chavua. * “Huenda jambo muhimu zaidi ambalo wadudu huchangia katika afya na hali njema ya wanadamu,” anaeleza Profesa May Berenbaum, “ni lile ambalo halitambuliwi mara nyingi, yaani, uchavushaji.” Miti ya matunda huwa na maua ambayo hutegemea chavua inayosafirishwa kutoka kwenye miti mingine ili kutoa mazao mazuri. Hivyo, unaweza kuona jinsi usafirishaji wa chavua ni muhimu kwa ajili ya hali yetu njema.

Jinsi Wachavushaji Wanavyovutiwa

Lazima maua yawavutie wachavushaji na vilevile kuwalisha. Maua hufanyaje hivyo? Yanaweza kuwaandalia mahali penye joto pa kupumzikia kwenye jua. Pia, yanaweza kuwavutia kwa kutokeza harufu na rangi nzuri. Vilevile, maua mengi hutoa miongozo kupitia madoadoa maridadi au mistari kuwaelekeza wachavushaji kwenye nekta.

Maua hutumia njia mbalimbali kuwavutia wachavushaji. Maua fulani hutoa harufu ya kuoza ili kuvutia nzi. Mengine hutumia ujanja ili kuhakikisha yamechavushwa vizuri. Kwa mfano, ua fulani la jamii ya okidi linalofanana sana na nyuki huwavutia kwa hila nyuki wanaotafuta wachumba. Maua mengine hunasa wadudu na kuwaachilia tu baada ya wadudu hao kuyachavusha kikamili. “Hakuna jambo lingine katika jamii ya miti lililo tata, linalohitaji kufanywa kwa usahihi au ustadi kabisa kuliko lile la kuhakikisha kwamba maua yamechavushwa,” anaandika mtaalamu wa mimea Malcolm Wilkins.

Ikiwa Muumba hangefanya mimea iwe maridadi ili iweze kuchavushwa, mamilioni ya mimea isingeweza kutokeza mazao. Akizungumza kuhusu matokeo ya utendaji huo wa ajabu, Yesu alisema hivi: “Jifunzeni kwa mayungiyungi ya shamba, jinsi yanavyokua; hayafanyi kazi, wala hayasokoti; lakini ninawaambia ninyi kwamba hata Sulemani katika utukufu wake wote hakupambwa kama moja la haya.”—Mathayo 6:25, 28, 29.

Kwa sababu ya uchavushaji, mimea hunawiri na pia kutokeza chakula ambacho kinategemeza uhai wetu. Ni kweli kwamba chavua inaweza kuwatatiza watu fulani, lakini sote tunapaswa kuwashukuru wachavushaji ambao wanafanya kazi kwa bidii kusambaza vumbi hili linaloendeleza uhai. Mavuno mazuri hutegemea sana utendaji huo wa kiasili ambao unaonyesha wazi kazi za ajabu za Muumba wetu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Kutungishwa kunaweza kuwa kupitia mchavusho tambuko (yaani, chavua inatolewa kwenye mmea mwingine) au kupitia mchavusho pweke (yaani, chavua inatolewa kwenye mmea uleule). Hata hivyo, mchavusho tambuko hutokeza unamna-namna wa mimea yenye afya na nguvu zaidi.

^ fu. 6 Kwa mfano, huenda kishada kimoja cha mti wa mbetula kikatokeza zaidi ya chembe milioni tano za chavua, na mbetula wa kawaida unaweza kuwa na maelfu kadhaa ya vishada.

^ fu. 9 Ili kutokeza kilo moja ya asali, nyuki wanahitaji kufunga safari milioni kumi hivi kwenda kwenye maua mbalimbali.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Wachavushaji

NZI NA MBAWAKAWA

Hao ni baadhi ya wachavushaji wakuu ambao hawasifiwi. Kama wewe hufurahia kula chokoleti unapaswa kumthamini nzi mdogo ambaye hufanya kazi ya maana ya kuchavusha maua ya mkakao.

POPO NA OPOSSUM

Baadhi ya miti mikubwa sana duniani, kama vile mti uitwao kapok na mbuyu, inawategemea sana popo kwa ajili ya uchavushaji. Popo wa matunda hula nekta na vilevile wao hula matunda na kusambaza mbegu zake, hivyo wao hufanya kazi maradufu. Nchini Australia wanyama wadogo wanaoitwa opossum, wasiokuwa na kondo na walio na kifuko cha kubebea wachanga wao, hutafuta maua ili kula nekta. Wakati huo, miili yao yenye manyoya hubeba chavua kutoka ua moja hadi lingine.

VIPEPEO NA NONDO

Chakula cha wadudu hawa maridadi hasa ni nekta, nao hubeba chavua kutoka ua moja hadi lingine. Okidi fulani maridadi hutegemea hasa nondo ili ziweze kuchavushwa.

CHOZI NA HUMMINGBIRD

Ndege hawa maridadi hurukaruka kutoka ua moja hadi lingine, wakila nekta. Chavua hunasa kwenye manyoya yaliyo kichwani na kifuani mwao.

NYUKI NA NYIGU

Miili yenye manyoya-manyoya ya nyuki hunaswa na chavua haraka kama tu miwani inavyopata vumbi, na ndiyo sababu nyuki ni wachavushaji bora. Nyuki mmoja tu mwenye manyoya anaweza kubeba chembe 15,000 za chavua. Mashamba ya New Zealand ya klova sasa yananawiri sana tangu kuingizwa kwa nyuki hao wenye manyoya kutoka Uingereza katika karne ya 19. Mashamba hayo huandaa chakula kinachohitajika hasa kwa ajili ya mifugo ya nchi hiyo.

Nyuki wa asali ndiye mchavushaji muhimu zaidi ulimwenguni. Kwa kawaida nyuki huyo hujishughulisha tu na aina moja ya ua linalopatikana kwa wingi karibu na mzinga wake. Christopher O’Toole, mtaalamu wa wadudu anakadiria kwamba “asilimia 30 hivi ya chakula chote cha wanadamu hutokezwa moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwa kutegemea uchavushaji wa nyuki.” Nyuki wanahitajika ili kuchavusha mimea kama vile lozi, matofaa, plamu, cheri, na kiwi. Wakulima huwalipa wafugaji wa nyuki kwa ajili ya faida ambayo kila mzinga hutoa.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Okidi ambayo inafanana na nyuki