Kutoka Misri Hadi Majiji Mengine Ulimwenguni
Kutoka Misri Hadi Majiji Mengine Ulimwenguni
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA
“IMEHAMISHWA kutoka nchi yake ya asili,” linasema gazeti la Italia Archeo, “nayo imekuwa alama ya wazi ya ustaarabu ulioitokeza.” Mingi kati ya minara hiyo ilitolewa Misri zamani na kupelekwa Istanbul, London, Paris, Roma, na New York. Wageni wanaotembelea jiji la Roma wanaweza kuona kwamba mengi ya maeneo yake maarufu yana minara hiyo.
Minara hiyo mirefu inayojulikana kama obelisk, ina umbo la mraba na sehemu yake ya juu imechongoka kama piramidi. Mnara wa zamani zaidi una miaka 4,000 hivi. Mnara wa karibuni zaidi una miaka 2,000 hivi.
Kwa kawaida, obelisk ni jiwe kubwa jekundu la matale lililochimbuliwa na Wamisri wa kale na kusimamishwa mbele ya makaburi na mahekalu. Mengi ni marefu sana. Mnara mrefu zaidi kati ya hiyo una urefu wa mita 32 na uzito wa tani 455 hivi, nao umesimamishwa kwenye uwanja mmoja huko Roma. Mingi imenakshiwa kwa picha zilizo na ujumbe mbalimbali.
Minara hiyo ilitengenezwa ili kumtukuza mungu-jua aliyeitwa Ra. Ilisimamishwa ili kumshukuru kwa ajili ya ulinzi na ushindi aliowapa watawala wa Misri na vilevile kuomba kibali chake. Inasemekana kwamba walioisimamisha minara hiyo waliiga umbo la piramidi. Inawakilisha miale ya jua inayoshuka ili kupasha joto na kuangaza dunia.
Isitoshe, minara hiyo ilitumiwa kuwatukuza Mafarao. Maandishi yaliyo kwenye minara hiyo yanawafafanua watawala mbalimbali wa Misri kwa maneno kama vile “apendwaye na Ra” au “mrembo . . . kama Atum,” ambaye alikuwa mungu wa jua wakati wa machweo. Mnara mmoja unasema hivi kuhusu uwezo wa kivita wa Farao mmoja: “Nguvu zake ni kama zile za Monthu [mungu wa vita], fahali anayekanyaga nchi za kigeni na kuua waasi.”
Minara ya kwanza ilisimamishwa huko Misri kwenye jiji liitwalo Junu (katika Biblia linaitwa Oni), jina linalodhaniwa kuwa linamaanisha “Jiji la Nguzo,” labda kwa kurejelea minara yenyewe. Wagiriki waliliita Junu Heliopolis, kumaanisha “Jiji la Jua,” kwa kuwa lilikuwa kituo kikuu cha ibada ya jua nchini Misri. Jina la Kigiriki Heliopolis, linapatana na jina la Kiebrania Beth-shemeshi, linalomaanisha “Nyumba ya Jua.”
Kitabu cha unabii cha Biblia cha Yeremia, kinataja kuhusu kuvunjwa kwa “nguzo za Beth-shemeshi, lililo katika nchi ya Misri.” Huenda hilo likarejelea minara ya Heliopolis. Mungu alishutumu ibada ya sanamu ambayo minara hiyo iliwakilisha.—Yeremia 43:10-13.
Uchimbuzi na Usafirishaji
Mnara mkubwa zaidi ambao bado upo unaonyesha jinsi minara hiyo ilivyojengwa. Mnara huo uliachwa karibu na Aswân, Misri, ambako ulikuwa ukichimbuliwa. Baada ya kuchagua mwamba unaofaa kutengeneza mnara na kuusawazisha, wafanyakazi walichimba mitaro kuuzunguka. Walichimba vijia chini yake na kuvijaza nguzo za miti ya kuvitegemeza, hadi sehemu ya chini ya mwamba ichimbuliwe. Mnara huo mkubwa ambao una tani 1,170 hivi ni mzito zaidi kuliko jiwe lingine lolote kuwahi kuchimbwa na Wamisri wa kale. Mnara huo ulipaswa kukokotwa hadi Mto Nile na kusafirishwa kwa mashua kubwa hadi mahali ambapo ungesimamishwa.
Kile kilichotukia ni kwamba, mnara huo ulioko Aswân uliachwa wafanyakazi walipotambua ulikuwa na ufa ambao haungeweza kurekebishwa. Kama ungekamilishwa, ungekuwa na urefu wa mita 42, na sehemu ya chini ingekuwa na mita 4 za mraba. Bado haijulikani jinsi minara hiyo ilivyoinuliwa na kusimamishwa.
Kutoka Misri Hadi Roma
Katika mwaka wa 30 K.W.K., Misri ikawa mkoa wa Roma. Maliki kadhaa Waroma walitaka kupamba mji wao mkuu kwa nguzo zenye umashuhuri mkubwa, hivyo obelisk 50 zilipelekwa Roma. Ili kuhamisha minara hiyo, meli nyingi kubwa ziliundwa. Minara hiyo ilipofikishwa Roma, iliendelea kuhusianishwa na ibada ya jua.
Milki ya Roma ilipoanguka, Roma iliporwa. Minara mingi iliangushwa na kusahauliwa. Hata hivyo, mapapa kadhaa walitaka kuiinua tena minara iliyokuwa katika magofu ya jiji hilo la kale. Kanisa Katoliki limekubali kwamba minara hiyo “ilijengwa na mfalme wa Misri hasa kwa ajili ya Jua” na kwamba zamani “ilileta utukufu usiofaa kwa mahekalu ya kipagani yenye kukufuru.”
Mnara wa kwanza ulipokuwa ukisimamishwa wakati wa utawala wa Papa Sixtus wa Tano (1585-1590) kulikuwa na sala na desturi za kufukuza pepo na kutoa baraka, kutia ndani kumwaga maji matakatifu na kufukiza uvumba. “Ninafukuza mapepo yote kutoka kwako,” akaimba askofu mmoja akiwa mbele ya mnara ulioko Vatikani, “ili ubebe Msalaba mtakatifu na uondolewe uchafu wa kipagani na mashambulizi ya uovu wa kidini.”
Hivyo, mtalii anapotazama minara iliyoko Roma leo, anaweza kuwazia ustadi uliohusika ili kuchimbua, kusafirisha, na kuisimamisha. Anaweza pia kustaajabu kwamba minara iliyotumiwa katika ibada ya jua sasa inatumiwa kurembesha jiji la mapapa. Huo ni upotovu ulioje!
[Picha katika ukurasa wa 15]
Luxor, Misri
[Picha katika ukurasa wa 15]
Roma
[Picha katika ukurasa wa 15]
New York
[Picha katika ukurasa wa 15]
Paris