Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Katika muda wa miaka kumi iliyopita, wakulima milioni 40 hivi nchini China wamepoteza mashamba yao kwa sababu ya kupanuka haraka kwa majiji.—CHINA DAILY, CHINA.

Ulimwenguni pote, vita 28 na mapigano mengine 11 yalitukia mnamo 2005.—VITAL SIGNS 2006-2007, TAASISI YA WORLDWATCH.

Kikundi fulani kutoka Taasisi ya Teknolojia ya Tokyo kimefaulu kurusha hewani ndege inayoendeshwa na mwanadamu iliyo na uzito mdogo sana wa kilo 55 na inayotumia betri za kawaida zinazoweza kutumika nyumbani. Ndege hiyo iliruka umbali wa mita 391 kwa sekunde 59.—MAINICHI DAILY NEWS, JAPANI.

Nchini Uholanzi vijana walio na umri wa miaka 12 hadi 20 hutembelea vituo fulani vinavyosemekana kuwa vya kubadilishana habari na kuwasiliana huku wakitumia kamera ya video iliyounganishwa kwenye Intaneti. “Imeripotiwa kwamba asilimia 40 ya wavulana na asilimia 57 ya wasichana wameombwa wavue nguo zao au wafanye tendo fulani la ngono mbele ya kamera ya video.”—RUTGERS NISSO GROEP, UHOLANZI.

Je, Mtu Anaweza Kuwa Mraibu wa Michezo ya Video?

“Utendaji wa ubongo wa watu ambao hucheza michezo ya kompyuta kupita kiasi ni sawa na ule wa waraibu wa kileo au wa bangi.” Ndivyo anavyosema mwanasaikolojia Ralf Thalemann, kiongozi wa kikundi cha utafiti kuhusu uraibu katika Hospitali ya Chuo Kikuu ya Charité huko Berlin, Ujerumani. Inafikiriwa kwamba msisimko unaotokana na kucheza kupita kiasi michezo ya kompyuta unaweza kusababisha kuongezeka kwa kemikali inayoitwa dopamine katika ubongo wa mchezaji, jambo ambalo hutokeza hisia ya kuwa salama ambayo mwishowe inaweza kusababisha “uraibu.” Uchunguzi mmoja unadokeza kwamba asilimia 10 ya wachezaji wa michezo ya video wanaweza kupatwa na jambo hilo.

Matajiri “Hawako Salama na Wana Shida”

Gazeti la Beijing China Daily linasema: “Mamilionea hujihisi hawako salama na wana shida.” Uchunguzi ulifanywa kati ya watu mbalimbali huko China Mashariki na China Kusini, walio na wastani wa yuan bilioni 2.2 (dola milioni 275). Watafiti ambao walichunguza “mtazamo [wa matajiri] kuelekea imani, ndoa, maisha, kazi, na pesa,” waligundua kwamba “wengi wa mamilionea hupenda na kuchukia pesa wakati uleule.” Baadhi ya waliohojiwa walisema kwamba licha ya kupata hadhi katika jamii na kupata hisi ya kutimiza jambo, “pesa imechangia sana kuwaletea shida.”

Kazi ya Shambani Ina Manufaa kwa Wagonjwa wa Akili

Zaidi ya wataalamu 100 kutoka nchi 14 walikutana huko Stavanger, Norway, ili kujifunza kuhusu utunzaji unaoitwa Kilimo kwa Afya, ambao ni mpango unaohusisha kilimo, kufundisha, na mambo ya afya. Kulingana na kituo cha utangazaji NRK, watu fulani ambao wamekuwa wagonjwa wa akili kwa miaka mingi hawahitaji tena kuwekwa hospitalini wanapoanza kufanya kazi za shambani. Kazi hiyo “husaidia kuboresha afya ya akili na mwili.” Zaidi ya mashamba 600 ya kienyeji nchini Norway hushirikiana na mradi huo wa Kilimo kwa Afya, nao hupata malipo ya ziada.

Matumizi ya Minara ya Makanisa

“Makanisa huko New England [Marekani] yamegundua jinsi ya kutatua tatizo la upungufu wa pesa: wameanza kukodisha minara ya makanisa kwa makampuni ya simu,” linasema gazeti Newsweek. Si rahisi kwa kampuni hizo kupata mahali pa kuweka minara ya antena za kurusha na kupokea ujumbe kutoka kwenye simu za mkononi kwa sababu ya masharti yaliyowekwa kwa ajili ya maeneo ya makazi, nao wakazi hawataki kuona antena zisizovutia karibu na maeneo wanamoishi. Kwa hiyo, kampuni za simu zinaficha vifaa vyao ndani ya minara ya makanisa. Msimamizi wa shirika moja anasema: “Kanisa la kwanza ambalo tuliweka antena sasa lina antena tatu, nalo linapata dola 74,000 kwa mwaka kwa matumizi ya nafasi ambayo hakuna mtu [alikuwa] akitumia.”