Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kwa nini mimi huzimia?

Kwa nini mimi huzimia?

Kwa nini mimi huzimia?

Daktari alitaka kupima shinikizo la jicho langu, na ili afanye hivyo ilikuwa ni lazima aguse mboni ya jicho langu kwa kifaa fulani. Nilijua ni nini kingetukia. Kila mara jambo hilo hutukia. Jambo hilo pia hutukia mwuguzi anaponichoma sindano ili anitoe damu. Nyakati nyingine kuzungumza kuhusu majeraha hufanya jambo hilohilo litukie. Yaani, mimi huzimia.

Ripoti moja kutoka Kanada inaonyesha kwamba asilimia 3 kati yetu huzimia tunapokuwa katika hali nilizotangulia kutaja. Ikiwa wewe hupatwa na hali kama hizo, huenda umejaribu kujizuia usizimie lakini ukashindwa. Huenda umejaribu kukimbilia chooni ili usizimie mbele ya watu. Lakini hilo si wazo zuri. Unaweza kuzimia ukiwa njiani na kujiumiza. Hali hiyo iliponisumbua mara nyingi sana niliamua kuchunguza inasababishwa na nini.

Baada ya kuzungumza na daktari mmoja na kuchunguza vitabu vichache, niligundua kwamba hali hiyo husababishwa na utendaji unaoitwa vasovagal. * Inafikiriwa kwamba wakati huo mfumo fulani wa mwili unaopaswa kudhibiti kuzunguka kwa damu huacha kufanya kazi kwa njia inayofaa, kama vile unaposimama baada ya kuketi kwa muda.

Hali fulani zinapotokea, kama vile unapoona damu au unapochunguzwa macho, misukumo isiyo ya hiari ya mfumo wako wa neva huanza kutenda kana kwamba umelala chini, ingawa kwa kweli umeketi au umesimama. Kwanza, moyo wako hupiga kwa kasi sana kwa sababu ya wasiwasi. Kisha, mapigo ya moyo wako hushuka na mishipa ya damu katika miguu hupanuka. Kwa sababu hiyo, damu huongezeka miguuni na kupungua kichwani. Ubongo wako hukosa oksijeni na hivyo wewe huzimia. Unaweza kuzuiaje jambo hilo?

Unaweza kutazama kando damu yako inapotolewa, au unaweza kujilaza chini wakati huo. Kama ilivyotajwa, unaweza kutambua dalili za utendaji huo kabla haujaanza. Kwa hiyo, kwa kawaida kuna wakati wa kuchukua hatua fulani kabla ya kuzimia. Madaktari wengi wanapendekeza ujilaze chini na kuinua miguu yako kwenye kiti au ukutani. Kufanya hivyo huzuia damu nyingi kuliko kawaida isishuke kwa wingi kuingia miguuni, na hivyo unaweza kuzuia utendaji huo usikamilike. Baada ya dakika chache tu, huenda ukaanza kujisikia vizuri.

Ikiwa habari hii itakusaidia kama ilivyonisaidia, utaweza kutambua dalili za kukufanya uzimie. Kisha unaweza kuchukua hatua haraka ili kuzuia jambo hilo.—Tumetumiwa makala hii.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 “Vasovagal” ni utendaji wa mishipa ya damu katika neva ndefu inayoitwa vagus. Neno la Kilatini vagus humaanisha “kuzurura.”

[Blabu katika ukurasa wa 28]

Kulala chini wakati wa matibabu kunaweza kukusaidia