Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mwamba Mkubwa Ajabu

Mwamba Mkubwa Ajabu

Mwamba Mkubwa Ajabu

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KANADA

KWA KARNE nyingi wavuvi na watu wanaosafiri baharini wameutumia kama alama yenye kutegemeka. Washairi, waandishi, na wasanii wameusifu. Kitabu kimoja kinafafanua mwamba huo kuwa “wa ajabu na wenye kuvutia.” Kwenye ukingo wa mashariki wa Rasi ya Gaspé katika Ghuba ya St. Lawrence, Mwamba Percé umesimama kwa fahari katika maji ya bluu yenye kung’aa ya Bahari ya Atlantiki. Mwamba huo una urefu wa mita 433 hivi, upana wa karibu mita 90, na kimo cha zaidi ya mita 88.

Wakati mmoja, wenyeji wenye ujasiri walipanda mwamba huo na kukusanya mayai kutoka kwenye viota vya ndege. Hata hivyo, ili kuhifadhi na kulinda mwamba huo na vilevile ndege wanaoishi juu yake, mnamo 1985 serikali ya Quebec ilitangaza Mwamba Percé na Kisiwa cha Bonaventure kilicho karibu kuwa hifadhi za ndege. Kisiwa cha Bonaventure ni eneo la pili ambalo ndege wengi zaidi wa jamii ya membe huja kuzaliana.

Watu fulani wanadai kwamba hapo kale, Mwamba Percé ulikuwa umeungana na eneo la bara na huenda ulikuwa na matao manne. Ingawa hivyo, leo kuna tao moja tu lenye upana wa zaidi ya mita 30, lililo upande wa mwamba unaoelekeana na bahari. Wakati maji ya bahari yanapopungua, tuta la mchanga huunganisha mwamba huo na nchi kavu. Wakati wa kipindi hicho ambacho huchukua saa nne, watalii wenye ujasiri wanaweza kutembea hadi kwenye mwamba huo na kutembea kwa shida kwa dakika 15 hivi kando ya mwamba huo huku wakipigwa na mawimbi ili kufikia tao hilo.

Kwa wale wenye ujasiri, kuna tahadhari. Mtalii mmoja aliyepanda kwa kutambaa juu ya mawe yaliyokuwa yameanguka ili kufikia tao hilo anasema: “Baada ya kila dakika chache unaweza kuogopeshwa unaposikia ‘pwaa!’ wakati mawe yanayoanguka yanapopiga maji kwa kishindo kama cha mabomu madogo. Mawe mengine huangukiana na kutoa mlio kama wa bunduki iliyofyatuliwa.”

Wageni wengi wameona kwamba Mwamba Percé ni maridadi ajabu. Hata hivyo, huo ni sehemu ndogo tu ya mandhari maridadi zilizopo duniani. Mandhari hizo ni nyingi na tofauti kama nini! Unapoona mandhari hizo, huenda hata wewe unachochewa ‘kusimama tuli na kukazia fikira kazi za ajabu za Mungu.’—Ayubu 37:14.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]

© Mike Grandmaison Photography