Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Utiaji Nguo Rangi Nyakati za Kale na Siku Hizi

Utiaji Nguo Rangi Nyakati za Kale na Siku Hizi

Utiaji Nguo Rangi Nyakati za Kale na Siku Hizi

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

JE, UMEWAHI kuona jinsi rangi inavyoathiri hisia zetu? Basi haishangazi kwamba katika historia yote, wanadamu wametia nguo zao rangi.

Tunaponunua nguo na mapambo au vitambaa vinavyotumiwa kutengeneza vitu hivyo, hatutaki rangi yake ichujuke au kufifia. Ili kujifunza mbinu zinazotumika kutia nguo rangi inayokolea, na jinsi mbinu za kitamaduni za kutia rangi zilivyositawi, tulitembelea Shirika la Watiaji Rangi katika Jumba la Maonyesho ya Rangi huko Bradford, kaskazini mwa Uingereza. * Tukiwa huko tuliona rangi mbalimbali zisizo za kawaida ambazo zimetumiwa kwa karne nyingi.

Rangi Zilizotumiwa Zamani

Kufikia sehemu ya pili ya karne ya 19, rangi ambazo zilitumiwa kutia nguo zilitokana na vitu vya asili, kama vile mimea, wadudu, na samaki-gamba. Kwa mfano, mmea unaoitwa woad ulitokeza rangi ya bluu (1), mmea unaoitwa weld ulitokeza rangi ya manjano (2), na mmea unaoitwa madder ulitokeza rangi nyekundu. Rangi nyeusi ilitoka katika mti unaoitwa logwood, na kuvu inayoitwa archil ilitoa rangi ya zambarau. Samaki-gamba anayeitwa murex alitokeza rangi ya zambarau ya bei ghali ambayo wengine huiita zambarau ya Tiro au rangi ya wafalme (3). Rangi hiyo ilitumiwa kwenye nguo zilizovaliwa na maliki Waroma.

Muda mrefu kabla ya maliki Waroma, watu mashuhuri na matajiri walivaa mavazi yaliyotiwa rangi iliyotokana na vitu vya asili. (Esta 8:15) Kwa mfano, rangi nyekundu zilitolewa katika wadudu wa kike wanaoitwa kermes (4). Inaonekana kwamba rangi nyekundu ya kochinili, iliyotumiwa kwa ajili ya mapambo ya maskani ya Israeli na pia mavazi ya kuhani mkuu wa Israeli, ilitokana na wadudu hao.—Kutoka 28:5; 36:8.

Hatua za Kutia Rangi

Vitambaa vilivyoonyeshwa katika Jumba la Maonyesho ya Rangi zinaonyesha kwamba hatua nyingi za kutia rangi ni tata sana kuliko kuchovya nguo ndani ya rangi. Mara nyingi, hatua moja ya kutia rangi inahusisha kutumia kemikali fulani ya pekee ambayo hushikamana na nguo na rangi. Inapotumiwa, rangi hushikamana na kitambaa na hivyo haiwezi kuchujuka inapowekwa ndani ya maji. Kemikali nyingi hutumiwa kufanya hivyo, na nyingine hata ni hatari kuzitumia.

Njia fulani za utiaji rangi hutokeza harufu mbaya. Mojawapo ya njia hizo ni ile iliyotumiwa kutokeza rangi nyekundu. Njia hiyo ilikuwa tata na ilichukua muda mrefu. Njia hiyo ilitumiwa katika nguo zilizotengenezwa kutokana na pamba na ilitokeza rangi nyekundu nyangavu ambayo haingeweza kuathiriwa na mwangaza, ilipofuliwa, au ilipotiwa dawa ya kuondoa madoa. Wakati mmoja njia hiyo ilipitia hatua 38 tofauti na kukamilishwa baada ya miezi minne! Baadhi ya nguo maridadi zaidi zilizoonyeshwa katika jumba hilo la makumbusho ni zile zilizotiwa rangi hiyo nyekundu (5).

Kuvumbuliwa kwa Rangi Zinazotengenezwa Viwandani

Inasemekana kwamba rangi ya kwanza ambayo haikutengenezwa kutokana na vitu vya asili, ilitengenezwa na William Henry Perkin mnamo 1856. Katika maonyesho hayo, kuna maelezo fulani kuhusu ugunduzi wa Perkin wa rangi ya mauve, yaani, rangi iliyokolea ya zambarau. Kufikia mwisho wa karne ya 19, rangi nyingine nyingi zenye kuvutia zilitengenezwa viwandani. Leo zaidi ya aina 8,000 za rangi hizo hutengenezwa (6). Vitu vya asili pekee ambavyo bado vinatumiwa kutengeneza rangi ni logwood na kochinili.

Sehemu ya Maonyesho ya Rangi na Vitambaa katika Jumba la Maonyesho ya Rangi linatoa maelezo yanayofafanua hatua zinazohitajika leo ili kutia rangi vitambaa vinavyotengenezwa viwandani, kama vile rayoni. Rayoni inayoitwa viscose, ambayo ndiyo aina maarufu zaidi ya rayoni inayotumika sasa, ilianza kutengenezwa kwa ajili ya kuuzwa mnamo 1905. Kwa kuwa rayoni ina kemikali zilezile kama pamba, rangi nyingi zilizopatikana wakati huo zingeweza kutumika. Hata hivyo, aina chache mpya za rangi zilihitaji kutokezwa kwa ajili ya vitambaa vya kisasa zaidi vinavyotengenezwa viwandani kama vile, rayoni inayoitwa acetate, poliesta, nailoni, na akriliki.

Jitihada za Kutokeza Rangi Isiyochujuka

Tunaponunua nguo au vitambaa, sisi hutaka rangi yake idumu. Hata hivyo, rangi ya nguo nyingi hufifia kwa sababu ya jua au kwa sababu ya kufuliwa mara nyingi, hasa sabuni zinapotumiwa. Nyakati nyingine, rangi ya nguo hufifia kwa sababu ya jasho au hubadilika zinapofuliwa pamoja na nguo nyingine. Ili rangi idumu nguo zinapofuliwa, chembe za molekuli zinapaswa kushikamana sana na nyuzi zake. Kufuliwa mara nyingi na madhara yanayosababishwa na sabuni hufanya rangi iachane na nyuzi na hivyo nguo inapoteza rangi. Watiaji rangi hujaribu kuona ikiwa bidhaa zao zinaweza kustahimili athari zinazotokezwa na mwangaza, kufua, sabuni, na jasho.

Kutembelea kwetu Sehemu ya Rangi na Vitambaa katika Jumba la Maonyesho ya Rangi, kulitutia moyo tuchunguze ni nini kimetumiwa kutengeneza nguo zetu. Zaidi ya hilo, tulijifunza kuhusu mbinu za hali ya juu ambazo zimetumiwa kuhifadhi rangi za nguo zetu licha ya kufuliwa mara nyingi.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Shirika la Watiaji Rangi huendeleza sayansi ya rangi.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]

Photos 1-4: Courtesy of the Colour Museum, Bradford (www.colour-experience.org)

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

Photo 5: Courtesy of the Colour Museum, Bradford (www.colour-experience.org); Photo 6: Clariant International Ltd., Switzerland