Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Bata-Maji Mweusi” kwenye Mifereji ya Venice

“Bata-Maji Mweusi” kwenye Mifereji ya Venice

“Bata-Maji Mweusi” kwenye Mifereji ya Venice

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA

IKIWA imezingirwa na kuta zilizofyonza maji, madaraja ya mawe, madirisha yenye michoro, na baraza za ghorofani zilizojaa maua, mashua hiyo inasonga kupitia mfereji fulani. Ina rangi nyeusi, ni yenye fahari, na haina kelele. Kwa mbali inafanana na bata-maji mweusi. Badala ya kuwa na manyoya mororo, mwili wake umetengenezwa kwa mbao na shingo yake imetengenezwa kwa chuma, nayo inasonga kwa madaha kama ya bata-maji kati ya mifereji ya Venice, nchini Italia. Mashua hiyo ni gondola, ambayo kulingana na watu fulani ndiyo mashua maarufu zaidi ulimwenguni. Mashua hiyo ilibuniwa lini? Kwa nini ni maarufu sana? Ni nini kinachoitofautisha na mashua nyingine?

Ilibuniwa Lini?

Si rahisi kusema gondola ya kwanza ilibuniwa wakati gani hususa, ingawa watu fulani wanaamini ilibuniwa katika karne ya 11 W.K. Ilichorwa kwa mara ya kwanza mwishoni mwa karne ya 15. Lakini katika karne ya 17 na 18 ndipo ilianza kutengenezwa kwa umbo lake maarufu na linaloitofautisha na mashua nyingine. Sehemu ya chini ya gondola ilikuwa bapa, lakini katika kipindi hicho mashua hiyo ilianza kutengenezwa kwa umbo lake refu na omo ya chuma.

Vilevile si rahisi kujua jina gondola lilitoka wapi. Wengine wanasema neno “gondola” linatokana na neno la Kilatini cymbula, jina lililokuwa la boti dogo, au kutokana na conchula ambao ni mnyambulisho wa neno concha, linalomaanisha “kombe.”

Inapatikana Hasa Venice

Uhusiano kati ya mashua hiyo na jiji la Venice unaonekana waziwazi. Kwa kweli, huenda gondola ndiyo ishara muhimu zaidi ya jiji hilo. Hebu wazia picha zote za Venice zinazoonyesha gondola.

Kuna jambo lingine linalohusianisha mashua hiyo na jiji la Venice. Kusafiri kwenye mifereji ukiwa juu ya gondola “ni njia tofauti kabisa ya kuona jiji la Venice,” anasema Roberto, mwendesha gondola ambaye huwaongoza watalii kwenye mifereji ya huko. “Huoni tu sehemu zenye kuvutia za kawaida, unaona uhalisi wa Venice yenyewe.” Mwandishi maarufu Mjerumani Johann Wolfgang von Goethe alisema kwamba akiwa kwenye mashua hiyo alihisi kama “Mkuu wa Bahari ya Adriatiki, kama tu anavyohisi mkaaji yeyote wa Venice anapojilaza kwenye gondola yake.” Roberto anasema: “Mwendo wa polepole wa gondola unapatana kabisa na mazingira ya Venice. Ukiwa umestarehe kwenye mito laini, unahisi kwamba huna wasiwasi wowote.”

Mambo ya Pekee ya Gondola

Unapoangalia gondola, huenda ukashangaa kuona ni kana kwamba inasonga ikifuata mstari fulani, kwa sababu ina kasia moja tu iliyo upande wa kulia wa mashua ambayo imefungwa kwenye mhimili ulio katikati ya mashua. Ni rahisi kufikiri kwamba bila kusogeza-sogeza kasia mashua ingeelekea upande mmoja tu au ingezunguka mahali pamoja, lakini si hivyo. Kwa nini? Gilberto Penzo, mtaalamu wa mashua za kale, anaandika hivi: “Tukitumia mfano unaolinganisha umbo la mashua hiyo na kiwiliwili cha mwanadamu, mkuku utawakilisha uti wa mgongo na kiunzi kitawakilisha mbavu, kisha tunaweza kusema kwamba gondola ina tatizo baya sana la kujipinda uti wa mgongo.” Hilo linamaanisha kwamba, upande wa kulia wa kiunzi ni mwembamba kuliko upande wa kushoto kwa sentimita 24. Kwa sababu hiyo gondola huelea majini upande wake wa kulia ukiwa chini kuliko upande wa kushoto. Kwa sababu gondola huendeshwa kwa kasia moja huku mwendeshaji akiwa amesimama kwenye ukingo wa mashua hiyo, kuegama huko husaidia gondola kusonga kwa mstari ulionyooka.

Jambo la pekee la “bata-maji” huyo ni shingo, au omo yake. Tezi na omo ya mashua hiyo ndizo sehemu pekee zilizotengenezwa kwa chuma. Omo “ni yenye kuvutia na ya kipekee sana,” anaandika mwandishi Gianfranco Munerotto, “hivi kwamba mtu anayeiona kwa mara ya kwanza hawezi kuisahau.” Mbeleni, omo hiyo ya chuma ilisaidia kusawazisha uzito wa mwendesha gondola anayepiga kasia akiwa kwenye tezi, lakini sasa inatumiwa kuirembesha mashua hiyo. Kulingana na mapokeo, sehemu fulani zilizounganishwa kwenye omo huwakilisha sestieri, au maeneo sita ambayo jiji la Venice limegawanywa, huku sehemu ndogo inayotokeza nyuma ya shingo ikiwakilisha kisiwa cha Venice kinachoitwa Giudecca. Inasemekana kwamba umbo la omo linalofanana na herufi S huwakilisha umbo la Mfereji wa Grand huko Venice.

Jambo lingine linalofanya gondola iwe ya kipekee ni rangi nyeusi ya “manyoya” yake. Maelezo mengi sana yametolewa kuhusu sababu inayofanya mashua hizo kuwa nyeusi. Kulingana na ufafanuzi mmoja, katika karne ya 16 na 17, gondola zilipakwa rangi zenye kuvutia sana nazo zilifanywa zionekane kuwa za kifahari kupita kiasi na hivyo ili kusawazisha mambo, Bunge ya Venice ililazimika kuwatoza faini wamiliki wa mashua zilizopendeza zaidi. Lakini watu wengi walipendelea kulipa faini badala ya kuondoa mapambo hayo. Kwa sababu hiyo, hakimu mmoja aliamuru kwamba gondola zote zinapaswa kuwa na rangi nyeusi. Ufafanuzi mwingine unasema kwamba rangi nyeusi ilitumiwa kama ishara ya kuomboleza maelfu ya waliokufa kutokana na Tauni. Vilevile, ufafanuzi mwingine unasema kwamba rangi nyeusi ya mashua hizo ilitumika kuonyesha waziwazi weupe wa wanawake makabaila wa Venice. Hata hivyo, ukweli wenyewe ni rahisi sana. Mwanzoni, rangi nyeusi ilitokezwa kwa sababu ya lami iliyotumiwa kufanya mashua hizo zisiingize maji.

Baada ya kusafiri ukiwa juu ya bata-maji huyo mweusi, unarudi mahali ulipoanzia safari kwenye ngazi zilizo kando ya mojawapo ya mifereji ya Venice. Macho yako yanapoitazama gondola ikiondoka, huenda ukajiuliza ikiwa bata-maji huyo atageuza shingo yake ndefu na kulainisha manyoya yake.

[Picha katika ukurasa wa 24]

Upande mmoja wa kiunzi ni mwembamba kuliko upande mwingine

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Omo yake maarufu

[Picha katika ukurasa wa 25]

Roberto, mwendeshaji “gondola” katika mifereji ya Venice

[Picha katika ukurasa wa 25 zimeandaliwa na]

© Medioimages