Je, Ungependa Kula Viwavi?
Je, Ungependa Kula Viwavi?
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ZAMBIA
WATU wengine hawapendi kula viwavi. Lakini watu wengine wengi hufurahia kula wadudu hao watamu. Chakula kinachopendwa sana katika sehemu fulani za Afrika, ni kiwavi cha nondo anayeitwa Imbrasia belina. Barani Afrika kiwavi huyo anayeitwa mopane, jina linalotokana na mahali ambapo wadudu hao wanapenda kuishi, yaani kwenye mti wa mopane. Wakaaji wengi wa vijijini husubiri kwa hamu kukusanya viwavi hao wanaofaa sana kwa chakula. Keith Leggett, kutoka Shirika la Kuhifadhi Jangwa la Kalahari anasema, “Viwavi hao ni chanzo muhimu sana cha protini.” Pia viwavi hao huchangia sana kuhifadhi mazingira ya eneo hilo
la savana ambalo mara nyingi huwa kavu na halina rutuba sana.Mvua inaponyesha katika maeneo ya kusini mwa Afrika mapema katika mwezi wa Novemba (Mwezi wa 11), ardhi inakuwa na utendaji mwingi. Wakati huo mamilioni ya pupa huwa nondo. Katika majuma machache, mabuu hayo hubadilika na kuwa viwavi na kisha wanapokomaa wanapata umbo la kuvutia kama la “soseji” nono.
Katika maeneo ambayo vyakula vyenye wanga kama muhogo na mahindi huliwa sana, watu hupenda kula vyakula hivyo pamoja na viwavi. Ingawa wengi wetu hatungefikiria kula viwavi hao, wao ni wenye thamani hasa katika maeneo ambayo protini ni ghali au haipatikani kwa urahisi kwa sababu asilimia 60 ya miili ya viwavi hao ina protini. Viwavi fulani wanaoliwa wana protini sawa na ile inayopatikana kwenye nyama au samaki, nao huchangia asilimia 75 ya mahitaji ya mtu mzima ya protini, vitamini, na madini. Naam, wadudu hao wadogo wana lishe bora!
Walaji wa viwavi hushangaa kwamba wakulima wakubwa hutumia pesa nyingi kununua kemikali za kupigana na wadudu hao wenye lishe. Mamilioni ya wadudu hao wanapokula, wao hubadili majani yasiyoweza kuliwa ambayo nyakati nyingine huwa yenye sumu kuwa chakula chenye thamani. Wao hufanya hivyo bila kutumia vifaa vya kulimia vya bei ghali na bila kutibiwa na madaktari wa wanyama! Wadudu hao hukusanywa kwa mikono, nao ni chakula kinachopatikana bila jitihada nyingi.
Viwavi wanaoitwa mopane huchangia sana kurutubisha ardhi porini. Ingawa tembo wa Afrika hula sana, uwezo wake wa kumeng’enya chakula ni mdogo sana unapolinganishwa na ule wa kiwavi wa mopane. Kwa muda mfupi wa majuma sita wakiwa viwavi, wao hula chakula mara kumi zaidi na kutokeza mbolea mara nne zaidi ya tembo wanaolisha katika eneo lilelile. Si ajabu kwamba kiwavi huongeza uzito wa mwili wake mara 4,000! Kwa hiyo, haishangazi kwamba kukusanya viwavi kusikodhibitiwa kumepunguza rutuba ya udongo na kudhuru mazingira.
Viwavi hao hukusanywaje? Kila kunapokuwa na msimu wa mvua, wanawake wa vijijini hukusanyika ili kukusanya viwavi wa mopane mara mbili kwa mwaka. Kwa majuma kadhaa, wao hukusanya viwavi, kisha wanatoa viungo vya ndani, wanavichemsha, na kuvianika. Hata hivyo, kukusanya na kutayarisha viwavi wa aina fulani kunahitaji uangalifu wa pekee. Lazima manyoya au miiba ya kujilinda ya viwavi fulani iondolewe. Pia, uangalifu unahitajiwa unapotayarisha chakula hicho kwa sababu baadhi ya viwavi hula mimea inayoweza kuwadhuru wanadamu. Baada ya kutayarishwa, viwavi waliokaushwa wanaweza kutafunwa, ingawa mara nyingi wanatiwa tena ndani ya maji, wanachemshwa katika mchuzi, au kukaangwa kwa nyanya na kitunguu.
Huenda wazo la kula kiwavi likachochea hamu ya kula au huenda ukashikwa na kichefuchefu. Labda utajaribu kuepuka kula chakula hicho cha kipekee. Lakini kumbuka, viwavi ni chanzo kikubwa cha protini na riziki kwa ajili ya familia nyingi za Afrika.
[Picha katika ukurasa wa 26]
Kiwavi wa “mopane” ana thamani sana kwa sababu ana kiasi kikubwa cha protini
[Picha katika ukurasa wa 27]
Kwa muda mfupi wa majuma sita, viwavi wa “mopane” huongeza uzito wa miili yao mara 4,000