Ni Nani Wanaofurahia Nyakati Nzuri Kiuchumi?
Ni Nani Wanaofurahia Nyakati Nzuri Kiuchumi?
TUNAISHI katika ulimwengu wenye utajiri. Je, ni rahisi kuamini hilo? Kwa kweli, mataifa fulani yana pesa nyingi kuliko yanavyoweza kutumia. Imekadiriwa kwamba jumla ya mapato ya nchi zote ulimwenguni kutokana na bidhaa na huduma zilizotolewa katika mwaka wa 2005, ilizidi dola trilioni 60. Ikiwa pesa hizo zingegawanywa, kila mtu ulimwenguni angepata dola 9,000. Na mapato hayo yanaongezeka.
Lakini takwimu hizo zinatofautiana sana na hali halisi. Kulingana na kichapo cha karibuni cha Umoja wa Mataifa, watu watatu matajiri zaidi ulimwenguni wana mali nyingi zaidi kuliko jumla ya mapato ya mataifa 48 maskini zaidi. Na ripoti ya shirika la Mpango wa Ustawi wa Umoja wa Mataifa inasema kwamba watu bilioni 2.5 wanapata chini ya dola mbili kila siku. Mamia ya mamilioni hawapati chakula cha kutosha na hawawezi kupata maji safi ya kunywa.
Nchini Marekani, wanasoshiolojia wanachunguza kikundi cha watu ambao wanaelekea kuwa maskini. Watu hao wanakabili hatari ya kuwa maskini. Zaidi ya watu milioni 50 nchini humo wako katika hali hiyo licha ya utajiri mkubwa wa nchi hiyo.
Kwa nini pesa nyingi sana zinamwagika katika hazina na akaunti za benki huku mamia ya mamilioni ya maskini wakizidi kuzama katika umaskini? Kwa nini watu wengi hawafaidiki kutokana na utajiri wa ulimwengu unaozidi kuongezeka?
[Blabu katika ukurasa wa 3]
Watu watatu matajiri zaidi ulimwenguni wana mali nyingi zaidi kuliko jumla ya mapato ya mataifa 48 maskini zaidi
[Picha katika ukurasa wa 2, 3]
Watoto walioajiriwa katika kiwanda hiki cha matofali hulipwa senti 50 za Marekani kwa siku
[Hisani]
© Fernando Moleres/ Panos Pictures
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
© Giacomo Pirozzi/Panos Pictures