Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Tunda Linalopendwa Sana na Watengenezaji wa Manukato

Tunda Linalopendwa Sana na Watengenezaji wa Manukato

Tunda Linalopendwa Sana na Watengenezaji wa Manukato

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA

MANUKATO yametumiwa kwa miaka mingi. Katika nyakati za Biblia, nyumba zilitiwa manukato, vilevile mavazi, vitanda, na pia watu wenye uwezo walijipaka manukato. Vitu vilivyotumiwa kutengeneza manukato vilitia ndani mmea wa udi, marhamu, mdalasini, na viungo vingine.—Methali 7:17; Wimbo wa Sulemani 4:10, 14.

Uto unaotolewa katika mimea bado ni muhimu sana katika kutengeneza manukato. Tumekuja Calabria, eneo la kusini la rasi ya Italia kuona mahali ambapo uto huo hupatikana. Huenda usijue matunda ya aina ya bergamot kwa jina, lakini inasemekana kwamba harufu yake hupatikana katika asilimia 33 hivi ya manukato ya wanawake na karibu nusu ya manukato ya wanaume yanayouzwa madukani. Acha tukufahamishe mmea huu.

Mti wa bergamot ni mti wa jamii ya mlimau ambao nyakati zote una rangi ya kijani kibichi. Maua yake hutokea wakati wa masika, na matunda yake laini ya manjano yenye ukubwa wa chungwa hivi huwa yameiva mwishoni mwa majira ya kupukutika kwa majani au mwanzoni mwa majira ya baridi kali. Wataalamu wengi husema kwamba mti huo ni mchanganyiko wa mbegu nyingi, na chanzo chake hakijulikani. Huwezi kupata miti hiyo ikimea msituni, wala haipandwi kutokana na mbegu. Ili kuizalisha, wakulima hulazimika kukata matawi ya miti iliyopo na kuipachika kwenye aina fulani za mlimau.

Kwa watengenezaji wa manukato, matunda ya bergamot yana sifa za pekee. Kitabu kimoja kinachozungumzia uto unaotolewa katika matunda hayo kinasema mti huo una uwezo wa pekee wa “kuchanganyika na kufanyiza harufu mbalimbali, ili kutokeza manukato ya aina moja, na hivyo kutokeza harufu nzuri mahali popote unapotumiwa.” *

Uzalishaji wa Bergamot Huko Calabria

Maandishi ya kihistoria yanaonyesha kwamba miti ya bergamot ilikuzwa mwanzoni mwa karne ya 18 na kwamba mara kwa mara wenyeji waliwauzia wasafiri uto wa matunda yake. Hata hivyo, faida ya utengenezaji wa manukato ilifanya miti hiyo ipandwe kwa wingi. Katika mwaka wa 1704, Gian Paolo Feminis, Mwitaliano aliyehamia Ujerumani, alitengeneza manukato aliyoyaita Aqua admirabilis au “maji yanayotamanika.” Kiungo chake kikuu kilikuwa uto wa bergamot. Baadaye, manukato hayo yaliitwa eau de Cologne, yaani, “maji ya Cologne,” au cologne, jina la jiji ambapo yalitengenezewa.

Shamba la kwanza la bergamot lilipandwa huko Reggio mwaka wa 1750, na kwa sababu ya faida kubwa kutokana na mauzo ya uto wake, watu wengi walianza kupanda miti hiyo. Miti hiyo hukua vizuri sehemu ya kusini katika hali ya hewa ya wastani bila kuathiriwa na upepo mkali wa kaskazini, lakini haikui vizuri kukiwa na upepo mkali, mabadiliko ya ghafula ya joto, na unyevunyevu wa muda mrefu. Sehemu iliyo na hali hizo ina upana wa kilomita 5 na urefu wa kilomita 150, nayo iko karibu na pwani ya kusini ya Italia. Ingawa kuna jitihada za kuzalisha miti hiyo kwingineko, matunda mengi hukuzwa katika mkoa wa Reggio. Nchi ya Côte d’Ivoire, barani Afrika, huzalisha pia matunda hayo kwa wingi.

Mafuta ya bergamot, ambayo ni ya rangi ya kijani-manjano hutokana na maganda ya tunda hilo. Njia ya kienyeji iliyotumiwa kukamua mafuta hayo ilihusisha kukata tunda katikati, kutoa nyama yake, na kukamua maganda yake ili uto utoke kwenye utando wa nje ya maganda hayo na kufyonzwa na sifongo. Pauni 200 hivi za matunda yalihitaji kukamuliwa ili kupata pauni moja tu ya uto. Leo, kiasi kikubwa cha uto hukamuliwa kwa mashini zilizo na vifaa vya kuondoa maganda.

Ingawa Hayajulikani, Yanatumiwa Sana

Huenda tunda hilo lisijulikane nje ya Calabria lakini kitabu kimoja kinasema, “wataalamu wanathamini sana tunda hilo.” Harufu yake nzuri haipatikani tu kwenye manukato bali pia inaweza kupatikana kwenye sabuni, viondoa harufu, dawa ya meno, na mafuta ya kujipaka. Uto wa bergamot hutumiwa kuongeza ladha kwenye chai, aiskrimu, peremende, na vinywaji. Kwa kuwa unaweza kubadili rangi ya ngozi unatumiwa kutengeneza mafuta ambayo watu hujipaka wanapoota jua. Pia unatumika kutengeneza dawa za kuua viini zinazotumiwa katika upasuaji, matibabu ya macho, na ngozi. Asidi fulani inayopatikana katika matunda ya bergamot hutumiwa kuzuia damu kuvuja na pia hutumiwa kutengeneza dawa za kuzuia kuharisha.

Wachunguzi wamegundua vitu 350 hivi katika uto wa bergamot, ambavyo hufanya uto huo uwe na harufu nzuri na faida nyingine nyingi. Vyote hivyo vinapatikana katika tunda moja tu!

Labda waandikaji wa Biblia hawakuijua miti ya bergamot. Hata hivyo, yeyote ambaye angependa kuchunguza sifa za mlimau huo na hekima ya Muumba wake ana sababu ya kuunga mkono maneno haya ya mtunga-zaburi: “Msifuni Yehova . . . , enyi miti ya matunda.”—Zaburi 148:1, 9.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Kama vile watu fulani huwa na mizio kwa sababu ya vitu kama chavua au maua, wengine huathiriwa na manukato. Gazeti la Amkeni! halipendekezi bidhaa yoyote.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Uto wa bergamot hukamuliwa kutoka kwenye maganda ya matunda

[Hisani]

© Danilo Donadoni/Marka/age fotostock