Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Waliokoka Ugaidi Mumbai

Waliokoka Ugaidi Mumbai

Waliokoka Ugaidi Mumbai

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI INDIA

JIJI la Mumbai, ambalo zamani liliitwa Bombay, lina watu zaidi ya milioni 18. Kila siku, kati ya watu milioni sita na milioni saba husafiri kwa treni mpaka kazini, shuleni, vyuoni, madukani, au kwenye sehemu zinazopendeza. Kunapokuwa na watu wengi, badala ya kubeba abiria 1,710 kwenye kila treni yenye mabehewa tisa, wao hubeba abiria 5,000 hivi. Wakati kama huo, Julai 11, 2006, (11/7/2006) magaidi walishambulia treni za Mumbai. Kwa muda wa dakika 15 hivi, mabomu saba yalilipuka katika treni tofauti-tofauti kwenye Reli ya Magharibi, watu 800 walijeruhiwa na watu zaidi ya 200 wakafa.

Watu kadhaa katika makutaniko 22 ya Mashahidi wa Yehova huko Mumbai na maeneo ya karibu hutumia treni hizo na walikuwa katika treni zilizolipuliwa. Hakuna yeyote kati yao aliyekufa, lakini wachache walijeruhiwa. Kwa mfano, Anita alikuwa akielekea nyumbani kutoka kazini. Treni aliyokuwa amepanda ilikuwa imejaa pomoni, kwa hiyo alisimama karibu na mlango wa behewa la daraja la kwanza ili aweze kutoka kwa urahisi. Treni ilipokuwa ikisonga, kwa ghafula akasikia mlipuko mkubwa, na behewa lake likajaa moshi mweusi. Alipochungulia upande wa kulia, aliona kwamba sehemu zenye chuma za behewa lililokuwa karibu zilikuwa zimeng’oka na kuning’inia nje ya treni. Alishtuka kuona miili na sehemu za miili zikirushwa kwenye reli. Baada ya sekunde kadhaa, ambazo zilionekana kuwa kama muda mrefu kwake, treni ilisimama. Yeye pamoja na abiria wengine, waliruka nje na kukimbia mbali kabisa na treni hiyo. Anita alimpigia simu mumewe, John, na akafaulu kumpata; baada ya dakika chache watu hawangeweza kuwasiliana kwa simu kwa kuwa karibu kila mtu alikuwa akijaribu kupiga simu wakati huo. Wakati wote huo, Anita alikuwa ametulia lakini alipoanza kuongea na mumewe, ndipo alipoanza kulia. Alimweleza yaliyotukia na kumwomba aje kumchukua. Alipokuwa akimngojea, mvua ilianza kunyesha na kuondoa uthibitisho ambao ungewasaidia polisi.

Claudius, Shahidi mwingine wa Yehova, aliondoka ofisini mapema kuliko kawaida. Alipanda treni ya saa 11:18 jioni kwenye Kituo cha Churchgate, yaani, kituo cha jiji cha Reli ya Magharibi na kuingia behewa la daraja la kwanza. Alipokuwa akitafuta kiti kwa ajili ya safari yake ya saa moja hadi kwenye kituo cha Bhayandar, alimwona Shahidi mwingine kutoka kutaniko la karibu anayeitwa Joseph. Muda ulisonga haraka walipokuwa wakipashana habari. Kisha, Joseph akalala kwa sababu ya uchovu uliosababishwa na kazi yake. Kwa kuwa treni ilikuwa imejaa, Claudius alisimama kabla ya kituo alichokuwa ashukie ili aweze kufikia mlango. Claudius aliposimama, Joseph aliamka na kuegemea upande wa nyuma wa kiti ili amuage. Claudius alishikilia chuma kwenye kiti ili ainame na kuongea naye. Labda hilo ndilo jambo lililomwokoa Claudius. Kwa ghafula, kukawa na kelele. Behewa lilitikisika kwa nguvu, likajaa moshi, na kuwa na giza tititi. Claudius alirushwa sakafuni katikati ya viti na hangeweza kusikia chochote isipokuwa mlio fulani. Mahali alipokuwa ametoka kusimama, kulikuwa na shimo kubwa. Wasafiri waliokuwa wamesimama kando yake walirushwa kwenye reli na wengine waliokuwa wamekufa walikuwa wamelala sakafuni. Aliokoka mlipuko wa tano kati ya milipuko saba iliyotokea kwenye reli Jumanne hiyo.

Claudius alipelekwa hospitalini huku nguo zake zikiwa zimejaa damu. Damu hiyo hasa ilikuwa imetoka kwa wasafiri wengine. Alikuwa na majeraha madogo—aliumia sikio, aliungua mkono mmoja na nywele. Akiwa hospitalini alimwona Joseph na Angela, mke wa Joseph, ambaye alikuwa katika behewa la wanawake lililokuwa karibu. Angela hakuumia. Joseph alijeruhiwa jicho lake la kulia na hangeweza kusikia. Mashahidi hao watatu walimshukuru Yehova kwa kuwa hai. Claudius alisema kwamba baada tu ya kurudiwa na fahamu alifikiria jambo hili, ‘Hakuna maana yoyote ya kufuatilia pesa na mali katika mfumo huu kwa sababu unaweza kupoteza uhai wakati wowote!’ Alifurahi kama nini kwamba uhusiano wake pamoja na Mungu wake, Yehova, ndilo jambo muhimu zaidi maishani mwake!

Kwa muda mfupi tu, jiji la Mumbai lilikumbwa na mafuriko, ghasia, kisha milipuko ya bomu. Hata hivyo, Mashahidi zaidi ya 1,700 wa huko wana bidii. Kwa bidii wanaendelea kuwaeleza majirani wao kuhusu tumaini zuri la ulimwengu mpya ambao hautakuwa na jeuri.—Ufunuo 21:1-4.

[Blabu katika ukurasa wa 23]

Mahali alipokuwa ametoka kusimama, kulikuwa na shimo kubwa

[Picha katika ukurasa wa 23]

Anita

[Picha katika ukurasa wa 23]

Claudius

[Picha katika ukurasa wa 23]

Joseph na Angela

[Picha katika ukurasa wa 22 zimeandaliwa na]

Sebastian D’Souza/AFP/Getty Images