Je, Una Tatizo la Upofu wa Rangi?
Je, Una Tatizo la Upofu wa Rangi?
“Ninapovaa, mke wangu huniangalia kuhakikisha kwamba rangi za nguo zangu zinapatana,” anasema Rodney. “Wakati wa kifungua kinywa yeye hunichagulia kipande cha tunda kwa sababu siwezi kujua ikiwa tunda limeiva. Ninapotumia kompyuta kazini mara nyingi sijui nibofye wapi kwenye kiwambo kwani vitu vingi hutofautishwa kwa rangi. Ninapoendesha gari siwezi kutofautisha taa za barabarani kwani taa nyekundu na kijani huonekana sawa kwangu, hivyo mimi huangalia ikiwa taa iliyowaka iko juu au chini. Lakini taa za kuongozea magari zilizopangwa kwa mstari uliolala hunitatiza sana.”
* Kama ilivyo kwa watu wengine wanaoathiriwa na hali hiyo, si kwamba Rodney anaona rangi nyeusi na nyeupe tu, bali anaweza kuona rangi nyingine vilevile. Lakini tatizo ni kwamba hawezi kuona rangi fulani kama vile watu wasio na tatizo hilo wanavyoziona.
RODNEY ana tatizo la upofu wa rangi. Alirithi tatizo ambalo husababisha kasoro katika retina, sehemu inayopokea nuru ndani ya jicho. Tatizo la Rodney humpata mwanamume 1 kati ya 12 ambao wana asili ya Ulaya, na mwanamke 1 kati ya 200.Kwa kawaida katika jicho la mwanadamu, retina huwa na aina tatu za chembe zenye umbo la pia ambazo hutambua rangi. Kila moja imeundwa iweze kutambua rangi moja kati ya zile za msingi, yaani, bluu, kijani, au nyekundu. Nuru hupiga chembe hizo zenye umbo la pia kwa njia mbalimbali nazo huwasiliana na ubongo na kumwezesha mtu aone rangi. * Hata hivyo chembe za watu wenye upofu wa rangi haziwezi kutambua rangi moja au zaidi kwa kiwango kinachofaa, kwa hiyo hawawezi kutambua rangi vizuri. Ni vigumu kwa watu wengi wenye tatizo hilo kutofautisha kati ya rangi ya manjano, kijani, rangi ya machungwa, nyekundu, na hudhurungi. Tatizo hilo hufanya iwe vigumu kuona kuvu ya kijani kwenye mkate wa hudhurungi au kwenye jibini ya manjano, au inakuwa vigumu kutofautisha mtu mwenye jicho la bluu na nywele nyeupe na yule aliye na jicho la kijani na nywele nyekundu. Ikiwa mtu ana chembe dhaifu za kutambua rangi nyekundu, ua la waridi la rangi nyekundu linaonekana kuwa jeusi. Ni watu wachache sana wenye tatizo hilo ambao hawawezi kuona rangi ya bluu.
Watoto Wenye Tatizo la Upofu wa Rangi
Mara nyingi tatizo la upofu wa rangi ni la urithi, kwa hiyo mtu huzaliwa nalo na watoto walio na tatizo hilo wanakabiliana nalo bila kujua. Kwa mfano, hata kama hawawezi kuona tofauti kati ya rangi wanaweza kutambua tofauti kati ya uangavu wa rangi mbalimbali na kuzihusianisha na majina yake. Pia wao wanaweza kutambua vitu kwa kutegemea muundo wake na kwa kugusa badala ya kuvitambua kwa rangi yake. Kwa kweli, watoto wengi hawajui kwamba wana tatizo hilo.
Kwa kuwa shule nyingi hutumia vifaa vya kufundishia vya rangi, hasa katika madarasa ya chini, wazazi na walimu wanaweza kufikiri kwa makosa kwamba mtoto ana tatizo la kusoma na kumbe tatizo lake ni la upofu wa rangi. Mwalimu mmoja alimwadhibu mtoto wa miaka mitano kwa kuchora picha ya mawingu ya rangi ya waridi, watu wa rangi ya manjano, na miti yenye majani ya hudhurungi. Mtoto aliye na upofu wa rangi, anaweza kuona rangi hizo kuwa sawa kabisa. Jambo hilo limefanya wenye mamlaka wapendekeze kwamba watoto wachanga wachunguzwe kwa ukawaida ikiwa wana upofu wa rangi.
Ingawa hakuna matibabu kwa tatizo hilo, haliongezeki kadiri muda unavyopita wala kutokeza matatizo mengine ya macho. * Hata hivyo, upofu wa rangi ni tatizo linalofadhaisha sana. Chini ya Ufalme wa Mungu, Yesu Kristo ataondoa kutokamilika kote kutoka kwa wanadamu wanaomhofu Mungu. Hivyo, watu wenye matatizo yoyote ya macho wataweza kuona uumbaji wote wa Yehova ukiwa katika fahari yake.—Isaya 35:5; Mathayo 15:30, 31; Ufunuo 21:3, 4.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Tatizo la upofu wa rangi huwapata watu wote, lakini wengi wanaoathiriwa ni wenyeji wa asili wa Ulaya.
^ fu. 4 Wanyama wengi wanaweza kutambua rangi, ingawa njia yao ya kutambua rangi ni tofauti na yetu. Kwa mfano, mbwa wana aina mbili za chembe kwenye retina zao, yaani, ya bluu na nyingine iliyo kati ya rangi nyekundu na kijani. Ndege wengine nao wana aina nne za chembe na hata wanaweza kutambua aina fulani ya nuru ambayo wanadamu hawawezi.
^ fu. 8 Wakati mwingine, upofu wa rangi unaweza kusababishwa na magonjwa. Ukigundua mabadiliko ya kuona rangi baadaye maishani, unaweza kumwona daktari wa macho.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]
KUPIMA UPOFU WA RANGI
Mara nyingi kujua aina na kiwango cha upofu wa rangi huhusisha madoa yaliyopangwa ya rangi mbalimbali. Kipimo kinachotumika sana ni Ishihara, nacho kina mipangilio 38. Kwa mfano, mpangilio mmoja ukiangaliwa mchana na mtu wa kawaida, ataona namba 42 na 74 (kushoto), naye mtu aliye na tatizo la kawaida la kutoona rangi nyekundu na ya kijani, hataona namba yoyote hapo juu lakini ataona 21 chini. *
Kama vipimo vinaonyesha kuna tatizo, daktari wa macho anaweza kupendekeza uchunguzi zaidi ili kutambua ikiwa ni tatizo la kurithi au kuna mambo mengine ambayo yamesababisha tatizo hilo.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 15 Michoro hii inaonyeshwa tu kwa kusudi la kutoa kielelezo. Vipimo vinapaswa kufanywa na daktari anayestahili.
[Hisani]
Color test plates on page 18: Reproduced with permission from the Pseudoisochromatic Plate Ishihara Compatible (PIPIC) Color Vision Test 24 Plate Edition by Dr. Terrace L. Waggoner/www.colorvisiontesting.com
[Sanduku katika ukurasa wa 19]
KWA NINI WANAUME WENGI WANAATHIRIWA?
Matatizo ya upofu wa rangi yanapatikana kwenye kromosomu ya X. Mwanamke ana kromosomu mbili za X, naye mwanamume ana moja ya X na nyingine Y. Kwa hiyo mwanamke akirithi tatizo kwenye kromosomu ya X, kromosomu ile nyingine italifuta. Lakini mwanamume akirithi tatizo hilo hana kromosomu ya pili ya X ya kulifuta.
[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 18]
JINSI TUNAVYOONA RANGI
Nuru inayotoka kwenye vitu inapita kwenye konea na lenzi na inaelekezwa kwenye retina
Konea
Lenzi
Retina
Taswira huingia kwenye jicho ikiwa imejipinda lakini baadaye ubongo huirekebisha
NEVA YA JICHO hupeleka picha kwenye ubongo
RETINA ina chembe zenye umbo la pia na kijiti. Zikiwa pamoja zinamfanya mtu aone vizuri
Chembe zenye umbo la kijiti
Chembe zenye umbo la pia
CHEMBE ZENYE UMBO LA PIA zinamsaidia mtu kutambua rangi nyekundu, kijani, au bluu
Nyekundu
Kijani
Bluu
[Picha]
Uwezo wa kawaida wa kuona
Jicho lenye upofu wa rangi