Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
▪ Katibu mtendaji wa Wizara ya Usafiri nchini Marekani, Maria Cino, amesema kwamba “moja kati ya uhalifu mkubwa zaidi unaofanywa nchini Marekani ni ule wa mtu kuendesha gari akiwa amelewa.” Asilimia 39 ya watu waliokufa katika misiba ya barabarani mwaka wa 2005, ilihusisha kileo.—WIZARA YA USAFIRI YA MAREKANI.
▪ “Kuna takataka zaidi ya 18,000 za plastiki zinazoelea kwenye kila kilomita ya mraba baharini.”—SHIRIKA LA MAZINGIRA LA UMOJA WA MATAIFA.
▪ “Wafanyakazi Wamarekani wanatumia saa nusu bilioni kila mwaka wakicheza michezo [ya kompyuta] kazini, na hilo husababisha makampuni yapoteze dola bilioni 10.” Gharama hizo hazitii ndani wakati “wanaotumia kwenye Intaneti wakati wa kazi kwa ajili ya mambo ya kibinafsi.”—MANAGEMENT-ISSUES WEB SITE.
Jeuri Dhidi ya Watoto
Shirika la Afya Ulimwenguni linasema: “Kwa watoto wengi jeuri ni sehemu ya maisha yao ya kila siku.” Ripoti ya karibuni ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ilisema kwamba “mwaka wa 2002, karibu watoto 53,000 waliuawa ulimwenguni pote.” Isitoshe, mamilioni ya watoto wanatumiwa vibaya kwa kulazimishwa kufanya kazi, ukahaba, au ponografia (picha au habari za ngono). Je, maovu hayo yangeweza kuepukwa? Ripoti hiyo ilisema: “Kuwalinda watoto nyumbani kunatia ndani kuwafunza na kuwatunza kwa njia inayofaa, kuwapo kwa uhusiano mzuri kati ya wazazi na watoto, na kutoa nidhamu isiyohusisha jeuri.”
Marafiki Wazuri Wanatusaidia Tuwe na Maisha Marefu!
Ripoti ya gazeti Journal of Epidemiology and Community Health inaonyesha kwamba huenda marafiki wazuri wakamsaidia mtu awe na maisha marefu. Kuna uchunguzi uliofanywa kwa kipindi cha miaka kumi huko Australia uliohusisha watu 1,500 wenye umri wa miaka 70 na zaidi, ili kuona jinsi mahusiano yao yalivyochangia urefu wa maisha yao. Watu waliokuwa na marafiki wachache walikufa zaidi kwa asilimia 22 kuliko wale waliokuwa na marafiki wengi. Ripoti hiyo inasema kwamba marafiki huwaathiri watu wazee inapohusu mambo kama vile “kushuka moyo, uwezo wa kufanya mambo, kukabiliana na matatizo, na pia kujithibiti.”
Waingereza Wana Madeni Mengi
“Zaidi ya asilimia 33 ya watu wazima wenye akaunti ya benki wanachukua pesa kwenye benki zinazozidi zile ambazo wameweka akiba,” gazeti The Daily Telegraph la London linasema. Badala ya kutumia maandalizi hayo kukiwa na hali ya dharura, Waingereza milioni 3.5 wanaona kutumia pesa hizo kuwa “jambo la lazima.” Keith Tondeur, mkurugenzi mkuu wa shirika la Credit Action, analalamika kuhusu “watu katika jamii yetu wenye mazoea ya kutosheleza tamaa zao mara moja.” Tondeur anaonya: “Kati yetu kuna mamilioni wanaotumia pesa zinazozidi mapato yao, hata wanakosa pesa kwa ajili ya elimu, lakini wengi hawatambui gharama zinazotokana na tabia hii.”
Ndege Zinazosafiri Usiku Zinaongeza Joto Ulimwenguni
Jarida Scientific American limeripoti kwamba mvuke unaoachwa na ndege za abiria unaathiri kiwango cha joto hewani. Wakati wa mchana mvuke huo hupunguza kiwango cha joto. Lakini usiku, mvuke huongeza kiwango cha joto. Ripoti hiyo inasema kwamba wachunguzi Waingereza wamegundua kuwa “ingawa ndege zinazosafiri kati ya saa 12 jioni na 12 asubuhi ni robo tu ya ndege zote zinazoruka kwa siku moja, katika kipindi hicho ndege huongeza kiwango cha joto kwa asilimia 60 hadi 80.”