Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Shark Bay—Eneo la Ajabu la Baharini

Shark Bay—Eneo la Ajabu la Baharini

Shark Bay—Eneo la Ajabu la Baharini

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

SHARK BAY (Ghuba ya Papa) ni ghuba kubwa iliyo kwenye sehemu ya mashariki zaidi ya Australia, kilomita 650 kaskazini mwa jiji la Perth. Mnamo 1629, mvumbuzi Mholanzi Francois Pelsaert alisema kwamba eneo hilo la jangwa ni “nchi kavu iliyolaaniwa, ambako hakuna nyasi zozote zinazoweza kuota.” Wageni walipaita Mahali Pasipo na Matumaini, Mahali Pasipofaa Kitu, na Mahali Penye Kuvunja Moyo.

Hata hivyo, leo zaidi ya watu 120,000 hutembelea eneo hilo kila mwaka. Eneo hilo linavutia sana hivi kwamba liliingizwa kwenye Orodha ya Maeneo Yanayostahili Kuhifadhiwa Ulimwenguni mwaka wa 1991. *

Eneo la Malisho Lenye Utendaji Mwingi

Ikiwa Pelsaert angeangalia chini ya bahari angeona nyasi alizokuwa akitafuta, kwani Shark Bay ndilo eneo kubwa zaidi duniani lililo na aina tofauti-tofauti za nyasi za baharini. Eneo hilo lote lina ukubwa wa kilomita 4,000 za mraba. Ufuo wa Wooramel Seagrass pekee unaenea kilomita 130 upande wa mashariki wa Shark Bay.

Nyasi za baharini ni mimea inayotoa maua, ambayo hutegemeza viumbe wengi wa baharini. Kamba, samaki wadogo, na viumbe wengine wengi huishi kati ya mimea hiyo. Nyasi hizo za baharini huandaa chakula kwa ajili ya viumbe 10,000 hivi waitwao dugong, au ng’ombe wa baharini. Wanyama hao wapole na wenye udadisi mwingi ambao wanaweza kufikia uzito wa kilo 400, hula nyasi hizo, nyakati nyingine wakiwa katika makundi ya ng’ombe zaidi ya 100. Kwa sasa inaelekea kwamba huko Australia kaskazini ndiko ng’ombe hao wanapatikana kwa wingi zaidi ulimwenguni, kuanzia Shark Bay upande wa magharibi hadi Moreton Bay upande wa mashariki. *

Kama tu jina la mahali hapo linavyoonyesha, Shark Bay ina papa wengi sana wa aina tofauti-tofauti. Papa hao wanatia ndani papa mwenye kuogopesha anayeitwa tiger na pia kuna papa-nyangumi ambaye ni papa mkubwa asiyedhuru, naye ndiye samaki mkubwa zaidi ulimwenguni. Kwenye eneo hilo pomboo na papa wanaishi pamoja, jambo ambalo wengi hufikiria haliwezekani. Kwa kweli, watafiti wamegundua kwamba asilimia 70 ya pomboo wana makovu yanayotokana na kushambuliwa na papa. Nyangumi wengi wenye nundu hupumzika hapo kila mwaka wakiwa safarini kuelekea kusini, na kuna idadi kubwa ya kasa wanaoenda kutagia mayai yao hapo kila mwaka.

Je, Kweli Hiyo Ni Miamba?

Tofauti na sehemu nyingine za ghuba hiyo, Hamelin Pool iliyo kwenye upande wa kusini zaidi wa Shark Bay haipendezi na inaonekana kama haina uhai. Kwa sababu ya mvukizo mwingi sana eneo hilo lina chumvi maradufu ya chumvi ya bahari yenyewe. Kunakuwa na vitu vinavyofanana na miamba yenye rangi hafifu ya kijivu kwenye ukingo. Hata hivyo, uchunguzi wa uangalifu unaonyesha kwamba “miamba” hiyo ni stromatolite, vitu ambavyo hutokezwa na wadudu wengi wadogo wenye chembe moja wanaoitwa cyanobacteria au mwani wenye mchanganyiko wa rangi ya bluu na kijani. Unaweza kupata bilioni tatu kati yao katika eneo la mita 1 ya mraba!

Wadudu hao wadogo huchanganya uteute unaonata na vitu vilivyotolewa katika maji ya chumvi ili kufanyiza saruji ambayo wao huongeza hatua kwa hatua kwenye nyumba yao iliyo kama mwamba. Hatua hizo zote huchukua wakati mwingi sana. Kwa kweli, miaka 1,000 hivi inaweza kuwa imepita mwamba huo unapokuwa na kimo cha sentimita 30!

Hamelin Pool ina stromatolite nyingi na za aina tofauti-tofauti kuliko sehemu nyingine duniani. Isitoshe, hilo ndilo eneo pekee duniani lenye mkusanyo wa aina hiyo wa stromatolite.

Mambo Yanayovutia ya Shark Bay

Viumbe wanaovutia zaidi huko Shark Bay ni pomboo wenye pua pana (bottlenose) wanaopatikana eneo la Monkey Mia kwenye Rasi ya Denham. Monkey Mia ni moja kati ya sehemu chache ulimwenguni ambapo pomboo ambao si wa kufugwa huja kukutana na watu. Hakuna anayejua walianza lini kukutana huko na watu.

Watu wengine wanasimulia kwamba katika miaka ya 1950, pomboo walielekeza samaki kwenye sehemu yenye maji yasiyo na kina kirefu ili waweze kuwakamata kwa urahisi, jambo ambalo linaonekana hadi leo. Labda watu walichukua fursa hiyo kuwalisha na kuwa marafiki wao. Mnamo 1964, mvuvi mmoja huko Monkey Mia alimrushia pomboo aliyekuwa akicheza karibu na mashua yake samaki. Pomboo huyo ambaye alikuja kuitwa Charlie, alirudi usiku uliofuata na akachukua samaki kutoka mkononi mwa mvuvi huyo. Muda si muda, marafiki wa Charlie walijiunga naye.

Tangu wakati huo, vizazi vitatu vya pomboo vimewafurahisha mamilioni ya wageni wanaotembelea eneo hilo. Pia wamewafurahisha wanabiolojia zaidi ya 100 kutoka nchi mbalimbali ambao wamefanya utafiti kuhusu wanyama hao, ikiwafanya kuwa pomboo waliofanyiwa utafiti mwingi zaidi kuliko pomboo wengine duniani.

Mara nyingi siku hizi pomboo wakiwa na watoto wao hupenda kutembelea Monkey Mia hasa saa za asubuhi. Umati wa wageni husubiri kwa hamu kuwasili kwao, lakini ni wachache tu wanaowalisha. Kwa nini? Kwa sababu walinzi wa mbuga wanajaribu kuwazuia wasizoee kulishwa. Hata hivyo, watu wote waliopo wanaweza kushuhudia tukio zima. Mwanamke mmoja alisema hivi, “Laiti wanadamu wangeweza kuwa na uhusiano kama huu na viumbe vyote!”

Biblia inafunua kwamba tamaa kama hiyo inaonyesha kusudi la kwanza la Mungu kwa ajili ya mwanadamu la kutiisha wanyama wote kwa amani. (Mwanzo 1:28) Kama unapenda wanyama, utafurahia kujua kwamba ingawa kutimizwa kwa kusudi la Mungu kulikatizwa kwa muda na dhambi, kutatimizwa kikamili wakati ambapo Ufalme wa Mungu, chini ya Yesu Kristo, utatawala dunia.—Mathayo 6:9, 10; Ufunuo 11:15.

Chini ya Ufalme wa Mungu dunia nzima itakuwa hifadhi yenye umaridadi wa kiasili, iliyojaa viumbe vyenye uhai na afya. Karibuni wanadamu watafurahia zaidi kutembelea maeneo kama vile Shark Bay.—Zaburi 145:16; Isaya 11:6-9.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Maeneo yenye thamani ya kipekee ya kitamaduni au kiasili hutiwa kwenye Orodha ya Maeneo Yanayostahili Kuhifadhiwa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni.

^ fu. 7 Ingawa dugong wana uhusiano na nguva, wao ni wa jamii tofauti. Nguva wana mikia iliyojipinda nao dugong wana mikia iliyonyooka kama vile mikia ya pomboo.

[Ramani katika ukurasa wa 15]

 

AUSTRALIA

SHARK BAY

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Picha ya angani ya ufuo wa Monkey Mia

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

“Dugong” au ng’ombe wa baharini

Picha zimeandaliwa na]

© GBRMPA

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Mabilioni ya wadudu wadogo sana hujenga “stromatolite”

[Picha katika ukurasa wa 17]

Pomboo ambao si wa kufugwa hufika kwenye ufuo wa Monkey Mia

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

© GBRMPA; satellite map: Jeff Schmaltz, MODIS Rapid Response Team, NASA/GSFC

[Picha katika ukurasa wa 17]

All images, except dugong, supplied courtesy Tourism Western Australia