Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Safari yenye Msiba ya Manowari za Hispania

Safari yenye Msiba ya Manowari za Hispania

Safari yenye Msiba ya Manowari za Hispania

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA

ZAIDI ya miaka mia nne iliyopita, vikosi viwili vya wanamaji vilipigana katika Mlango-Bahari wa Uingereza. Vita hivyo kati ya Waprotestanti na Wakatoliki vilikuwa sehemu ya mapambano yaliyotokea katika karne ya 16 kati ya majeshi ya Malkia Mprotestanti Elizabeth wa Kwanza wa Uingereza na Mfalme Mkatoliki Philip wa Pili wa Hispania. Kitabu The Defeat of the Spanish Armada kinaeleza hivi: “Kwa maoni ya watu waliokuwa wakiishi wakati huo, vita hivyo kati ya majeshi ya wanamaji wa Uingereza na Hispania katika Mlango-Bahari wa Uingereza vilikuwa mapambano ya kufa na kupona kati ya majeshi ya nuru na majeshi ya giza.”

Watu waliokuwa wakiishi Uingereza wakati huo wanafafanua Manowari za Hispania kuwa “jeshi kubwa zaidi la wanamaji kusafiri baharini.” Lakini uamuzi wa kutuma majeshi hayo ulikuwa mbaya kwani maelfu ya watu walikufa. Safari hiyo ilikuwa na kusudi gani, na kwa nini haikufaulu?

Kwa Nini Walijaribu Kuvamia?

Kwa miaka mingi, maharamia Waingereza walipora meli za Hispania, na Malkia Elizabeth wa Uingereza aliunga mkono kwa dhati uasi wa Uholanzi dhidi ya utawala wa Hispania. Isitoshe, Mfalme Mkatoliki Philip wa Pili aliona kuwa ni jukumu lake kuwasaidia Waingereza Wakatoliki waondolee mbali harakati ya Waprotestanti ambao waliiona kuwa “uasi.” Kwa sababu hiyo, Manowari za Hispania zilikuwa na makasisi na washauri wa kidini 180 hivi. Majeshi ya Manowari yalipokusanyika, kila mtu aliungama dhambi zake kwa kasisi na akala Sakramenti.

Hali ya kidini nchini Hispania na ya mfalme wa nchi hiyo ilionekana wazi katika maneno haya ya Mjesuti Mhispania Pedro de Ribadeneyra: “Mungu Bwana wetu, atatutangulia kwa sababu tunatetea imani na kusudi lake takatifu. Tukiwa na kapteni kama huyo hatuogopi chochote.” Kwa upande mwingine, Waingereza walitumaini kwamba ikiwa wangeshinda vita hivyo Uprotestanti ungeenea katika bara lote la Ulaya.

Mbinu aliyopendekeza Mfalme wa Hispania ilionekana kuwa kazi rahisi. Aliagiza Manowari hizo ziende hadi Mlango-Bahari wa Uingereza na kulichukua jeshi la Dyuki wa Parma la watu 30,000 huko Flanders. * Kisha vikosi hivyo viwili vingepitia Mlango huo na kutua pwani ya Essex, na mwishowe kuingia London. Philip alifikiri kwamba Wakatoliki Waingereza wangemsaliti malkia wao Mprotestanti na kujiunga na jeshi lake.

Hata hivyo, mbinu ya Philip ilikuwa na dosari nyingi. Ingawa alifikiri alitegemezwa na kuongozwa na Mungu, alipuuza mambo mawili, yaani, nguvu ya jeshi la wanamaji la Uingereza na ugumu wa kuchukua majeshi ya Dyuki wa Parma bila kuwa na mahali penye kilindi kilichofaa kwa ajili ya kukutana.

Jeshi Kubwa Lililo Gumu Kuongoza

Philip alimweka rasmi Dyuki wa Medina-Sidonia awe kamanda wa Manowari hizo. Ingawa Dyuki huyo hakuwa na ujuzi wa kuongoza majeshi ya majini, alikuwa na uwezo mzuri wa kupanga mambo na muda si muda, makapteni wake wenye ujuzi walifurahia kumuunga mkono. Pamoja, waliunda kikosi cha vita na kutafuta maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kikosi hicho kikubwa. Walikubaliana kuhusu ishara watakazotumia kuwasiliana, mpangilio wa kusafiri, na mbinu ya kudumisha umoja katika jeshi lao la kimataifa.

Wakitumia meli 130 zilizokuwa na askari 20,000 hivi na mabaharia 8,000, waliondoka mji wa Lisbon Mei 29, 1588 (29/5/1588). Lakini upepo mkali wa dhoruba uliwafanya watue huko La Coruña, kaskazini-magharibi mwa Hispania, ili wafanye ukarabati na kuongeza bidhaa nyingine. Akiwa na wasiwasi kuhusu chakula, maji, na afya ya askari wake, Dyuki wa Medina-Sidonia alimwandikia mfalme waziwazi kuhusiana na mashaka yake juu ya safari hiyo. Lakini Philip alisisitiza kwamba kamanda wake aendelee na safari kama walivyokuwa wamepanga. Kwa hiyo Manowari hizo ziliendelea na safari, na miezi miwili baada ya kutoka Lisbon zikafika Mlango-Bahari wa Uingereza.

Vita Kwenye Mlango-Bahari wa Uingereza

Majeshi ya Wahispania yalipofika kwenye pwani ya Plymouth, huko kusini-magharibi mwa Uingereza, majeshi ya Waingereza yalikuwa yakingoja. Pande zote mbili zilikuwa na idadi inayolingana ya meli lakini muundo wa meli hizo ulitofautiana. Meli za Hispania zilikuwa ndefu na kwenye sitaha kulikuwa na bunduki za masafa mafupi. Kulikuwa na minara kwenye omo na tezi iliyofanya zifanane na minara iliyoelea. Wanajeshi Wahispania walitaka kutumia mbinu ya kuwakaribia maadui na kuwavamia. Nazo meli za Waingereza zilikuwa fupi na zilienda kwa kasi zikiwa na mizinga ya masafa marefu. Makapteni wao walitaka kuepuka kukaribia maadui na hivyo waangamize meli za Wahispania kutoka mbali.

Ili kukabiliana na wepesi na mizinga ya meli za Uingereza, kamanda wa Manowari za Hispania alipanga meli hizo kwa umbo la nusu mwezi. Meli zenye nguvu zilizokuwa na bunduki za masafa marefu zililinda miisho yote. Kwa hiyo, hata maadui wakitokea upande upi, Manowari hizo zingegeuka na kukabiliana nao kama vile nyati anavyoelekeza pembe zake kuelekea simba anayemkaribia.

Majeshi hayo mawili yalizozana-zozana kwenye Mlango-Bahari wa Uingereza na yakapigana vita viwili vidogo. Mpangilio huo wa meli za Wahispania uliwasaidia, na mizinga ya masafa marefu ya Waingereza haikuweza kuizamisha meli yoyote ya Wahispania. Makapteni Waingereza walikata kauli kwamba lazima wavunje mpangilio huo na kuwakaribia. Walipata nafasi hiyo Agosti (Mwezi wa 8) 7.

Dyuki wa Medina-Sidonia alifuata maagizo aliyopewa na kuelekeza Manowari zake hadi mahali walipopaswa kukutana na Dyuki wa Parma na vikosi vyake. Dyuki wa Medina-Sidonia alipokuwa akisubiri ujumbe kutoka kwa Dyuki wa Parma, aliamrisha meli zake zitie nanga kwenye pwani ya Ufaransa huko Calais. Meli za Hispania zikiwa zimetia nanga na hivyo kukabili hatari ya kushambuliwa kwa urahisi, Waingereza walituma meli nane ambazo walizijaza vitu vinavyoweza kulipuka na kuziwasha. Makapteni wengi Wahispania walijaribu kurudi baharini ili waziepuke meli hizo. Kisha upepo mkali na mikondo ya bahari iliwasukuma upande wa kaskazini.

Jua lilipochomoza siku iliyofuata, vita vya mwisho vilipiganwa. Majeshi ya Waingereza yalivamia meli za Wahispania kutoka karibu, na meli tatu hivi ziliteketezwa na nyingine nyingi zikaharibiwa kwa kiasi fulani. Kwa sababu Wahispania hawakuwa na silaha za kutosha, walivumilia uvamizi huo.

Dhoruba kali iliwafanya Waingereza waache kupigana hadi siku iliyofuata. Asubuhi hiyo, Wahispania walijipanga tena katika umbo la nusu mwezi, na wakiwa na silaha chache walijitayarisha kupigana na maadui wao. Lakini kabla ya Waingereza kushambulia, meli za Wahispania zilisukumwa na upepo na mikondo na kukwama kwenye vilima vya mchanga huko Zeeland karibu na pwani ya Uholanzi.

Ilipoonekana kwamba hawana matumaini yoyote, upepo uliwasukuma kaskazini kwenye bahari ambapo walikuwa salama. Lakini hawangeweza kurudi hadi Calais kwani meli za Waingereza zilikuwa zimefunga njia, na upepo mkali bado ulikuwa unasukuma meli za Wahispania zilizokuwa zimeishiwa nguvu kaskazini. Dyuki wa Medina-Sidonia aliamua kwamba hangeweza kuendelea na vita hivyo na badala yake aokoe meli na wanajeshi wengi iwezekanavyo. Aliamua kurudi Hispania kwa kuzunguka kupitia Scotland na Ireland.

Dhoruba na Kuvunjika kwa Meli

Safari ya kurudi nyumbani haikuwa rahisi kwa Manowari hizo zilizokuwa zimevamiwa. Kulikuwa na chakula kidogo sana, na kwa sababu matangi yalikuwa yanavuja, kulikuwa na maji machache. Mashambulizi ya Waingereza yalikuwa yameharibu meli nyingi na chache sana zingeweza kusafiri. Kisha, zikiwa kwenye pwani ya kaskazini magharibi ya Ireland, Manowari hizo zilikumbwa na dhoruba kali kwa majuma mawili. Meli nyingine zilipotea kabisa na nyingine zikavunjika kwenye pwani ya Ireland.

Hatimaye, mnamo Septemba (Mwezi wa 9) 23, meli za kwanza za Manowari zilijikokota kuingia bandari ya Santander, kaskazini mwa Hispania. Ni meli 60 hivi na karibu nusu ya watu walioondoka Lisbon waliofaulu kurudi nyumbani. Maelfu walizama baharini. Wengine wengi walikufa kutokana na majeraha au magonjwa waliyopata walipokuwa wakirudi nyumbani. Kwa waokokaji waliofika kwenye pwani ya Hispania, masaibu hayakuishia hapo.

Kitabu The Defeat of the Spanish Armada kinasema: “Meli kadhaa hazikuwa na vyakula, hivyo watu waliendelea kufa njaa,” ingawa walikuwa wametia nanga kwenye bandari moja ya Hispania. Kitabu hicho kinasema kwamba meli moja ilivunjika katika bandari ya Laredo huko Hispania, “kwa sababu hakukuwa na wanaume wa kutosha wa kuteremsha matanga na kutia nanga.”

Matokeo ya Kushindwa

Kushindwa kwa Manowari za Hispania kuliwachochea sana Waprotestanti wa Ulaya Kaskazini, hata ingawa vita vya kidini viliendelea. Waprotestanti waliamini kwamba ushindi huo ulithibitisha kwamba walikuwa na kibali cha Mungu, jambo linaloonyeshwa na medali moja ya Waholanzi iliyotengenezwa kukumbuka tukio hilo. Medali hiyo ilikuwa na maandishi haya, Flavit יהוה et dissipati sunt 1588 na maana yake ni “Yehova alipuliza nao wakatawanyika mwaka wa 1588.”

Baada ya muda, nchi ya Uingereza ikawa serikali kuu ya ulimwengu kama kitabu Modern Europe to 1870 kinavyosema: “Mnamo 1763, Uingereza iliibuka kuwa serikali kuu ya ulimwengu kibiashara na kikoloni.” Kwa kweli, “katika 1763 Milki ya Uingereza ilitawala ulimwengu kana kwamba Roma ilikuwa imefufuliwa na kupanuliwa,” kinasema kitabu Navy and Empire. Baadaye, Uingereza iliungana na koloni yake ya zamani, Marekani, na kufanyiza serikali ya ulimwengu ya Uingereza na Marekani.

Wanafunzi wa Biblia wanapendezwa sana na kuinuka na kuanguka kwa serikali kuu za ulimwengu. Hiyo ndiyo sababu Maandiko Matakatifu yamezungumzia kwa urefu mfuatano wa serikali kuu za ulimwengu ikianza na Misri, Ashuru, Babiloni, Muungano wa Umedi na Uajemi, Ugiriki, Roma, na hatimaye serikali ya ulimwengu ya Uingereza na Marekani. Kwa kweli, Biblia ilitabiri mapema sana kuinuka na kuanguka kwa serikali kadhaa kati ya hizo.—Danieli 8:3-8, 20-22; Ufunuo 17:1-6, 9-11.

Tukitafakari yale yaliyotukia kiangazi cha 1588, ni wazi kwamba lilikuwa jambo muhimu sana kwa Manowari za Hispania kushindwa. Miaka 200 hivi baada ya kushindwa kwa Manowari hizo, Uingereza iliibuka kuwa serikali kuu ya ulimwengu, na mwishowe ikatimiza sehemu muhimu ya unabii wa Biblia.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 8 Hii ilikuwa sehemu ya Uholanzi iliyotawaliwa na Wahispania katika karne ya 16. Eneo hilo lilitia ndani sehemu za pwani za kaskazini ya Ufaransa, Ubelgiji, na Uholanzi.

[Ramani/Picha katika ukurasa wa 26, 27]

 

Safari ya Manowari za Hispania

—— Njia iliyotumiwa kuvamia

–– Safari ya kurudi

X Vita

HISPANIA

Lisbon

La Coruña

Santander

FLANDERS

Calais

UHOLANZI YA HISPANIA

UNITED NETHERLANDS

UINGEREZA

Plymouth

London

IRELAND

[Picha katika ukurasa wa 24]

Mfalme Philip wa Pili

[Hisani]

Biblioteca Nacional, Madrid

[Picha katika ukurasa wa 24]

Malkia Elizabeth wa Kwanza

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Dyuki wa Medina-Sidonia ndiye aliyekuwa kamanda wa Manowari za Hispania

[Hisani]

Cortesía de Fundación Casa de Medina Sidonia

[Picha katika ukurasa wa 25 zimeandaliwa na]

Museo Naval, Madrid