Historia ya Maumivu ya Meno
Historia ya Maumivu ya Meno
Kwenye soko lililo katika mji moja wa zamani, tapeli mmoja anasimama na kujigamba kwamba anaweza kung’oa jino bila kusababisha maumivu yoyote. Tapeli mwenzake ambaye anajifanya anasitasita anamsogelea, naye tapeli wa kwanza anajifanya ni kana kwamba anamng’oa jino na kisha anainua gego lenye damu juu ili watu waone. Kuona hivyo, watu wenye maumivu ya meno wanakubali kulipa pesa ili meno yao yang’olewe. Ngoma na tarumbeta zinapigwa ili mayowe ya watu hao yasiwaogopeshe wengine. Baada ya siku chache, nyakati nyingine vidonda hivyo huanza kuoza na kuingiza sumu kwenye damu, lakini tayari tapeli ameenda zake.
SIKU hizi ni watu wachache sana wenye maumivu ya meno wanahitaji kuwaendea wahuni kama hao. Leo, madaktari wa meno wanaweza kutibu maumivu ya meno na hata kuzuia yasing’olewe. Hata hivyo, watu wengi huogopa kwenda kwa daktari wa meno. Kuchunguza jinsi madaktari wa meno walivyogundua njia za kutuliza maumivu hayo, kutafanya tuthamini matibabu ya kisasa ya meno.
Baada ya mafua, ugonjwa ambao umewasumbua watu zaidi ni kuoza kwa meno. Huo si ugonjwa ulioanza majuzi tu. Shairi la Mfalme Sulemani linaonyesha kwamba katika Israeli la kale ilitazamiwa kwamba watu wazee wangepatwa na matatizo yanayosababishwa na kupoteza meno.—Mhubiri 12:3.
Hata Wafalme Waliteseka
Ingawa Elizabeth wa Kwanza alikuwa malkia wa Uingereza, hakuepuka maumivu ya meno. Mjerumani aliyemtembelea na kuona meno yake meusi alisema kwamba hilo lilikuwa “tatizo la kawaida kwa Waingereza kwa sababu walitumia sana sukari.” Mnamo Desemba (Mwezi wa 12) 1578, malkia huyo alikuwa na maumivu makali ya jino yaliyomsumbua usiku na mchana. Madaktari wake walipendekeza jino hilo ling’olewe, lakini alikataa kwa sababu aliogopa maumivu ya kung’olewa. Ili kumshawishi, askofu wa London, John Aylmer, alikubali jino lake ambalo huenda lilikuwa limeoza ling’olewe mbele ya malkia huyo. Hilo lilikuwa tendo la ujasiri kwa sababu mzee huyo alikuwa na meno machache sana!
Wakati huo watu wa kawaida ambao walihitaji kung’olewa meno walimwendea kinyozi au mfua vyuma. Lakini sukari ilipoanza kuuzwa kwa bei rahisi, maumivu ya meno yaliongezeka na kukawa na uhitaji mkubwa wa wang’oaji stadi. Hivyo, madaktari na wapasuaji fulani walianza kupendezwa na kutibu meno yaliyokuwa na matatizo. Lakini, ilibidi wajifunze wenyewe mbinu za kutibu meno kwa kuwa wale waliokuwa na ujuzi walificha siri hiyo. Pia hakukuwa na vitabu vingi vilivyozungumzia jambo hilo.
Karne moja baada ya Elizabeth wa Kwanza, Mfalme Louis wa 14 alitawala Ufaransa. Alisumbuliwa na maumivu ya meno kwa miaka mingi, na mnamo 1685 aling’olewa meno yake yote ya upande wa juu kushoto. Watu fulani wanadai kwamba maumivu hayo ya meno ndiyo yaliyomfanya Mfalme huyo afanye uamuzi mbaya wa kuondoa uhuru wa ibada nchini Ufaransa, jambo
ambalo lilisababisha mateso makali dhidi ya wafuasi wa dini ndogondogo.Jinsi Tiba ya Meno ya Kisasa Ilivyoanza
Maisha ya anasa ya Louis wa 14 yaliathiri jamii ya watu walioishi Paris na kutokeza wataalamu wa meno. Kuwa na sura nzuri kulikuwa muhimu ili mtu aendelee kuheshimiwa kati ya watu wa tabaka la juu. Kulikuwa na uhitaji mkubwa wa meno bandia ambayo yalivaliwa hasa ili kuwa na sura nzuri na si kwa ajili ya kula. Uhitaji huo ulitokeza kikundi kipya cha madaktari, yaani, madaktari wa meno ambao waliwahudumia tu matajiri. Daktari mashuhuri wa meno huko Paris alikuwa Pierre Fauchard, ambaye alijifunza kufanya upasuaji katika jeshi la wanamaji la Ufaransa. Aliwashutumu madaktari wapasuaji ambao waliwaachia watu wasio na ustadi kama vile vinyozi na matapeli kazi ya kung’oa meno naye akawa wa kwanza kujiita daktari wa meno.
Mnamo 1728, Fauchard alikomesha zoea la kuficha siri za matibabu ya meno alipoandika kitabu kuhusu mbinu alizojua. Hivyo, akaja kuitwa “Mwanzilishi wa Utaalamu wa Meno.” Yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kuwaketisha wagonjwa kwenye kiti maalumu badala ya kwenye sakafu. Pia Fauchard alitengeneza vifaa vitano vya kung’oa meno lakini alifanya mengi zaidi ya kung’oa meno tu. Alibuni kekee ya daktari wa meno na mbinu za kujaza matundu. Alijifunza jinsi ya kuondoa mizizi ya meno na kujaza tundu hilo na pia kupachika jino bandia kwenye mizizi. Meno bandia ambayo alitumia yalichongwa kutoka kwa pembe za tembo na yalikuwa na springi ya kuyashikilia. Fauchard alifanya udaktari wa meno kuwa kazi maalumu. Kazi yake ilienea hadi Marekani.
Maumivu ya Rais wa Kwanza wa Marekani
Karne moja baada ya Louis wa 14, George Washington wa Marekani, alikuwa na matatizo ya meno. Kuanzia alipokuwa na umri wa miaka 22 aling’olewa jino karibu kila mwaka. Hebu wazia mateso aliyopata alipokuwa akiongoza jeshi lake. Kufikia mwaka wa 1789, alipokuwa rais wa kwanza wa Marekani, alikuwa na meno machache sana.
Pia Washington aliteseka kiakili kwa sababu kung’olewa meno mengi kuliharibu sura yake, na meno yake bandia yalipachikwa vibaya. Alihangaikia sana sura yake huku aking’ang’ana kujenga sifa mbele za watu akiwa rais wa taifa jipya. Wakati huo, meno bandia yalichongwa kutoka kwa pembe za tembo na hivyo yalikuwa yakitoka kwa urahisi. Wanaume wenye kuheshimika wa Uingereza walikuwa na matatizo kama hayo ya Washington. Inasemekana kwamba walibuni ucheshi wao wa kichinichini wakiwa wamefunga mdomo ili kuepuka kucheka kwa sauti na hivyo kuonyesha meno yao bandia.
Hadithi ya kwamba Washington alivaa meno bandia yaliyotengenezwa kwa mbao si ya kweli. Meno hayo yalikuwa ya wanadamu, pembe za tembo, risasi, lakini si mbao. Huenda madaktari wake walipata meno hayo kutoka kwa watu waliopora makaburi. Pia, wafanyabiashara wa meno wangefuata majeshi na kung’oa meno ya wanajeshi waliokufa na waliokuwa wakikaribia kufa baada ya pigano. Kwa sababu hiyo ni matajiri tu ambao wangeweza kununua meno bandia. Ni katika miaka ya 1850 baada ya kugunduliwa kwamba mchanganyiko wa mpira na salfa ungeweza kutumiwa kushikilia meno bandia, ndipo watu wa kawaida walipoweza kuyanunua. Ingawa madaktari wa meno wa Washington walikuwa wamefanya maendeleo katika taaluma ya meno, hawakuelewa kabisa kilichosababisha maumivu ya meno.
Kwa Nini Meno Huuma?
Tangu zamani watu waliamini kwamba minyoo ndiyo husababisha maumivu ya meno, na wazo hilo liliendelea hadi miaka ya 1700. Mnamo 1890, daktari wa meno Mmarekani, Willoughby Miller,
aliyekuwa akifanya kazi katika Chuo Kikuu cha Berlin, Ujerumani, aligundua ni nini husababisha meno yaoze na kuyafanya yaume. Aina fulani ya bakteria ambayo hula hasa sukari hutokeza asidi inayoshambulia meno. Lakini unaweza kuzuiaje meno yasioze? Jibu la swali hilo liligunduliwa kimakosa.Kwa miaka mingi madaktari wa meno huko Colorado, Marekani walishangaa ni kwa nini watu wengi katika eneo hilo walikuwa na meno yenye rangi ya kahawia. Mwishowe iligunduliwa kwamba tatizo hilo lilisababishwa na maji yaliyokuwa na floraidi nyingi. Lakini walipokuwa wakichunguza tatizo hilo, watafiti waligundua jambo muhimu sana ambalo lingezuia maumivu ya meno: Meno ya watu waliolelewa katika eneo ambako maji hayakuwa na floraidi ya kutosha yalioza haraka. Floraidi, ambayo hupatikana kiasili katika maji ya maeneo mengi, hufanyiza sehemu fulani ya gamba la jino. Maji yasiyo na floraidi ya kutosha yanapoongezwa kiwango cha kutosha, visa vya kuoza kwa meno hupungua kwa asilimia 65 hivi.
Hivyo fumbo likafumbuliwa. Kwa kawaida maumivu ya meno husababishwa na kuoza kwa meno. Sukari huchangia kufanya meno yaoze. Floraidi husaidia kuzuia tatizo hilo. Bila shaka, floraidi peke yake haiwezi kuzuia meno kuoza, lazima mtu apige mswaki na kutumia uzi mwembamba kuondoa uchafu katikati ya meno.
Kutafuta Tiba ya Meno Isiyo na Maumivu
Kabla ya dawa ya kutia ganzi kugunduliwa, matibabu ya meno yalisababisha maumivu mengi. Madaktari wa meno waling’oa meno yaliyokuwa yameoza kwa vifaa vyenye ncha kali kisha wakashindilia chuma chenye moto kujaza tundu. Kwa kuwa hawakuwa na matibabu mengine, waliua sehemu zenye neva kwa kusukuma chuma chenye moto kabisa ndani ya mizizi. Kabla ya vifaa maalumu na dawa za kutia ganzi kubuniwa, kung’oa jino hakukuwa mchezo wa watoto. Watu walikubali kupitia maumivu hayo kwa sababu tu hawangeweza kuvumilia maumivu ya meno yaliyooza. Ingawa mitishamba kama vile kasumba, bangi, na dudai zilikuwa zimetumiwa kwa karne nyingi, vitu hivyo vilipunguza tu maumivu. Je, madaktari wa meno wangepata mbinu ya kutibu meno bila maumivu?
Dawa ya kutia ganzi iliyotengenezwa kutokana na oksidi-nitrasi au gesi ya kuwafanya watu wacheke, iligunduliwa muda mfupi baada ya mwanakemia Mwingereza Joseph Priestley kuitayarisha mnamo 1772. Lakini hakuna aliyeitumia kama dawa ya kutia ganzi hadi mwaka wa 1844. Desemba 10 mwaka huo, Horace Wells, daktari kutoka Hartford, Connecticut, Marekani, alihudhuria mkutano ambao wale waliovuta gesi hiyo waliwatumbuiza watu. Wells aliona kwamba mtu aliyeathiriwa na gesi hiyo alikwaruza mguu wake kwenye benchi ngumu bila kuhisi maumivu. Wells alikuwa mwanamume mwenye huruma na hivyo alihisi uchungu kwa maumivu aliyowasababishia wagonjwa wake. Mara moja alifikiria kutumia gesi hiyo kutia ganzi. Lakini kabla ya kuitumia kwa wengine, aliamua kuitumia yeye mwenyewe. Siku iliyofuata, aliketi kwenye kiti chake na kuvuta gesi hiyo hadi akapoteza fahamu. Kisha daktari mwenzake akang’oa gego lake. Hilo lilikuwa tukio muhimu katika historia. Mwishowe, mbinu ya kufanya upasuaji bila maumivu ilikuwa imepatikana! *
Tangu wakati huo matibabu ya meno yamepitia maendeleo mengi ya kiteknolojia. Hivyo, utaona kwamba leo kwenda kumwona daktari wa meno si jambo la kuogopesha sana.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 22 Siku hizi dawa za kutia ganzi za sindano hutumiwa zaidi ya oksidi-nitrasi.
[Picha katika ukurasa wa 28]
Meno bandia ya George Washington, rais wa kwanza wa Marekani, yaliyotengenezwa kwa meno ya tembo
[Hisani]
Courtesy of The National Museum of Dentistry, Baltimore, MD
[Picha katika ukurasa wa 29]
Picha iliyochorwa na msanii kuonyesha matibabu ya kwanza ya meno kwa kutumia oksidi-nitrasi kutia ganzi, mwaka wa 1844
[Picha zimenandaliwa na]
Courtesy of the National Library of Medicine
[Picha katika ukurasa wa 27 zimeandaliwa na]
Courtesy of the National Library of Medicine