Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Njoo Upumzike Vanuatu

Njoo Upumzike Vanuatu

Njoo Upumzike Vanuatu

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI NEW CALEDONIA

Je, unajihisi umechoka? Ungependa kupumzika? Basi hebu wazia ukipumzika katika kisiwa cha kitropiki chenye hali nzuri ya hewa. Jiwazie ukiogelea katika maji safi, ukitembea katika misitu yenye kuvutia au ukichangamana na watu wa makabila na tamaduni tofauti-tofauti. Je, bado kuna paradiso kama hiyo duniani? Bila shaka! Paradiso hiyo iko katika visiwa vya Vanuatu.

VANUATU ambayo imefanyizwa kwa visiwa vidogo 80 iko kusini magharibi ya Pasifiki kati ya Australia na Fiji. Kulingana na wanajiolojia, miamba mikubwa ya chini ya ardhi iligongana katika eneo hilo na kufanyiza milima mirefu ambayo sehemu yake kubwa iko chini ya bahari. Vilele vya milima mirefu zaidi vilitokea juu ya uso wa bahari na kufanyiza visiwa vyenye mawe vya Vanuatu. Leo kusuguana kwa miamba iliyo chini ya ardhi huchochea matetemeko madogo na kutokeza volkano hai tisa. Watalii wenye ujasiri wanaweza kusogelea lava yenye moto.

Kuna misitu mikubwa ya mvua katika visiwa hivyo. Misitu hiyo ina miti mikubwa ya mibaniani, ambayo matawi yake ya juu huenea eneo kubwa. Pia kuna zaidi ya aina 150 za okidi na 250 za mikangaga chini ya misitu hiyo. Fuo maridadi na miamba iliyochongoka inazunguka maji safi yenye matumbawe na samaki wengi wenye rangi mbalimbali. Watalii wasioharibu mazingira husafiri kutoka sehemu za mbali kuja kuogelea pamoja na wanyama wapole wanaoitwa dugong wanaopenda kucheza na watu katika Kisiwa cha Epi. *

Wala-Watu na Waabudu-Mali

Wavumbuzi kutoka Ulaya walifika Vanuatu kwa mara ya kwanza mnamo 1606. * Visiwa hivi vilikuwa na makabila ya watu wakali, na kula watu kulikuwa zoea la kawaida. Wakati huo, misitu ya misandali, mti wenye harufu nzuri unaopendwa sana Asia, ilikuwa imeenea sana. Wakitambua kwamba wanaweza kupata faida, wafanyabiashara wa Ulaya walikata miti hiyo. Kisha wakaanza kuwatumia wenyeji kama wafanyakazi.

Wenyeji hao walitumiwa kufanya kazi katika mashamba ya miwa na pamba huko Samoa, Fiji, na Australia. Ingawa inasemekana kwamba wafanyakazi hao walikubali kwa hiari kuajiriwa kwa muda wa miaka mitatu, ukweli ni kwamba wengi wao walitekwa nyara. Kuelekea mwisho wa miaka ya 1800 biashara ilipokuwa imepamba moto, zaidi ya nusu ya wanaume katika visiwa fulani vya Vanuatu walikuwa wakifanya kazi katika nchi za ng’ambo. Wengi wao hawakurudi. Karibu wakaaji 10,000 wa visiwa vya Pasifiki walifia nchini Australia, wengi wao wakifa hasa kwa magonjwa.

Pia magonjwa kutoka Ulaya yaliua watu wengi katika visiwa vya Vanuatu. Wenyeji hao hawakuwa na kinga ya kutosha dhidi ya surua, kipindupindu, ndui, na maradhi mengine. Kitabu kimoja kinasema: “Mafua ya kawaida tu yalisababisha vifo vingi.”

Wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo waliwasili Vanuatu mnamo 1839 na inasemekana kwamba mara moja walialikwa kwenye mlo, yaani walichinjwa na kuliwa! Wengi wa wamishonari waliokuja baada yao walikumbana na kisanga hichohicho. Hata hivyo baada ya muda fulani, makanisa ya Protestanti na Katoliki yalijiimarisha kotekote katika visiwa hivyo. Leo, zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa Vanuatu hudai kuwa ni waumini wa kanisa fulani. Ijapokuwa hivyo, mwandishi Paul Raffaele anasema kwamba “wakazi wengi huwaheshimu sana wachawi, ambao hutumia mawe yenye pepo kufanya mazingaombwe ili kumvuta mpenzi mpya, kumnonesha nguruwe, au kumuua adui.”

Pia huko Vanuatu kuna madhehebu ya waabudu-mali. Wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu, wanajeshi nusu milioni wa Marekani walipitia Vanuatu wakielekea vitani katika maeneo ya Pasifiki. Wenyeji walistaajabia mali nyingi za wanajeshi hao. Vita vilipokwisha, Wamarekani hao walifunga virago vyao na kuondoka. Mashine na vifaa vya mamilioni ya dola vilitupwa baharini. Vikundi vya kidini vinavyoitwa madhehebu ya waabudu mali, vilijenga mahali pa kuegesha meli na viwanja vya ndege na kufanya mazoezi wakitumia vifaa bandia ili kuwashawishi wageni hao warudi. Hata leo, mamia ya wanakijiji wa Kisiwa cha Tanna husali kwa John Frum, “masihi Mmarekani wa kuwaziwa tu” ambaye wanadai kwamba, siku moja atarudi na kuwaletea mali nyingi sana.

Utamaduni Mbalimbali

Visiwa hivi vina lugha na desturi mbalimbali. Kitabu kimoja cha watalii kinasema hivi: “Inadaiwa kwamba visiwa vya Vanuatu ndivyo vyenye lugha nyingi zaidi duniani.” Angalau lugha 105 na lahaja nyingi huzungumzwa kotekote katika visiwa hivyo. Kibislama, Kifaransa na Kiingereza ndizo lugha rasmi, ingawa Kibislama ndiyo lugha ambayo hutumiwa katika biashara.

Hata hivyo, kuna jambo moja ambalo halijabadilika katika visiwa hivyo vyote: Kila sehemu ya maisha ya watu hao huongozwa na mila. Hata sherehe ya kale ya uzazi kwenye Kisiwa cha Pentecost ilichochea zoea la watu kuruka kutoka juu sana wakiwa wamefungwa kamba inayonyumbuka miguuni. Kila mwaka wakati wa mavuno ya viazi vikuu, wanaume na vijana huruka kutoka kwenye mnara uliotengenezwa kwa mbao wenye urefu wa mita 20 hadi 30. Kamba-kamba za mmea wa mzabibu zilizofungwa kwenye miguu yao ndizo tu huwazuia wasianguke chini na kufa. Vichwa vya warukaji hao vinapogusa ardhi inatazamiwa kwamba “watarutubisha” ardhi kwa ajili ya mavuno ya mwaka unaofuata.

Ni hivi karibuni tu kwamba vijiji fulani katika Kisiwa cha Malekula vimeanza kuruhusu wageni watembelee huko. Makabila yanayojulikana kama Big Nambas na Small Nambas huishi huko. Waliogopewa sana kwa kuwa zamani walikuwa wakila watu na inasemekana kwamba walikula mtu mara ya mwisho mwaka wa 1974. Pia desturi yao ya kuwafunga watoto wa kiume vitambaa kichwani ili wawe na vichwa “maridadi” virefu, ilikwisha miaka mingi iliyopita. Leo, watu wa makabila ya Namba ni wenye urafiki na wao hufurahia kuwaonyesha wageni utamaduni wao.

Watu Wanaoishi Kwenye Paradiso

Wageni wengi husafiri kwenda Vanuatu kwa likizo fupi. Lakini Mashahidi wa Yehova walifika huko miaka 70 hivi iliyopita ili kuwasaidia watu kiroho. Jitihada za Mashahidi katika ‘sehemu hii ya mbali zaidi ya dunia,’ zimekuwa na matokeo mazuri. (Matendo 1:8) (Ona sanduku “Naacha Kuwa Mraibu wa Kava.”) Mnamo 2006, makutaniko matano ya Mashahidi katika nchi hiyo yalitumia zaidi ya saa 80,000 kuhubiri ujumbe wa Biblia kuhusu dunia itakayogeuzwa kuwa paradiso. (Isaya 65:17-25) Inapendeza kujua kwamba Paradiso hiyo itaondoa mfadhaiko na wasiwasi unaoletwa na maisha ya sasa!—Ufunuo 21:4.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Dugong ni wanyama wa baharini wanaokula mimea wanaoweza kukua kufikia urefu wa mita 3.4 na uzito wa kilo 400.

^ fu. 7 Vanuatu iliitwa New Hebrides kabla ya kupata uhuru mnamo 1980.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]

VISIWA VYENYE FURAHA

Mnamo 2006, visiwa vya Vanuatu vilikuwa vya kwanza katika orodha iliyotolewa na shirika la Uingereza linaloitwa New Economics Foundation. Shirika hilo lilichunguza nchi 178 kuhusiana na furaha, kuishi muda mrefu na kiwango cha kuharibu mazingira. “[Vanuatu] ilikuwa ya kwanza katika orodha hiyo kwa sababu watu wake wana furaha, wao huishi miaka 70 hivi, na hawaharibu sana mazingira,” linasema gazeti Vanuatu Daily Post.

[Picha]

Vazi la kitamaduni

[Hisani]

© Kirklandphotos.com

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]

NAACHA KUWA MRAIBU WA KAVA

Willie, mwenyeji wa Kisiwa cha Pentecost, alianza kunywa kava alipokuwa kijana. Kinywaji hicho kikali kinacholewesha hutengenezwa kutokana na mizizi iliyopondwa ya mpilipili. Kila usiku alirudi nyumbani kutoka kwenye baa ya kava akiwa amelewa chakari huku akiyumbayumba. Madeni yake yaliongezeka. Mara nyingi alikuwa mjeuri na kumpiga mke wake, Ida. Kisha mfanyakazi mwenzake ambaye ni Shahidi wa Yehova, alimtia moyo Willie ajifunze Biblia. Willie alikubali. Mwanzoni Ida alipinga uamuzi wake wa kujifunza. Lakini mwenendo wa mume wake ulipoanza kuwa mzuri, alibadili maoni yake naye akaanza pia kujifunza. Walifanya maendeleo ya kiroho. Baada ya muda, Willie akaacha mazoea yake mabaya. Yeye na Ida walibatizwa na kuwa Mashahidi wa Yehova mwaka wa 1999.

[Picha katika ukurasa wa 15]

 

NEW ZEALAND

AUSTRALIA

BAHARI YA PASIFIKI

FIJI

[Picha katika ukurasa wa 16]

Warukaji hujihusisha katika zoea hili hatari sana katika sherehe ya kale ya uzazi

[Hisani]

© Kirklandphotos.com

[Picha katika ukurasa wa 15 zimeandaliwa na]

© Kirklandphotos.com

[Picha katika ukurasa wa 15 zimeandaliwa na]

© Kirklandphotos.com

[Picha katika ukurasa wa 16 zimeandaliwa na]

© Kirklandphotos.com