Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Wametimiza Fungu Muhimu Katika Maendeleo ya Kitiba”

“Wametimiza Fungu Muhimu Katika Maendeleo ya Kitiba”

“Wametimiza Fungu Muhimu Katika Maendeleo ya Kitiba”

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO

Mashahidi wa Yehova wanajulikana ulimwenguni pote kwa kuchagua matibabu yasiyohusisha damu wanapokuwa na matatizo ya afya. Watu fulani huchambua msimamo huo unaotegemea Biblia. Hata hivyo, gazeti, Reforma la Mexico City ambalo husomwa na watu wengi, lilimnukuu Dakt. Ángel Herrera, daktari mkuu wa upasuaji katika Taasisi ya Kitaifa ya Tiba ya Uvimbe. Alisema hivi: “Mashahidi hawapuuzi mambo. Wala wao si watu wanaoshikilia tu maoni yao bila sababu. . . . [Wao] wametimiza fungu muhimu katika maendeleo ya kitiba kwa kuwasaidia madaktari waone uhitaji wa kuzuia damu isivuje sana.”

Miaka 15 iliyopita, Dakt. Herrera alichagua kikundi cha madaktari na wataalamu wa unusukaputi ambao walifanya upasuaji kadhaa bila kutumia damu. Dakt. Isidro Martínez, mtaalamu wa unusukaputi aliyekuwa katika kikundi hicho alisema hivi: “Mtaalamu wa unusukaputi atatumia mbinu zote ili kuzuia damu isivuje sana. Kwa hiyo, kwa kweli tunaweza kuwasaidia Mashahidi wa Yehova kwa kuheshimu msimamo wao wa kidini.”

Mnamo Oktoba 2006, gazeti Reforma liliripoti kwamba kuna zaidi ya mbinu 30 za matibabu zinazoweza kutumiwa badala ya kutiwa damu mishipani. Matibabu hayo yanatia ndani kuchoma mishipa ya damu, kufunika viungo kwa kitambaa cha shashi ambacho kina kemikali zinazozuia damu kuvuja, na kutumia umajimaji unaoongeza kiasi cha damu. *

Dakt. Moisés Calderón daktari mkuu wa upasuaji wa moyo katika Hospitali Kuu ya La Raza huko Mexico City hufanya upasuaji bila kutumia damu. Alisema hivi katika gazeti Reforma: “Kutiwa damu mishipani kuna madhara yake. Kuna hatari ya kuambukizwa virusi, bakteria, au vimelea. Pia, mwili unaweza kuikataa damu hiyo na kusababisha matatizo ya figo na mapafu.” Kwa sababu ya hatari hizo, Dakt. Calderón alisema hivi: “Sisi huwafanyia upasuaji wagonjwa wote kana kwamba wao ni Mashahidi wa Yehova. Tunajitahidi sana kuzuia uvujaji wa damu, kuokoa damu iliyovuja, na kutumia dawa ambazo humsaidia mgonjwa asivuje damu sana.”

Gazeti hilo lilinukuu Matendo 15:28, 29, andiko ambalo Mashahidi wa Yehova hutumia kuwa msingi wa msimamo wao. Mitume walitoa amri hii katika andiko hilo: “Roho takatifu na sisi wenyewe tumependelea tusiwaongezee ninyi mzigo zaidi, ila mambo haya ya lazima, kuendelea kujiepusha na vitu vilivyotolewa dhabihu kwa sanamu na damu na vitu vilivyonyongwa na uasherati.”

Dawati la Habari za Hospitali katika ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Mexico linaripoti kwamba kuna Halmashauri za Uhusiano na Hospitali 75 nchini humo na wajitoleaji 950 ambao huwatembelea madaktari ili kueleza kuhusu matibabu yanayoweza kutumiwa badala ya damu. Madaktari 2,000 hivi nchini Mexico wamekubali kuwatibu Mashahidi wa Yehova bila kutumia damu. Mashahidi huthamini sana ushirikiano wa madaktari hao ambao pia wamekuwa na ustadi wa kuwasaidia wagonjwa wengine ambao si Mashahidi.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Gazeti la Amkeni! halipendekezi tiba yoyote hususa isiyohusisha damu, kwa kuwa linatambua kwamba huo ni uamuzi wa mtu binafsi.

[Picha katika ukurasa wa 30]

Dakt. Ángel Herrera

[Picha katika ukurasa wa 30]

Dakt. Isidro Martínez

[Picha katika ukurasa wa 30]

Dakt. Moisés Calderón